Mkurugenzi wa Jamii Media, Maxence Melo akamatwa na Polisi

Jamii Africa

MKURUGENZI Mtendaji wa Jamii Media na mwanzilishi wa mtandao maarufu wa JamiiForums, anashikiliwa na Jeshi la Polisi katika kituo kuu cha polisi, Dar es Salaam, kwa madai ya kugomea agizo la muda mrefu la jeshi hilo.

Polisi wamekuwa wakiagiza na kuamuru kupewa taarifa za watumiaji wa JamiiForums bila mafanikio.

Maxence alipigiwa simu leo akiwa ofisini kwake asubuhi akitakiwa kufika kituoni hapo na alitekeleza mwito huo.

Baada ya kufika polisi kati, akiwa ameongozana na mhariri na mwanaharakati wa uhuru wa mawasiliano, Simon Mkina na mwanasheria, Nakazael Tenga, Maxence alinyimwa dhamana ya polisi.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa Maxence atafikishwa makahamani kesho asubuhi kujibu mashitaka ya kuzuia upelelezi wa polisi dhidi ya makosa ya mtandao.

JamiiForums imekuwa na msimamo wa kutotoa habari za wachangiaji wake kwa yeyote, kwani kufanya hivyo ni kuingialia uhuru na faragha ya wateja wake.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, msingi mkuu wa mtandao wa JamiiForums umekuwa kulinda faragha ya watumiaji wake.

Watumiaji wa mtandao wa JamiiForums wako huru kuweka mijadala, kuanzisha mijadala, kuchangia chochote pasipo kuvunja sheria za nchi au kuhatarisha usalama wa taifa.

Kampuni ya Jamii Media, inayoendesha mitandao ya JamiiForums.com na FikraPevu.com imejijengea heshima na umaarufu kwa muda mrefu kutokana na namna inavyoendesha na kusimamia shughuli zake ambazo kwa kiwango kikubwa ni za kimtandao.

Mtandao wa JamiiForums ni mtandao mkubwa wa Kiswahili kwa Afrika Mashariki na duniani ukiwa na wasomaji wasiopungua Milioni 2.5 kwa mwezi ambapo kwa mwaka 2016, mtandao huu unatimiza rasmi miaka 10 tangu uanzishwe.

Mtandao huu unasifika kwa kutoa fursa ya kipekee kwa watumiaji wake kutoa yaliyo mioyoni mwao huku wengine wakijifunza mbinu kadha wa kadha za kijasiriamali, afya, elimu na hata kuibuka wanasiasa wapya waliofundwa na wanajumuia ya JamiiForums.

Pamoja na kuendelea kutoa huduma hata katika nyakati ngumu, mtandao wa JamiiForums unakumbana mara kwa mara na changamoto nyingi zinazosababisha waanzilishi na waendeshaji wake kuwa katika misukosuko mara kwa mara, hasa na polisi.

Kwa muda mrefu tangu kuanzishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Jeshi la Polisi limekuwa likiushinikiza mtandao wa JamiiForums (kwa njia ya barua rasmi) kutoa taarifa za baadhi ya wateja wake.

JamiiForums katika kuhakikisha inasimamia usiri wa wateja wake, imekuwa ikihoji shinikizo kutoka Polisi yanazingatia sheria gani na kutaka kujua ni vifungu gani vya sheria ambavyo wadau wa mtandao huo wamevivunja bila kupewa maelezo yanayoridhisha zaidi ya kuelezwa kuwa hatua zaidi zitachukuliwa kama ushirikiano hautatolewa kwa Jeshi la Polisi.

Tayari Jamii Media imefungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania (Kesi namba 9 ya mwaka 2016); kutaka Sheria ya Makosa ya Mtandao, kifungu cha 32 na 38 viangaliwe upya kwa kuwa vinapelekea kuvunjwa kwa haki za msingi za watanzania watumiao mitandao ili kulinda maslahi ya umma kwa kuzingatia vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Baada ya kufungua kesi hiyo Serikali, kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliweka mapingamizi sita ikitaka kesi nzima ifutwe na Jamii Media walipe gharama zilizoingiwa.

Lakini mnamo tarehe 4, Agosti 2016 Mahakama Kuu ya Tanzania baada ya kuzipitia hoja zilizowasilishwa na Serikali na Wanasheria wa Jamii Media iliamua kuwa mapingamizi yote sita ya Serikali hayana mashiko na hivyo kesi ya msingi itaendelea kusikilizwa.

Maxence Melo anakamatwa huku kukiwa na Kesi hiyo ya Kikatiba dhidi ya taarifa ambazo Jeshi la Polisi wanazitaka, kesi ambayo mahakama kuu itatolea hukumu, tarehe 20 Februari.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *