Hakimu Mwanza alalamika nyumba zake kuwekwa ‘X’

Jamii Africa

BAADHI ya wakazi wa jiji la Mwanza, akiwamo Hakimu mmoja wa Mahakama ya Mwanzo wamelalamikia maamuzi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kuwekewa alama za ‘X’ katika nyumba zao bila kushirikishwa, wakielekeza malalamiko hayo kwa Meya Josephat  Manyerere  (Chadema) wakidai kwamba anatumia vibaya madaraka yake kwa kukiuka taratibu sheria za ardhi.

Hii ni mara ya pili baada ya wakazi wa jiji hilo kumtuhumi Meya Manyerere kwamba alishirikiana na waumini wenzake wa kanisa la Waadventista  Wasabato (SDA) Majengo katika mtaa wa Mabatini Jijini hapa kujenga  jengo la gorofa la Kanisa hilo bila vibali.

Meya wa Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere

Habari zilizoifikia FikraPevu zinadai  kwamba  safari hii,  uongozi wa jiji chini ya Meya huyo umetoa  maamuzi  ambayo pamoja na mambo mengine, yameibua  manung’uniko  pamoja na hofu  kuhusiana  na  ardhi miongoni mwa wakazi wa mtaa wa Bwiru-Mnarani, wilaya ya Ilemela Jijini  hapa.

“ Sisi ni watu  wa kuagizwa tu; sasa wewe ungelifanyaje iwapo Meya  anakupigia simu na kukuagiza “ alidai  mmoja  wa wafanyakazi  wa idara ya ardhi, kwa sharti la kuotajwa jina.

Alidai mara  kadhaa, Meya  alikuwa akiwapigia simu  ili wakaweke  alama ya X katika baadhi ya nyumba  zilizoko katika mtaa  wa  Bwiru-Mnarani.

Baadhi ya wakazi wanadai kwamba kuna harufu ya ukabila na udini hatua  ambayo  inadaiwa  kuongeza  idadi ya  malalamiko, migogoro pamoja na  kesi  zinasababishwa na tabia ya   ukiukwaji  wa taratibu  na sheria  ya ardhi  jijini.

“ Kwa  mfano,  wiki  iliyopita Meya  alishinikiza  watumishi wa halmashauri  ambao  walifika katika mtaa wa Bwiru-Mnarani  na kuweka alama ya  X  katika baadhi ya nyumba, ikiwemo  nyumba za  Mheshimiwa  Hakimu, Isaack  Mbolile,” kilidai chanzo chetu cha habari kwa  sharti la kutotajwa jina.

Habari zinasema wamiliki wa nyumba hizo bado hawajaelezwa sababu za kuweka alama za X Katika nyumba zao.

Inadaiwa kuwa nyumba zilizowekwa alama ya X ziko nje ya eneo la barabara kuu, kwa mujibu wa maelezo pamoja na ramani iliyooneshwa kwa  wananchi hao, zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Habari zinadai  kwamba kila mwaka  wamiliki wa nyumba zilizowekwa alama ya X wanalipa kodi ya majengo kama kawaida.

“Sasa inakuwaje  jiji  wapokee  kodi ya nyumba ambazo ziko ndani ya hifadhi ya barabara; tena kwa zaidi ya miaka  mitano sasa” kilidai chanzo cha habari.

Alipoulizwa, Manyerere alikiri  kupokea  malalamiko kutoka  kwa  baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Bwiru-Mnarani .

Hata  hivyo, Meya huyo hakuwa tayari kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo huku akisisitiza kwamba yeye  hafanyi kazi kwa itikadi za dini na ukabila.

Alikiri pia kwamba  jiji limeagiza nyumba hizo ziwekewe  alama ya X, wakati ofisi yake ikiendelea  kufanya  madai yaliyofikishwa ofisini kwake.

“Ni kwamba mimi nimeletewa  malalamiko ofisini  kwangu ; na siyo lazima  niwasiliane na wenye  nyumba kabla ya kuweka  alama ya X  katika  nyumba zao,” alisema  Manyerere.

Alidai  yeye  ana uwezo wa kufanya  maamuzi yoyote  juu ya  malalamiko yanayofikishwa ofisini kwake.

“Unajua, mabaraza ya ardhi yana  kazi zake; na pia  mimi ninaweza kuchukua  uamzi wowote ninaoona inafaa dhidi ya malalamiko yanayonifikia   ofisini  yangu “ alisema

Kaimu Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji, Victre Mashamba alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yeye siyo msemaji.

Suala hilo ninalifahamu; lakini mimi siwezi kulizungumzia kwa vile siyo msemaji wa Halmashauri. Kamuulize  Meya ama Mkurugenzi Mtendaji,” alisema  Mashamba.

Alipoulizwa, Makamu mwenyekiti wa mtaa huo, Misana Mwanga, alikiri juu ya kuwepo kwa  suala hilo .

Alikiri pia kwamba yeye  alikuwa  amefuatana na watumishi wa  Halmashauri ya Jiji la Mwanza,  wakati zoezi hilo likitekelezwa.

“Ni kweli ninafahamu kwamba nyumba hizo ziko nje ya eneo la barabara  na kwamba mimi nilikuwepo wakati jiji wanaziorodhesha nyumba ambazo zimepitiwa na barabara  ya mtaa,” alikiri makamu mwenyekiti  huyo.

Alidai kuwa   hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu aliombwa na wafanyakazi wa Jiji ili awaoneshe ziliko nyumba walizokuwa wameagizwa kuziwekea  alama ya X.

Alikiri pia kwamba  nyumba  karibu zote  katika mtaa  huo zimejengwa bila vibali, isipokuwa nyumba  za biashara.

“Mimi  ninajipanga  kwenda mahakamani;… kwamba  kitendo cha kuweka alama za X  katika nyumba  zangu  ni cha kunidharirisha mbele ya jamii. Sijashirikishwa  kabla ya hatua hiyo; na pia  wakati wote nimelipa  kodi za majengo kama kawaida” alisema  mmojawapo ya watu ambao nyumba zao zimewekwa alama ya X,” alisema Issack Mbolile,  ambaye ni hakimu Mahakama ya Mwanzo Usagara, Msungwi  mkoani hapa akisisitiza kuchukua hatua dhidi ya walioweka alama za X katika nyumba zake.

Alidai ramani aliyonayo inaonesha kuwa viwanja vyake viko nje ya eneo la baarabara  na kwamba njama hizo zimefanywa na watu wachache ambao wanalenga kumchafua .

Habari hii imeandikwa na Juma  Ng’oko, Mwanza

1 Comment
  • Mimi ni mkazi wa mwanza, mzee wangu ana kesi na mpangaji wake kwa muda wa miaka mitano sasa ankaa kwenye nyumba bila kulipa kodi na kesi iko mahakama ya ardhi na inaukumiwa visivyo kulingana na hakimu na mshitakiwa wanavyopanga. je mtanisaidia vipi kujua mwenendo wa sheria za haki za kitanzania katika kumiliki haki za binaadam bila kukiuka haki za kibinadam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *