KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE: Wasomi wahoji uhuru wa kujieleza, utu, usawa na uadilifu wa viongozi

Jamii Africa

Wasomi nchini wamesema kuyumba kwa msingi ya umoja wa kitaifa, uwazi na uwajibikaji miongoni mwa viongozi na wananchi ni kikwazo kwa Tanzania kujenga amani ya kudumu na uchumi wa kati ifikapo 2025.

Akizungumza kwenye  Kongamano la Mwalimu Nyerere lilofanyika katika Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema  baba wa taifa alituachia msingi mzuri wa amani na umoja wa kitaifa na ili nchi ifikie uchumi wa viwanda, misingi hiyo inatakiwa iheshimiwe na kuendelezwa na viongozi.

Amesema Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuboresha huduma za kijamii, kupambana na rushwa, maradhi, ujinga na umasikini kwasababu alijenga umoja wa kitaifa ambao uliwaongoza wananchi katika dira moja ya maendeleo.

“Sasa yako maandishi mengi, diwani ya Mwalimu katika umoja imeandikwa katika vitabu vingi lakini alisema umoja ni moja ya tunu yetu watanzania, ndio iliyotuwezesha kuja pamoja katika vyama”, amesema Butiku.

Ameongeza kuwa ili tunu ya amani idumu na kutawala lazima nguzo za watu,utu,usawa ziimarishwe kwenye jamii na viongozi wawe mstari wa mbele kuwaunganisha wananchi na kutekeleza nguzo hizo kwa vitendo.

“Yote haya ambayo Mwalimu Nyerere alihangaika nayo ameyatoa wapi ? ameyatoa katika maisha ya familia za kiafrika. Katika maisha ya nyumba yako ziko nguzo nne na mzikumbuke; moja wapo watu, wenye utu. Katika hilo la watu na watu ni usawa. Msingi mmoja wa umoja wetu ni kukubali hilo kwamba sisi watu ni sawa na binadamu wote kwahiyo ni sawa tusisahau hilo”, amesema Butiku.

Amebainisha kuwa ili nguzo hizo zisimame imara na amani itawale katika maisha ya kila siku ni muhimu kwa viongozi na wananchi kuheshimiana, kushirikiana na kuimarisha misingi ya katiba na sheria. Pia viongozi watoe uhuru wa watu kujieleza na kutoa maoni juu ya mstakabali wa nchi yao.

“Watu wenye akili, busara, wastaarabu wanaheshimiana. Tatu, watu wote wanapenda kuwa huru. Nyerere alikuwa muumini wa utu wa binadamu na ndivyo alivyo, muumini kabisa sio wa kubabaisha wa umoja. Na usipoamini juu ya binadamu mwenzako ukamuona mjinga sijui nini kwasababu anasema sema sana”, amesema Butiku na kuongeza kuwa,

“Napenda kuwashauri mzingatie hili; ninyi ni watu, watu sawa, watu huru, watu wanaoheshimiana, watu wanaojali demokrasia. Mwalimu Nyerere hakutanguliza kwanza viwanda, alisimamia umoja, uhuru, utu na demokrasia, viwanda ni kazi tu ambazo zipo ndani yake”.

      Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku akizungumza katika moja ya kongamano la wanazuoni.

 

Kwa upande wake,  Mzee Ibrahim Kaduma  amesema amani ndio msingi wa maendeleo ya nchi na kama taifa tunataka kufikia uchumi wa kati ni lazima tuhifadhi amani na viongozi waliopo madarakani wawe ni mfano wa uwajibikaji katika kuwatumikia wananchi.

“Amani ni tunda la imani na itikadi sahihi, matumaini, umoja na ukweli, huruma, haki na upendo na katika hayo yote kuu ni upendo. Ndio maana Mwalimu Nyerere aliandika yanayoitwa maendeleo hayana maana kama hayawezi kuwaendeleza watu na hasa wanyonge”, amesema Mzee Kaduma.

Amesema Mwalimu Nyerere alikuwa mcha Mungu na aliamini katika misingi ya amani na kutenda mema kwa wananchi wake.  Ameongeza kuwa changamoto iliyopo ni kwa viongozi wa sasa kukosa utu, upendo na uadilifu na wanaingia madarakani kwa nia ya kujinufaisha wao na familia zao.

“Kutokana na upendo wake na huruma kwa wanyonge, Mwalimu Nyerere alijatahidi sana mara baada ya uhuru kuonyesha kwa vitendo juu ya umuhimu wa viongozi kuwatumikia watu  na si kuzitumikia nafsi zao”, amebainisha Mzee Kaduma.

Ameongeza kuwa katika siku za hivi karibuni Tanzania imeshuhudia kuyumba kwa misingi ya amani na ameitaka jamii kutafakari na kufanya tathmini za kina juu mstakabali wa taifa katika kuelekea uchumi wa kati.

“Katika miongo hii mitatu tangu Mwalimu atutoke tumeshuhudia kuota mizizi ya unafiki, wivu na kutengwa kwa watu wenye mapenzi mema na mawazo ya Mwalimu Nyerere. Aidha tunashuhudia tamaa zenye kuvuka mipaka za kutafuta fedha na utajiri. Matatizo yetu kuhusu ukosefu wa uadilifu katika taifa letu yamefikia hali mbaya zaidi kuliko hata yale ya ubaguzi wa rangi wa Afrika Mashariki”, amesema Mzee Kaduma.

Hata hivyo, ameshauri kuwa nchi inahitaji mbinu za kisayansi kuchunguza sababu zilizotufikisha hapa na namna ya kushinda; na vijana ndio sehemu muhimu ya kuleta mabadiliko katika jamii ili kuhakikisha viongozi wanazingatia misingi ya uadilifu na amani.

Hoja yake imeungwa mkono na Spika wa Bunge mstaafu, Anna Makinda ambaye amesema vijana  wanapaswa kutafakari  na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kusoma maandiko yake na kuafuta nafasi za uongozi ili kuleta mabadiliko katika jamii.

Ameongeza kuwa vijana waingie kwenye tunu za uongozi pasipo kujali umri walionao ili kuhakikisha mawazo na mtazamo chanya unajengeka katika gurudumu la maendeleo ya taifa.

“Hivi tunavyokongamana kitu gani tunaondoka nacho? Nyinyi watu mnaweza kuwa viongozi tena wakubwa kweli hata Mwalimu Nyerere alikuwa mdogo zaidi, inawezekana!”, ameshauri Anna Makinda.

Akichangia katika kongamano hilo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Prof. Mwesiga Baregu amesema ili amani ipatikane na viongozi wawatumikia wananchi kwa uadilifu, kuna umuhimu wa kukamilisha mchakato wa katiba mpya ya Jaji Joseph Warioba ambayo iliakisi kwa sehemu kubwa fikra na mitazamo ya Mwalimu Nyerere.

“Rasimu ya pili ya Warioba imejengwa katika misingi ya mwalimu Nyerere. Nashangaa chama cha Mwalimu Nyerere (CCM) kinakwamisha mchakato wa katiba unaoenzi fikra za Mwalimu”, amesema Prof. Baregu.

Aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mukandara (kushoto) akiwa na Profesa Issa Shivji katika moja ya kongamano la Mwalimu Nyerere.

 

Akiiwakilisha serikali katika kongamano hilo, Waziri wa Mazingira Muungano, January Makamba amesema changamoto za uongozi bado zipo lakini jamii inatakiwa kurejea misingi  ya uadilifu wa waasisi wa taifa na kujisahihisha pale tulipokesea ili kujiletea maendeleo yaliyokusudiwa.

“Utaribu wa kuwaenzi viongozi wa kitaifa na kuhifadhi kumbukumbu zao ni kudumisha na kuendeleza misingi na falsafa zilizotawala maisha yao na kurithishwa kizazi hadi kizazi. Uhifadhi huo wa kumbukumbu za waasisi hautoshi tu kubaki katika hifadhi bali kuzifanya zikae katika akili na hatimaye kubadili maisha ya watu na katika kizazi cha leo na kijacho”, amesema Waziri Makamba.

Amesema serikali itaendelea kuwaenzi waasisi wa taifa na kulinda urithi wa historia na falsafa zao. Pia amewataka vijana kutumia ujana wao vizuri katika kudumisha amani na umoja wa kitaifa, kujenga mshikamano katika ujenzi wa uchumi wa kati ifikapo 2025.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *