POLISI wageuka ‘Majambazi’

David Azaria

POLISI wa kituo cha Mavota kilichopo ndani ya eneo la kijiji cha Mavota, wilayani Biharamulo, katika mkoa wa Kagera, wanaolinda Mgodi wa Tulawaka wanakabiliwa na tuhuma nzito.

Wananchi wanatuhumu polisi hao kupiga, kunyang’anya fedha na mali kwa wananchi wanaojipenyeza na kuingia ndani ya mgodi na kuchukua mawe ya dhahabu.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wanasema wamechoshwa kukaa kijijini hapo bila kazi kutokana na kuzuiwa kuchimba dhahabu,huku wakishuhudia watu wengine kutoka nje ya kijiji wakipita katikati ya kijiji hicho na kwenda mgodini kuchukua mawe ya dhahabu.

“Tulichoamua sasa na sisi tunaingia tu humo ndani na kuchukua mawe ya dhahabu,na kutoka nayo,lakini bado cha ajabu hawa askari ambao ni watanzania wenzetu wanatuvizia wanatukamata na kisha kutunyang’anya…’’ anasema mmoja wa wachimbaji hao ambaye anaomba jina lake kuhifadhiwa.

Anasema kwanza kupenya hadi kuingia ndani ya mgodi ni kazi kubwa kutokana na ukuta wa zege uliozungushiwa katika mgodi huo,kwa ajili ya kuzuia wahalifu kuingia kwa urahisi.

Anaeleza kuwa wamekuwa wakipanda ukuta huo wenye urefu za mita zipatazo 25 kwenda juu,na kushuka ndani kisha kuingia ndani ya mgodi na kuchukua mawe ya dhahabu.

DSC00651
Huu ndio Mlango wa kuingilia ndani ya mgodi wa Tulawaka ulioko chini(UnderGround) ambapo vijana wanashuka na kupanda tena kwa ajili ya kuiba mawe ya dhahabu,ambayo baadaye wananyang'anywa na polisi.

Anasema zamani walikuwa wanachimbua ukuta huo na kuingia kupitia mashimo,lakini walikuwa wakitumia nguvu nyingi na muda mwingi katika kuchimbua kutokana na ugumu wa zege,na ndipo baadaye wakabuni njia hiyo ya kukwea ukuta.

Wengi wa Vijana waliozungumza na Mwandishi wa Makala haya ambao waliomba kuhifadhiwa majina yao kwa usalama wao isipokuwa Zablon Marco,Bundala Walwa na Emmanuel Limbu,wanasema wamekuwa wanapenya na kuingia ndani ya mgodi huo wenye urefu wa zaidi ya mita 1000 kwenda chini,kwa ajili ya kuokota mawe yenye dhahabu.

“Kule chini ni mahali hatari sana tunatembea kwa kufuata ukuta uliotengenezwa maalum wakati wa kuchimba shimo(Underground),na unapotoka huko ukiwa na kiroba chako kidogo cha mawe lakini yenye dhahabu nyingi unaporwa na polisi….’’anasema Walwa.

Anaongeza kuwa kuna wakati ambapo polisi wamekuwa wakiwaacha wakati wanaingia,na wanawavizia wakati wa kutoka na wanapowakamata wanawapekuwa na wakishawapora mawe yao ya dhahabu wanawaachia.

Hali hiyo inadaiwa kuongeza uhasama baina ya vijana hao pamoja na polisi ambapo kuna wakati vijana wanalazimika kuwashambulia polisi na kuwaua ama kuwapiga.

Kwa mfano Machi 21 mwaka jana wachimbaji wadogo waliokuwa wameingia ndani ya eneo la mgodi huo na kuchukua mawe ya dhahabu walimuua askari polisi.

Kuuawa kwa askari huyo aliyetambuliwa kwa jina la PC Dickson Mwenye namba G:2626 na kisha kumpora Bunduki aina ya SMG na risasi 46,kulija kutokana na askari huyo kutaka kuwapora mawe yao ya dhahabu.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mavota Paschal Joakim anasema kumekuwepo na malalamiko ya mara kwa mara ya wananchi kuporwa mali zao na Polisi,lakini anapokwenda kuhoji anajibiwa kwamba wameiba ndani ya mgodi.

Kijiji cha Mavota ni sehemu ya msitu wa hifadhi. Kituo cha polisi kipo kati ya makao makuu ya kijiji na mgodi wa Tulawaka unaomilikiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick Gold Corporation (Barrick).

Ni kilomita tano (5) kutoka makao makuu ya kijiji hadi mgodi wa Barrick – ukipitia mbuga yenye miti na nyasi ndefu.Mpaka kati ya mgodi wa Tulawaka na kijiji ni wa seng’enge.

Lakini dhahabu pia haziko kwenye shimo moja. Eneo lote ndani na nje ya seng’enge na hasa ndani ya Hifadhi ya Msitu uliozunguka mgodi linasemekana kuwa na madini haya ya thamani.

Katika mazingira haya wananchi wanapata dhahabu ama kwa kuchimba wenyewe katika eneo kati ya kijiji na mgodi, au kwa kuchenjua kutoka mawe yaliyotupwa na mgodi; au kwa uhusiano na waliomo ndani ya Mgodi.

Ni waliobeba tu vifurushi vya mawe ndio wanakamatwa na polisi, kunyang’anywa mawe yao ya dhahabu, kupigwa na wanaokaidi wakamatwa na kupelekwa kituo na kubambikiwa kesi.

Hakuna eneo maalum iliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Hii ni kero ya kwanza kubwa ambayo inawakabili wananchi wa Kijiji cha Mavota ambao wamekuwa wakitegemea kuendesha maisha yao kutokana na shughuli za uchimbaji.

Ukatili mwingine unaodaiwa kufanywa na polisi nikuwakamata wanaochunga mifugo pembezoni mwa hifadhi, “kuwabambikizia kosa” la kuingiza mifugo kwenye hifadhi na kuwatoza faini ya Sh. 10,000 kwa kila ng’ombe.

“Wafugaji wanakamatwa, wanapigwa, wanatozwa faini na wakishalipa hawapewi hata risiti ya faini waliyotozwa,” anaeleza mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Mashauri Maduka huku akitikisa kichwa kuonyesha masikitiko.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa na mwandishi wamekiri kuruhusiwa na polisi kwenda kuingia ndani ya mgodi lakini wanaporudi, wanatishiwa, wanapigwa na kunyany’anywa walichonacho.

Mchimbaji mdogo mkazi wa kijiji cha Runzewe aliyejitambulisha kwa jina Makoye Pascal, anasema anashangaa serikali kuruhusu kampuni ya nje na kuwatelekeza mwananchi anahoji.

“Mbona wachimbaji wadogo na wakubwa sote tunafanya shughuli moja?” anauliza.
Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa Gazeti hili umebaini kuwa kwa sasa Jeshi la polisi limekuwa likifanya mabadiliko ya Askari polisi wanaopelekwa kwa ajili ya kazi maalum ya kulinda mgodi wa Tulawaka kila baada ya wiki mbili.

Mabadiliko hayo yanatafsiriwa na wananchi wa Mavota kwamba ni mbinu ya kujitengenezea mazingira ya kila askari kujipatia fedha,kwa vile kwanza inadaiwa kwamba Mgodi umekuwa ukiwalipa posho ya shilingi 50,000/= kila siku,lakini pili ni fedha ambazo wanazipata kutokana na kuwapora wachimbaji mawe yao dhahahu na kuwatoza faini wafugaji.

Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera Philip Kalangi alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo,alimtaka mwandishi kwenda katika kituo cha polisi cha Mavota na kuwasiliana na Mkuu wa kituo hicho,ndipo awasiliane naye akiwa kituoni hapo.

Mwandishi wa Makala haya aliwasiliana na Uongozi wa Mgodi wa Tulawaka kwa kutuma maswali kwa njia ya maandishi juu ya vitendo vinavyodaiwa kufanywa na polisi wanaolinda mgodi huo kwa raia,pamoja na malipo ya posho yanayofanywa na mgodi kwa askari polisi.

Akijibu maswali hayo Ofisa mahusiano wa Kampuni ya Barrick Necta Foya anasema mgodi wa Tulawaka unafuata kanuni za Umoja wa Mataifa za usalama na haki ya Binadamu(United Nations Voluntary Principle on Security and Human Rights).

“Na tunatoa mafunzo ya kina kwa kampuni zetu za ulinzi pamoja na sungusungu wa eneo hilo ili kuhakikisha wanafuata masharti ya kanuni hizo…’’ anasema.

Anaongeza’’tuna makubaliano maalum(Memorandum of Understanding) na jeshi la polisi Tanzania ambalo linafanya doria nje ya ukuta kwenye eneo la mgodi kuhakikisha kuwa nao wanafuata kanuni hizi za umoja wa mataifa…’’.

Hata hivyo anasema kumekuwa na matukio kadhaa ambapo watu wanaruka ukuta na kuingia ndani ya eneo la shughuli za mgodi kwa lengo la kuiba mawe yenye dhahabu na mali nyingine za mgodi.

“Wafanyakazi wetu wa ulinzi huwasindikiza kwa usalama wavamizi hawa mpaka nje ya eneo la shughuli za mgodi na inapobidi kuwaweka chini ya ulinzi, jambo hili hufanywa bila kutumia nguvu nyingi kupitiliza…’’anaeleza Foya katika majibu yake kwa njia ya maandishi.

Anafafanua kuwa wahalifu wote ambao hukamatwa ndani ya eneo la mgodi hukabidhiwa kwa polisi kwa ajili ya taratibu za kisheria,”Wafanyakazi wetu wanafuata kanuni na sheria na hawatumii silaha za moto kukabiliana na wahalifu wanaoingia eneo la mgodi..’’.

Kuhusu malipo kama posho kwa askari Polisi Foya anasema mgodi hauajiri askari wa Jeshi la polisi Tanzania.”Tunaajiri kampuni binafsi za ulinzi ambazo zinajukumu la kuhakikisha usalama kwenye eneo la mgodi.Jeshi la polisi la Tanzania linaweka askari wake nje ya ukuta wa mgodi ambao wanafanya kazi ya Doria..’’.

1 Comment
  • Yeah..hiyo ndiyo hali halisi ya Tulawaka na Migodi mingine, watu wamesahauliwa na kudharauliwa (the gravely forgotten and ignored people surrounding the Mining area). Huwezi kuamini macho yako ukifika maeneo yale, watu wa vijiji vya jirani wana maisha duni sana huwezi amini kama Mwenyezi Mungu amewajaalia kuwa kwenye eneo lenye neema ya maliasili kama ile!!…

    BEEN THERE, AND PHYSICALLY SEEN THAT!!

     

    Rgds,

    Eng.Sadick Muhanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *