Madaktari Bugando waanza kazi, wakisubiri ahadi ya serikali kutekelezwa

Jamii Africa

MADAKTARI  katika  Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza,  wameungana na wenzao wa nchi nzima kusitisha mgomo na kuanza kutoa huduma ya matibabu, wakisubiri utekelezaji wa ahadi ya serikali na hivyo kupunguza adha iliyowakumba wananchi wa kanda ya ziwa.

Mwandishi  wa  FikraPevu  aliyetembelea hospitali hiyo ameshuhudia  madaktari  waliokuwa zamu  wakiendelea  na kazi  kwa mujibu wa ratiba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza, Dk. Charles Majinge

“Ni kama unavyotuona tunaendelea na kazi  kama kawaida. Mambo mengine tunasubiri  utekelezaji wa  ahadi ya Waziri Mkuu,” alisema daktari mmoja aliyekuwa kazini, lakini hakujitambulisha jina.

Hata hivyo, alisema  baadhi yao hawakuwapo kazini mwishoni mwa wiki maelezo kwamba walikuwa  wamesafiri  nje ya jiji la Mwanza, wakihofia kukamatwa kwa kuhusikana mgomo huo.

 

“Mimi nipo kazini  lakini sidhani kwamba sote  tutakuwa kazini kwa sababu baadhi yetu walikuwa  wamenza kusafiri nje ya jiji.  Kauli ya Waziri Mkuu  Mizengo Pinda kwamba wanastahili kukamatwa nayo  imechangia kuwatisha baadhi ya wenzetu,” alisema

Kwa  upande  wao, baadhi ya wagonjwa waliilaumu serikali kwa kuchelewesha mazungunzo  na madaktari; na hivyo kusababisha madhara makubwa kwa wagonjwa  na serikali kwa ujumla, na wengine walitupia lawama hizo kwa madaktari waliogoma.

“ Mimi binafsi  ninampongeza  Waziri Mkuu  kwa hatua aliyoifikia; lakini kwa upande  mwingine  ninamlaumu  kwa sababu  amefikia  muafaka  ndani ya matatizo makubwa ambayo yametokea  nchini tangu mgomo uanze,” alisema mgonjwa alijitambulisha kwa jina la Sospeter  Nyanda.

Alidai kwa vyovyote vile, hali hiyo  bado itaendelea  kuwaathiri madaktari  kiasi kwamba watafanya kazi  katika  hali ya wasiwasi; hadi   serikali itakapoanza kutekeleza ahadi  yake.

Alipoulizwa  ofisini kwake  juu  ya  mabadiliko hayo, Mkurugenzi Mtendaji  wa Hospitali hiyo, Dk. Charles Majinge, alisema kwamba madaktari  hospitalini hapo  walikuwa  kazini kama kawaida.

“ Mimi nilikuwa safarini; Lakini kwa ufupi ni kwamba madaktari  katika hospitali ya Rufaa Bugando wanaendelea  na kazi kama kawaida,” alisema Dk. Majinge.

Alisema  aliporejea Mwanza alikutana na tangazo  la madaktari hao  katika mbao za matangazo kuhusiana na mgomo wao hadi madai yao yatakapopatiwa ufumbuzi.

Hata hivyo, alidai ni mapema mno  kuthibitisha kwamba madaktari wote  walikuwa wameripoti kazini .

“Siyo rahisi  kusema kwamba madaktari wote wameingia  ama wataingia kazini kwa mujibu wa ratiba za hospitali; ila  nimewaagiza wakuu wa idara  wafuatilie,” alifafanua Mkurugenzi huyo.

Alisema pia kwamba hakuna vifo  vilivyotokea hospitalini hapo kutokana na mgomo huo, bali taarifa aliyoikuta inaonesha kuwepo kwa vifo  kutokana  na masuala ya kawaida.

“Kwa mfano kifo ninachokina hapa ni cha mama mmoja ambaye alifia wodini  baada ya kuvuja  damu nyingi  mara baada ya kujifungua   katika hospitali ya Butimba. Taarifa inaonyesha kondo la nyuma halikutoka na hivyo akavuja damu nyingi,” alisema Dk Majinge.

Habari hii imeandaliwa na Juma   Ng’oko, Mwanza

2 Comments
  • Huyu Dk Majinge huwezi kumsikia wala kumuona kwenye MEDIA wakati wa Mgomo unaendeleaanapenda kuonekana msafi anakimbia na kuwaachia ofisi wasaidizi wake, na kusingizia kuwa alikuwa nje ya ofisi natabiri tar 7/3 hataonekana akitoa statement mpka mgomo iushe!!

  • Kifo cha huyo Mama si cha kawaida probably madakatri hawakuwa kazini, Postpartum hemorrhage (PPH) due tu Retained Placenta!!! hata kama ni Placenta Accreta, Yeye kama Obstetrician he should have known that huyo Mama hakutakiwa kufa(Maternal death was preventable) kama Madaktari wangekuwa kazini, na kama Daktari yeyote angehusika najua My GOOD old friend angefanya maisha ya huyo daktari kuwa Magumu sana!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *