Suala la vifaa vinavyohusika na uchimbaji madini hapa nchini limekuwa na utata na mtazamo tofauti kwa kila upande uwe wa wafanyakazi migodini, wamiliki wa vitalu na serikali.
Bwana Hashimu Said Nyambi ni mchimbaji wa tanzanite kwa miaka 15 akiwa Mererani,anasema wanapata maradhi ya vifua mara kwa mara kutoka na na baruti kulipuliwa wakiwa ndani ya migodi na shughuli zote za uchimbaji wakizifanya bila ya kuwa na vifaa stahiki vya kujikinga na vumbi na moshi litokanalo na shughuli za uchimbaji.
“Mchimbaji mfanyakazi wa tanzanite huwa amevaa koti,surualiyakawaida kama jinsi ,viatu wengi wanaraba kofia ya nyuzi za sweta na tochi”alisema bwana Nyambi.
Inapotokea mchimbaji mfanyakazi anaugua kifua bwana Nyambi ameongeza hutibiwa katika hospitali ya Kibong’oto iliyopo katika wilaya ya siha mkoani Kilimanjaro, baada ya kuvuta hewa yenye kemikali kama cotex,fataki,futa na hakuna kuchekiwa afya ukiwa hapa.
Mchimbaji mwingine bwana Elipokea Elisante amesema hawajawahi kupewa mafunzo ya aina yoyote kuhusiana na matumizi ya vifaa na hakushindwa kusifu kampuni ya mwekezaji ya Tanzanite One kwa kuwa na vifaa vyenye ubora kwa wachimbaji wake.
“Baruti inapopigwa moshi wote unatupiga na vumbi linguine tunalipata wakati tunachota mchanga na machepe na huwezi ukafanya kazi hapa bila kuugua ndani ya miezi mitatu.”anakazia bwana Esante.
Bwana John Eliudi alisema mchimbaji mfanyakazi mali yake ni tochi na hakuna kifaa cha zaidi na vumbi lote linalotokana na uchimbaji madini ya tanzanite wanapambana nalo hivyo hivyo.
“Nipo machimbo haya kwa miaka sita, wachimbaji wengi wamepoteza maisha kwa kuwa wakiugua huenda hospitalini na hukutwa mapafu yao yameharibika vibaya” aliongea kwa uchungu bwana Eliudi.
Kwaupande wake Bi Stella Shayo mmiliki wa mgodi kitalu D amesema,kuhusu vifaa kwanza ameiomba serikali kuangalia suala la upandaji wa mara kwa mara wa bei kwani huwagharimu sana,na hata vilivyokuwepo kwa wachimbaji wafanyakazi (wanaapolo) huwa hawapendi kuvaa,nisuala linalohitaji kufuatilia sana,wengi wao huona uzito kuvitumia,na kuongeza kazi kubwa ni kuwahimiza wavitumie.
Bwana Oscar Gunewe,Mjumbe wa bodi ya taasisi ya Haki Madini anasema migodi ya wachimbaji wadogo inakabiliwa na tatizo la technolojia ,vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi na mitaji ya kujiendesha.
Bwana Gunewe ameongeza kuwa upandaji wa mara kwa mara wa bei za vifaa huwaathiri wachimbaji wadogo, sasa hivi (October 2012) seti moja ya vifaa vya kuthaminisha tanzanite imefika shilingi milioni 15.
Eng. Lawrent Mayala ambaye ni mkaguzi wa migodi na afisa madini mkazi, Mererani, amesema kwa upande wa ofisi yake wanawashauri wamiliki wanunue vifaa na wachimbaji kuwahimiza wavitumie hasa wale wanaochoronga miamba,na kaziya ukaguzi hufanyika mara kwa mara katika migodi yote iliyopo mererani.
Mkurugenzi waTANSORT bwana Archard Kalugendo kutoka Wizara ya Nishati na Madini anatolea ufafanuzi kuwa vifaa kuwa ghali ni kutokana na vinakotoka na malipo ya kuingiza vifaa hivyo ndio inafanya viwe juu na ni jukumu la mmiliki wa mgodi kuhakikisha vifaa vinapatikana kwani huagizwa nje ya nchi na watu binafsi.
Bwana Kalugendo ameongeza kuwa kwa upande wa kuchimba,serikali imeiagiza STAMICO hiki ni chama cha wachimbaji madini Tanzania kuanzisha vituo maalum vya kukodisha vifaa kwa wachimbaji wadogo.
“Vifaa hivi vinahitaji wataalam kwani hata wachimbaji wadogo wakipewa hawataweza kuvitumia mpaka wapewe mafunzo hivyo wajiunge katika vikundi kulifanikisha hili”anakazia bwana Kalugendo.
Dr.Kisonga Ridhiki wa hospitali ya rufaa ya Kibong’oto anayehusika na kutibu magonjwa ya kuambukiza alisema kweli tunawapokea wagonjwa wenye matatizo ya kifua kutoka wilaya ya Simanjiro ambako mji mdogo wa Mererani unapatikana.
Dr. Ridhiki aliongeza takwimu za mwaka 2009 za hospitalini hapo, zinaonyesha kati ya wagonjwa 529 wa ugonjwa wakifua kikuu(TB) waliofikishwa hospitalini hapo, kutoka Tanzania nzima asilimia 8.6 walitoka wilaya ya Simanjiro wakijumuisha wachimbaji na wasiokuwa wachimbaji.
Sambamba na hilo taarifa ya kumbukumbu ya hospital hiyo ya mwaka 2011 inayoonyesha waliopokelewa na kulazwa kwa matatizo ya kifua kikuu kutoka mkoa wa Manyara walikuwa 99, wanaume walikuwa 65 wakati wanawake walikuwa 34.
Akielezea hali ya wachimbaji wafikapo hospitalini hapo Dr. Ridhiki amesema wengi huwa wanahali mbaya sana katika mapafu yao kwani yanakuwa yamelika kutokana na vumbi na kemikali za migodini.
Ameongeza kuwa changamoto wanazozipata kwa wachimbaji pindi wanapolazwa wengi hutelekezwa hawapatiwi huduma stahiki na wanaosemekana kuwa waajiri wao, na kuachia jukumu hili kubebwa na hospitali, ila wapo baadhi yao huwahudumia.
Hospitali ya rufaa ya Kibong’oto inayotibu wagonjwa wakifua kikuu,ipo katika wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro,ilifunguliwa tarehe 29 mwezi wa Octoba mwaka 1952 na Lady Twining,baada ya miaka saba ya vita ya pili ya dunia chiniya utawala wa muingereza.
Sera ya madini ya mwaka 1997, ililenga kuanzisha mazingira mazuri ya kiafya na usalama na kuanzisha taratibu za fidia na hata Sera ya madini ya 2009 inasema itahakikisha inaweka mazingira salama katika migodi kwa wachimbaji wadogo.