Mwanza wamtetea Magufuli, wawaonya wanaopinga nauli Kigamboni

Jamii Africa

BODI ya Barabara Mkoani Mwanza, imewashambulia kwa maneno na kuwaonya Wabunge na wananchi wa Jijini Dar es Salaam kuacha mara moja kumtukana na kumkejeri Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli, juu ya kupandishwa kwa nauli ya kivuko cha Magogoni.

Wamesema, wabunge na wananchi wao hao wa Dar es Salaam, hawapaswi kulalamikia sh. 100 iliyoongezeka hadi kufikia nauli ya sh. 200 na 50 kwa watoto kwa safari moja katika kivuko hicho, kwani vivuko vilivyopo Mwanza nauli zake zinaanzia sh. 400 hadi 800 kwa safari moja, lakini wabunge na wananchi wa Mwanza hawajalalamika.

Hoja hiyo iliyoibuliwa na mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoani Mwanza, Clement Mabina, kwenye kikao cha Bodi hiyo ya Barabara mkoa wa Mwanza, kilichofanyika hii leo kwenye ukumbi wa BoT jijini hapa, iliteka mawazo ya wajumbe karibu wote, kisha wajumbe hao kuanza kuwashambulia kwa maneno wananchi wa Dar es Salaam kuhusiana na hatua yao ya kumbeza Waziri Magufuli kuhusu nauli hiyo mpya.

Lakini wakati hoja hiyo ikizidi kujadiliwa na wajumbe wa Bodi hiyo, Mbunge wa Ukerewe mkoani Mwanza, Salvatory Luyaga Machemli (CHADEMA), alisimama na kupinga ongezeko la nauli ya kutoka sh. 500 hadi 800 kwa kivuko cha Bugorola- Ukara kinachofanyakazi ndani ya Ziwa Victoria, na kusema wananchi wamemtuma kumpinga Waziri Magufuli kwa hilo.

"Hawa wabunge na wananchi wa Dar es Salaam waache mara moja kumtukana Waziri wetu Magufuli anayetoka Kanda ya Ziwa. Kuongezewa nauli ya sh. 100 wameona kubwa mna, mbona Mwanza tunalipa sh. 400 hadi 800 lakini hatulalamiki?.

"Iweje wao waanze kumshambulia na kumtukana Waziri wetu ambaye ni mtekelezaji mzuri sana wa maendeleo?. Tunataka waache kabisa kumtukana Waziri Magufuli na hapa naomba wajumbe tutoe na kupitisha azimio katika hili. Haiwezekani", alisema Mabina kisha kuungwa mkono na wajumbe wote kwa kupiga makofi mezani.

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Mwanza, Mabina, aliwashangaa wabunge wa Dar es Salaam kupoteza muda mwingi kujadili suala hilo la ongezeko la sh. 100, badala ya kushughulikia kero nyingi zinazowatatiza wananchi wao, kupitia ahadi walizowaahidi mwaka 2010.

Katika kikao hicho cha Bodi ya Barabara kilichoketi katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Mwanza, kilikuwa chini ya uenyekiti wake, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Evarist Welle Ndikilo, ambaye baadaye alikabidhi madaraka hayo kwa mbunge wa Jimbo la Busega Wilayani Magu, Dk. Titus Kamani.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Buchosa wilayani Sengerema, Dk. Charles Tizeba alihoji sababu za wabunge wa Dar es Salaam kutaka kuitisha maandamano kwa kupinga ongezeko la sh. 100 lililotolewa na Waziri Magufuli katika Kivuko cha Magogoni, na kuwataka wanasiasa hao washughulikie matatizo ya msingi yanayowakumba wananchi wao na si hilo la sh. 100.

"Hawa wazaramo wasitake kuleta mambo mengine hapa. Sisi huku Wasukuma na Wazinza mbona hatumtukani Waziri Magufuli wakati ndiyo tunaolipa gharama kubwa?. Ina maana watu wanaofanyakazi na kulipwa mishahara hapo Dar wanapinga kulipa 100?.

"Hawajui kwamba kivuko cha Magogoni kinaendeshwa na fedha za vivuko vya Mwanza?. Waache kabisa tabia hiyo, tungefurahi kama wangejikita kutekeleza ahadi zao na siyo vitisho kwa Waziri wetu. Mwanza tunamuunga mkono Waziri Magufuli na asitishike na watu hawa", alisema Dk. Tizeba kisha kuungwa mkono na wajumbe karibu wote.

Awali, Mbunge wa Ukerewe, Machemli alikieleza kikao hicho cha Bodi ya Barabara kwamba: "Ongezeko la kutoka sh. 500 hadi 800 kwenye kivuko hiki cha Bugorola-Ukara ni kikubwa sana. Wazaramo wa Dar es Salaam wanampinga Magufuli kwa kipato chao kinatokana na kuuza madafu, sisi Ukerewe uvuvi".

Hata hivyo, hoja hiyo ya Machemli ilionekana kuungwa mkono na baadhi ya wajumbe, kwani hakuna aliyempinga wakati akisisizitza hoja yake hiyo, kwa madai kwamba ametumwa na wananchi kuja kumpinga Waziri Magufuli kuhusu ongezeko hiyo ya sh. 500 hadi 800 kwa safari moja kule Ukara Ukerewe.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *