Imeelezwa kuwa watanzania wanashauriwa kuendelea kujihadhari na ugonjwa wa ukoma, licha ya kupungua kwa maambukizi yake katika maeneo mbalimbali nchini.
Tahadhari hiyo inatokana na uchunguzi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto uliofanyika katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 na kubaini kuwa wilaya 6 za Tanzania zilibainika kuwa na vimelea vya ukoma katika ngazi ya jamii.
Katika hotuba ya wizara hiyo kwa mwaka 2018/2019, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alibainisha kuwa, “kwa upande wa ugonjwa wa Ukoma, Wizara ilifanya uchunguzi wa vimelea vya Ukoma katika ngazi ya jamii kwenye Wilaya 6 zenye maambukizi makubwa katika mikoa ya Geita (Chato), Lindi (Liwale), Mtwara (Nanyumbu), Morogoro (Kilombero) na Tanga (Mkinga na Muheza).”
Katika kubaini visa vya ugonjwa huo, wananchi 500 walifanyiwa uchunguzi ambapo watu 54 sawa na asilimia 10.8 waligundulika kuwa na vimelea vya ugonjwa wa ukoma na kuanzishiwa matibabu.
Kati ya hao 500 waliofanyiwa uchunguzi, takriban watu 300 wamepatiwa tiba kinga ili wasisambaze kwa watu wengine au kuathirika zaidi na maambukizi hayo.
Waziri Ummy amesema wizara yake inaendelea na jitihada za kuwaelimisha wananchi jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo. Na wilaya ambazo zina maambukizi makubwa zimewekwa kwenye Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma.
Dalili za wazi ni kuwepo kwa ganzi na vidonda visivyouma kwenye mikono na miguu
Ukweli kuhusu Ukoma
Kwanza ifahamikie kuwa ukoma ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine. Kumekuwa na imani potofu kwa baadhi ya watu wakihusisha ukoma na visa vya kulogwa au kurithi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Ukoma ni ugonjwa wa kuambikiza ambao unaathiri ngozi na mishipa ya fahamu. Ukoma huenezwa kwa njia ya hewa. Chanzo cha maambukizi hayo ni mgonjwa ambaye hajaanza matibabu.
Kuna aina mbili za ukoma. Ukoma hafifu yaani wenye vimelea vichache na huwapata watu wenye kinga kubwa dhidi ya ukoma. Aina ya pili ni ukoma mkali au wenye vimelea vingi na huwapata watu wenye kinga ndogo dhidi ya ukoma. Mgonjwa mwenye aina hii huweza kuwaambukiza watu wengine kwa njia ya hewa iwapo hajapata matibabu.
Dalili za ukoma ni kujitokeza kwa baka au mabaka yasiyo na hisia katika sehemu yoyote ya mwili. Mabaka hayo yanaweza kuwa bapa, yamevimba, hayawashi, hayaumi na kukosa hisia ya mguso.
Dalili za wazi ni kuwepo kwa ganzi na vidonda visivyouma kwenye mikono na miguu. Kuvimba vinundu kwenye masikio na sehemu nyingine ya mwili. Kushindwa kufumba macho na kuishiwa nguvu kwenye misuli na kukamaa kwa viganja vya mikono na miguu.
Kuvimba mwili kukiambatana na homa kali na upofu. Kupoteza kwa viungo vya mwili kama vile vidole vya mikono au miguu. Dalili zote ni dhahiri, ukizipata unashauriwa kufika kwenye kituo cha tiba kilicho karibu yako kwaajili ya matibabu.
Ukoma hutibiwa kwa dawa mchanganyiko zinazojulikana kama ‘Multi Drug therapy’ (MDT). Tiba hutolewa bure katika vituo vyote vya tiba nchini.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya (WHO) Kila mwaka visa vipya 200,000 vya ukoma huripotiwa. Umoja wa Mataifa umeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 22 ambamo kila mwaka kuna visa vipya vya wagonjwa wa ukoma.