WANANCHI 464 wa kijiji cha Ikula, wilayani Kilolo mkoani Iringa wamekubali kuongeza mchango wa kusaidia ujenzi wa wodi ya wazazi katika zahanati yao, kutoka Sh 5,000 za mwaka jana hadi Sh 10,000 mwaka huu.
Uamuzi huo ulifikiwa mapema mwaka huu katika kikao cha halmshauri na mkutano mkuu wa kijiji hicho uliopitia matokeo ya utekelezaji wa mpango huo ulioanza Juni mwaka jana.
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Ramadhani Kigwama alisema wananchi hao walichanga Sh 5,000 kila mmoja walipoanza kutekeleza mpango huo.
“Zaidi ya Shilingi milioni mbili tulizopata mwaka jana tulizitumia kuanza ujenzi huo: tunataka ifikapo desemba mwaka huu tukamilishe ujenzi huo ndio maana tumekubaliana na kuongeza kiwango cha mchango mwaka huu,” alisema.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kijijini hapo na kuhudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla, Kigwana alisema wajawazito wanalazimika kusafiri zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma za matibabu katika kijiji jirani cha Mtandika.
“Zahanati yetu haina wakunga: ina mganga mmoja na wauguzi wasaidizi wawili; ukiondoa huduma za kliniki, huduma zingine muhimu kwa wajawazito na watoto lazima zifuatwe Mtandika,” alisema.
Siwema Mgunda (33) alisema mbali na kutopata huduma zote bure katika kituo cha Afya cha Mtandika kama sera ya Afya ya Mwaka 2007 inavyoelekeza, analazimika kutumia zaidi ya Sh 10,000 kukodi usafiri wa pikipiki (bodaboda) kwenda na kurudi kijijini kwake.
“Uchumi wetu unategemea kilimo; ni gharama kubwa kufuata huduma Mtandika; ujenzi wa wodi hii utaleta ukombozi mkubwa kwa wanawake na watoto wa kijiji hiki,” alisema.
Akiwapongeza wananchi wa kijiji hicho, Profesa Msolla alisema ujenzi wa wodi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa 2007 hadi 2017 unaotaka kila kijiji kiwe na zahanati pamoja na kila kata kuwa na kituo cha afya.
Alisema mpango huo ni mojawapo ya mikakati ya serikali ya kutokomeza adui maradhi: chimbuko la mpango huu ni Sera ya Afya ya mwaka 1990 iliyorejewa mwaka 2007 inayoelekeza kuongeza kasi ya kusogeza huduma bora za afya ya msingi kwa kila mwananchi ili kuboresha hali ya ustawi wa maisha na kukuza uchumi wa kipato.
Baadhi ya malengo ya MMAM kama yalivyoelekezwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ni pamoja na kupunguza vifo vya wajawazito kutoka 578 hadi kufi kia 175 kwa kila vizazi hai 100,000: kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka 5 kutoka 112 hadi 45 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai na kuongeza idadi ya wanawake wajawazito wanaohudumiwa na wahudumu wa afya wenye ujuzi, uzoefu na utalaamu wa kutosha kutoka asilimia 46 hadi 88.