Wakati nchi yetu ikiwa katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya njia za uzazi wa mpango, bado baadhi ya wanawake wa vijiji vya Yombo na Kongo wilayani Bagamoyo, hawafahamu kama Kondom ni njia mojawapo ya kupanga uzazi.
Sauda Ramadhan (40) mkazi wa kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo wilaya ya Bagamoyo, anasema hawezi kumshauri mumewe atumie kondom kama njia ya kupanga uzazi kwani anaamini kondom haiwezi kuzuia ujauzito.
Sauda ambaye ana watoto saba kwa sasa anasema ana mpango wa kutumia njia za uzazi wa mpango, kwani tayari ameshakuwa na watoto wa kumtosha, lakini akaweka wazi kwamba kondom si njia mojawapo atakayoitumia.
Naye Asha Shaaban mkazi wa kijiji cha Yombo, anasema anaogopa kumwambia mumewe atumie Kondom kama njia ya kupanga uzazi kwani, amewahi kuambiwa kwamba kondom huwa inabakia ndani ya uke wa mwanamke, na kumsababishia madhara, na haiwezi kutoka mpaka afanyiwe upasuaji.
Amina Salum, mkazi wa kijiji cha Yombo kata ya Yombo wilaya ya Bagamoyo, anaona kwamba ni ngumu kutumia kondom kama njia ya kupanga uzazi, kwani ni lazima atumie mwanaume, na kukiri kwamba kwa uzoefu wake wanaume wengi hasa walioko katika ndoa hawapendi kutumia kondom.
Mganga mkuu wa zahanati ya Yombo, Donald Malamsha anasema kuna umhimu wa kuwepo tena kwa kondom za kike, kwani kuwepo kwa kondom za kiume pekee, kunawanyima wanawake uhuru wa kufanya maamuzi katika kupanga uzazi.