Hofu ya kauli mbaya za wahudumu wa afya zaongeza vifo vya watoto na wajawazito

Gordon Kalulunga

HOFU za wananchi wengi kutukanwa au kukejeliwa na wahudumu wa afya wilayani Bunda mkoani Mara kimetajwa kuwa chanzo moja wapo cha vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi za halmashauri ya Bunda hivi karibuni, diwani wa kata ya Nyamang’uta Kalemba Jonathan Ilubi, alisema kuwa wananchi wengi wanadai kuwa wanaogopa kuwapeleka hospitali watoto wao mapema ili kukwepa (kauli mbaya) kutukanwa na wahudumu wa vituo vya afya.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo kuna ongezeko kubwa la vifo vya watoto chini ya miaka mitano na wanapowafikisha katika zahanati, vituo vya afya na hata hospitali wakiwa wamechelewa hugundulika kuwa watoto hao wamepungukiwa damu na wengine hupoteza maisha.

Kwa upande wa vifo vya wajawazito, mratibu wa afya ya mama na mtoto wilayani humo Daines Limo alisema kuwa sababu inayochangia kupungua kwa damu kwa wajawazito ni kutokana na kukosa lishe ya kutosha.

‘’Lishe kwa sasa katika wilaya hii hasa kwa wajawazito ni tatizo ambapo hata samaki hawapatikani kwa wingi kama zamani minofu yake inapelekwa viwandani na wanawake wakila dagaa na samaki minofu inaongeza madini chuma na damu mwilini’’ anasema Daines.

Anasema kwa sasa wajawazito kumi wanaofika kujifungua katika vituo vya afya au hospitalini, kati yao wawili hugundulika kuwa na upungufu wa damu na kutakiwa kuongezewa damu.

Mganga mkuu wa wilaya ya Bunda Dr. Rainer Kapinga anakiri kuwa kuna tatizo la upatikanaji wa damu salama wilayani humo na anazo taarifa za baadhi ya watumishi kuhusika kuuza damu kwa wagonjwa na tayari watumishi watatu wamewajibishwa kutokana na kushiriki kuuza damu.

‘’Utaratibu wa halmashauri tunanunua vifaa vyote vya kutolea damu na kuwekea lakini binadamu wana mambo yao hasa watu wa maabara na tayari watu watatu wamewajibishwa kutokana na suala hilo’’ anasema Dr. Kapinga.

Anaeleza ukubwa wa tatizo hilo la upungufu wa damu wilayani humo kuwa asilimia 60 ya wajawazito hupungukiwa damu kutokana na ukanda huo kuwa ni ukanda wa Maralia.

‘’Asilimia 60 ya wajawazito hupungukiwa na damu kutokana na ukanda huu kuwa wa Maralia na mtu anapokuwa mjamzito kinga zake hupungua’’ anasema Dr. Kapinga.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *