Maangamizi ya samaki asili Ziwa Viktoria

Eva-Sweet Musiba

Furu  samaki ambao kwa sasa ninaweza kukueleza tu kwa wajihi wake kama nilivyosimuliwa, akiwa na ukubwa wa kati ya  dagaa na sato wadogo, wamebaki kuwa historia kutokana na kazi ya binadamu.

Samaki huyu ambaye alikuwa anapatikana kwa wingi na kuwezesha chakula katika eneo kubwa la kandokando  mwa Ziwa Viktoria maeneo ya Musoma ametoweka kabisa na ukimpata ni sawa na kuona nyota ya jaha.

Hakuna maelezo muafaka kwanini wametoweka. Lakini wapo wanaoamini juu ya kuliwa kwao kwa samaki hao na sangara waliopandikizwa ziwani humo na wapo wanaoamini kwamba mvua zilizokuwa zinanyesha wakati wa uhuru ndio ziliangamiza uzazi wa furu.

Kutoweka kwa samaki unaoweza kuwaita wenyeji wa Ziwa Victoria hakuhitaji kuwa na ushahidi kwani katika mialo yote ya wilaya ya Musoma na hata wa kijiji cha Busekela (ambako mimi ndiko kwangu)  samaki hawa watamu ambao unasimuliwa na vikongwe hawapo, wanaonekana sangara na sato na hata sangara wenyewe nao wanaanza kuwa wa kubahatisha.

Pamoja na ukweli kuwa hakuna taarifa rasmi za kitafiti  kwa wananchi nini kimejiri kwa samaki hao, wakongwe wa eneo hili wanasikitishwa na mazingira hayo wakisema wamepoteza moja ya vitoweo vitamu ambavyo havina mfano.

Kikongwe, Nyamumwi Tete (84) Mkazi wa  kitongoji cha Mwisiba-Buira Kijiji cha Busekela, Wilaya ya Butiama alisema kuwa furu na aina nyingine 13 za samaki  aliokuwa amezoea kuwaona tangu kukua kwake kwa sasa hawaoni.

“Tangu kukua kwangu nimeona samaki aina nyingi ambazo sasa sizioni, samaki hao walikuwa watamu sana, wenye ladha nzuri na mwonekana mzuri lakini kwa sasa mhh sizioni, nakula  chengu (Sangara),ambaye hana ladha na anakifu kula pia ana harufu kali kwa wale wenye umri mkubwa” anasema bi Nyamumwi.

Anasema pia miaka ya karibuni alienda kununua samaki aina ya sangara anashangazwa kutowaona hata hao sangara wakubwa na hajui tatizo liko wapi, anashindwa kuelewa.

Anakumbuka kuwa kabla ya uhuru kulikuwa na samaki aina ya furu ambao walikuwa wamegawanyika mara mbili. Walikuwapo furu wakubwa  na wadogo wadogo ambao kwa sasa furu aina ya mbinga ambao ni wakubwa  hawaonekani, kulikuwa pia na sato, ambao pia walikuwa wa aina mbili sato mwekundu aitwaye nyamurungu au Imongo kwa  lugha ya kijita.

Anasema amekuwa akishuhudia kutoweka samaki mmoja hadi mwingine na hata ya baada ya samaki hao kutoweka walikuja samaki wengine waitwao singida ambao anasema walikuwa na rangi nyeusi kama chungu na walikuwa wafupi  ambao pia kwa sasa anapatikana mmoja mmoja kwa nadra sana.

“Nikimpata samaki huyo huwa moyo wangu unafurahi sana” anasema bi Nyamumwi ambaye hakusita kusema kwamba huenda Mungu ndiye anawaangamiza na kuleta wengine.

Aliongeza kuwa baada ya kutoweka kwa aina hizo za sato, kwa sasa kuna sato mweupe ama wa kijivu ambaye naye hapatikanani kwa wingi kama hapo awali.

Kikongwe huyu alikuwa na maelezo mengi kuhusu samaki ambao amekutana nao na kutoweka. Aliwataja samaki wengine waliotoweka na maumbile yake kuwa ni njegele ambaye alikuwa na magamba huku akifanana fanana na Sangara, ngalala na sarakuyu ambao  ni jamii ya ningu ambao  walikuwa na miba mingi, mayai makubwa na walikuwa pia na magamba,  mbete (domodomo) ambaye alikuwa na magamba machache na mdomo wa kuchongoka pia anapapasi, nembe (matusi ya Mwanza) ambao wana mfupa mmoja.

Samaki hawa katika Wilaya ya Butiama wametoweka ila wanapatikana kwa uchache sana mkoa wa Mwanza. Ningu pia wanapatikana kwa uchache katika Wilaya ya Bunda kipindi cha mvua za masika,kwani wanakuwa wanatokea kwenye mito kuingia ziwani.

Wengine ni ngere (gogogo),  imamba (kamonga), mumi na mbofu ambao wao hawana magamba na Soga.

Katika kipindi hiki cha utafiti bado hakuna muktadha unaoeleweka wa kutoweka kwa samaki ingawa wasomi wamekuwa wakiitaja uvuvi usiokuwa na mpangilio kuwa ndio sababu. Wanasema samaki wanavuliwa pasipo taratibu huku kukiwapo ongezeko la watu wanaovua samaki bila kufuata taratibu zinazotakiwa.

Taasisi  ya Utafiti wa uvuvi Tanzania(TAFIRI)  nayo haijaweka bayana tafiti zake  zenye lengo la kuueleza umma namna bora ya kurejesha samaki hawa ambao watu wanahistoria nao huku wakienda sanjari na samaki wakubwa wenye kutafutiwa soko Ulaya.

Hakuna data za kutosha kuhusu uvuvi Ziwa Victoria na wakati wa utafiti huu kujua kulikoni Maofisa wa tafiri walikuwa na majibu mengine ya kitaifa na wala si ya kikanda.

Mtafiti Mwandamizi  wa  Uvuvi  wa Taasisi  ya Utafiti wa uvuvi Tanzania  (TAFIRI), Kituo cha Sota Wilaya ya Rorya,Philemon Nsinda  alisema tatizo la uvuvi kupita kiasi cha uwezo wa samaki kuzaliana ikichangiwa na usimamizi hafifu wa uvuvi ni miongoni mwa mambo ambayo yamechagia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria.

Anasema samaki anaowafahamu waliotoweka ziwani ni kama: Oreochromis esculentus, Barbus altianalis na Furu aina  mbalimbali ambao kwa sasa hana picha zao mfano Scale na baadhi ya  samaki fish eater haplochromines.

Kwa maneno yake anakiri: “Samaki hawa walikuwa kitoweo kitamu kwa takriban makabila karibu yote ya Kanda ya ziwa Victoria.Kutoweka kwa samaki hawa katika Ziwa kumeacha ombwe la kiikolojia, na kupungua kwa samaki wenye kutoa protini na kipato kwa jamii inayozunguka Ziwa Victoria”.Alisema Nsinda.

Inawezekana kuwarejesha?

Lengo kuu la TAFIRI ni kufanya tafiti kwa kuzingatia mahitaji katika sekta ya uvuvi na kutoa ushauri elekezi kwa wadau na watu wengine wanaohitaji ushauri kuhusu uvuvi.

Kati ya mwaka 1998 na 2004 palifanyika tafiti za kuwezesha kurejesha samaki waliotoweka Ziwani chini ya Mradi wa LVEMP I. Mpango unaofanyika kwa sasa ni kufanya tafiti na kutoa mapendekezo na ushauri serikalini wa namna zitakaosaidia kuwalinda samaki walio katika hatari ya kutoweka.

Nilipata kuuliza maswali kwa mtaalamu huyo,Je wanaweza kupandikizwa katika mabwawa na kurejeshwa tena ama  species zake haziwezi kupatikana tena?

Samaki waliotoweka wanaweza kupandikizwa katika vitaru maalum vya kufugia samaki na baadae kurejeshwa ziwani. Aidha, kuna samaki waliotoweka/waliokatika hatari ya kutoweka ziwani mfano Oreochromis esculentus na Oreochromis valiabilis wanapatikana kwenye maziwa madogo (Satellite lakes) yaliyo ndani na Bonde la Ziwa Victoria.

Oreochromis-esculentusOreochromis esculentus (Graham, 1928)

 Nini kifanyike ili vizazi vijavyo viweze kufaidi samaki ambao kwa sasa wapo ambao pia wana hatari ya kutoweka? Hili lilikuwa swali la msingi na majibu yake kutoka kwa mtafiti yalikuwa jumla.

Alisema tafiti za kujua hali ya mazingira, chakula na maeneo ya mazalia na makulia ya samaki hao zinapaswa kufanyika ili kubaini mahitaji ya samaki hao. Wakati huo msisitizo ukiwekwa juu ya uvuvi endelevu wa samaki na ulinzi wa mazalia na makuzia yao.

Akimzungumzia sangara mtafiti huyo alisema kwamba aina hiyo ya samaki imechangia tu kutoweka kwa baadhi ya samaki katika ziwa na si busara kutua mzigo wote kwake pekee.

Alisema kuna sababu nyingine kama uvuvi kupita kiasi cha uzalianaji, matumizi ya zana haramu za uvuvi (kokoro, sumu, Ndina, Nyavu za makila zenye macho madogo, uvuvi wa katuli, uharibifu wa mazingira, na mabadiliko yanayoendelea ya tabia nchi).

Barbus-altianalisBarbus altianalis (Boulenger, 1900)

Mradi maalumu kitaifa

Wakati hakuna taarifa rasmi ya namna ya kufanya kurejesha samaki wa asili wa Ziwa Victoria utafiti uliofanywa kitaifa wa samaki aina sato umebainishwa kwamba unaweza kuongeza kipato kwa wananchi wengi wa Tanzania.

Kitaifa kuna aina 26 za samaki aina ya sato kati ya aina 50 zilizopo duniani.

Hiyo imebainika katika utafiti kuhusu aina za samaki jinsi ya kuweza kukuza jamii hizo uliofanywa na Mradi maalum unaotumia vinasaba kutunza Rasilimali za Samaki wa maji baridi unaofanywa chini ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kwa miaka mitatu.

Akieleza matokeo ya utafiti wa miaka mitatu uliofanywa na mradi huo kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya Bangor na Bristol vya Uingereza, Mtafiti Mkuu wa TAFIRI,Dk.Benjamin Ngatunga aliyeongoza utafiti huo amesema kuwa kila samaki wanatakiwa kukuzwa katika jamii iliyopo katika ziwa,mto au bonde eneo husika.

Alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa samaki nchini wataongezeka ikiwa  aina iliyopo katika bwawa la Mtera  yenye uwezo wa kufugwa katika maji ya aina tofauti itafugwa kwa wingi nchini.

Alisema katika mradi huo samaki huyo wa Mtera alikuzwa Mbalali ,Rufiji na hata  maji chumvi na akaonekana anakubaliana na mazingira.

“Kwa sasa tumekuwa tukifuga aina moja ya samaki wa sato wa mkoani mwanza bila kupa mafanikio kwani tumebaini aina hiyo inakula sana na kuzaa na kila samaki jambo ambalo ni vigumu kukuza aina hiyo”alisema

Alisema kati ya matokeo waliyopata ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuongeza idadi ya samaki ni kufuga sato wanaopatikana Mtera katika maeneo tofauti hata maji ya chumvi.

Nini  kifanyike? (ushauri)

Kama kumefanyika utafiti wa sato nini kinanashindikana kumrejesha samaki mtamu wa Ziwa Victoria Furu? Labda fedha nyingi zinatakiwa kuangalia hili, lakini mpaka hapo itakapotekelezeka inaonekana sato ndio anaweza kurejeshwa lakini si furu wa Ningu.

Naye Charles Mafwere(60) ambaye ni mvuvi mpaka sasa anadai kuwa kutoweka kwa samaki hao ni kunatokana na kuwepo kwa samaki aina ya sangara ambaye anakuwa anapata kitoweo kwa samaki wanaokua, pia ongezeko la watu limekuwa kubwa kulingana na mahitaji ya watu, vilevile uvuvi haramu ni chanzo kikubwa cha kusababisha kutoweka kwa samaki hao pia ametoa angalizo kuwa serikali isipochukua hatua kali kwa wavuvi haramu kuna hatari kubwa ya kutoweka kabisa kwa samaki wachache waliopo.

Sheria ya uvuvi na 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 na sera ya uvuvi ya mwaka 1997  haijakidhi lengo kuu la kulinda,kuendeleza na kukuza usimamizi endelevu wa rasilimali ya uvuvi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo kwani samaki wanaendelea kutekeketea na jitihada kidogo sana zinafanyika ili kulinda samaki wengine wasitoweke.

Uvuvi ni shughuli muhimu inayowapa kipato jamii ya wavuvi wanaoishi kandokando ya ziwa ambapo jumla ya wavuvi 25,792 sawa na asilimia 1.5 ya idadi ya wakazi wa Mkoa wa Mara wamepata ajira kutokana na shughuli hiyo,sanjali na chakula,pia uvuvi unaingiza kipato kikubwa kwa Taifa pia Mkoa.

Katika kipindi cha mwaka 2013 jumla ya nyavu haramu 18,780 zilikamatwa, yakiwemo makokoro ya sangara 473, nyavu za timba 5,295, nyavu za makila zenye ukubwa wa macho chini ya inchi sita 12,967 na nyavu za dagaa zenye ukubwa wa macho chini ya milimita nane zipatazo 45,pia samaki wachanga aina ya sato kilo 5,653 na sangara kilo 17,081.

Jumla ya kilo 3,600,742 na mazao mbalimbali ya samaki  yenye thamani ya dola za kimarekani 23,982,196 yalisafirishwa kwenda nje ya nchi.

Katika oparesheni iliyofanyika jan 4 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa aliongoza uteketezaji wa wa zana haramu za uvuvi zipatazo 13,538 zenye thamani ya sh. 341,038,000 kwa mujibu wa kanuni ya uvuvi ya mwaka 2001 kifungu cha 66 (i)(a) (b)(e)(f)(g)(h)(k) ambavyo vinapiga marufuku kutengeneza, kuhodhi, kuuza ,kulimiki na kutumia zana hizo katika uvuvi ndani ya ziwa viktoria.

2 Comments
  • mimi nimeupenda sana huo walaka nawapongeza sana cha msingi ni serikali ituajiri sisi maafisa uvuvi ili tukalinde rasilimali za uvuvu kwa ajili ya kizazi cha sasa na baadae pia

  • aksante sana nimewajua zaidi samaki wa maji baridi(fresh water) manake niliwajua zaidi wa maji chumvi(sea water) kutokana na kusoma feta kampas ya mbegani na vitendo nilifanyia zaidi dar na tanga thanks for more lesure

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *