Kipindupindu charudi katika mikoa 6. Watu 458 walazwa, 6 wafariki

Jamii Africa

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa ugonjwa wa kipindupindu umerudi, mwezi Novemba 2016 wagonjwa 458 wameripotiwa kuugua ugonjwa huo nchini, sita kati yao wamepoteza maisha.

Ugonjwa huu upo katika Mikoa 6 ambayo ni, Morogoro(wagonjwa 282), Dodoma(wagonjwa 96 na vifo 2), Mara(wagonjwa 31), Kigoma(wagonjwa 30 na vifo 4), Arusha(Wagonjwa 11) na Dar es Salaam wagonjwa 8.

Ameongeza kwa kusema kuwa baadhi ya halmashauri nchini zinaficha taarifa za wagonjwa wa kipindupindu kwa kuogopa kuchukuliwa hatua na Rais Magufuli(Kutumbuliwa).

Waziri Ummy amewataka Viongozi wa Halmashauri nchini kutoficha taarifa za wagonjwa wa Kipindupindu kwani ni makosa kisheria na inawanyima fursa wananchi kusogezewa na Serikali sababu ukubwa wa tatizounakuwa haujajulikana.

Tatizo la ugonjwa wa kipindupindu lilianza kuripotiwa mwaka jana mwezi mei mwaka 2015, Mkoani Kigoma wakati wakimbizi wa Burundi walipokuwa wakikimbilia nchini sababu ya machafuko nchini mwao.

Tangu kipindi hicho ugonjwa huo umekuwa ukitokomea na kurudi na umekuwa ukisababisha vifo hasa maeneo yasiyozingatia usafi.

DALILI KUU ZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU

Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaoambukizwa kwa kula chakula au kinywanji chenye vimelea vya Vibrio cholera. Vimelea hivi hupatikana kwenye Kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au mtu mwenye vimelea ambaye hajaonyesha dalili.

KUEPUKANA NA KIPINDUPINDU

Kunawa mikono wakati wote kabla ya kutayarisha au kula chakula, kusafisha vyombo kama sahani, vikombe n.k.
Nawa mikono kabisa kwa sabuni; kiganja, upande wa nyuma wa mkono, katikati ya vidole na kucha kwa sekunde. Baada ya haja na kabla ya kula.

Kuwa na akiba ya maji yaliyochemshwa.

Kupika chakula vizuri maana halijoto juu ya 75 °C (hadi 85 mlimani) inaua bakteria;

Kumenya matunda yote.

Kufunika chakula maana nzi wanapitisha bakteria kwa miguu yao.

Maji ya choo yanayotokana na wagonjwa wa kipindupindu yanapasa kupitia mashimo ya choo yaliyohifadhiwa vizuri ili kuzuia usambazaji wa bakteria.

Vifaa vyote vinavyotumiwa na wagonjwa vinapaswa kuchemshwa kwa maji ya moto.

Mtu anayeshikana na wagonjwa wa kipindupindu anapaswa kunawa mikono.

Mashimo ya choo yanapaswa kuwekwa dawa za kuua bakteria kwa kutumia klorini.

Tumia maji yaliyotibiwa pekee hasa ikiwa ni ya kunywa; yachemshe au utie matone 5 ya klorini kwa kila galoni 1 au utumie dawa ya kutakasa maji.

Yaache maji yatulie kwa dakika 30 kabla ya kunywa.

Epuka kwenda haja karibu au ndani ya chanzo cha maji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *