SHULE ya Msingi Malolo yenye wanafunzi 386 (wavulana 189 na wasichana 197) katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma haina walimu wa kike kwa zaidi ya miaka 30, hali inayoleta changamoto kubwa hasa kwa watoto wa kike.
Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu umebaini kwamba, licha ya changamoto nyingi zinazoikabili shule hiyo iliyo katika Kata ya Malolo, tatizo la uhaba wa walimu, hususan wa kike, limekuwa sugu kiasi cha kuleta mazingira magumu kwa wanafunzi wasichana ambao wameshindwa kupata elimu ya hedhi.
“Kukosekana kwa walimu wa kike ni changamoto kubwa, kwa sababu wasichana wengi wanapevuka mapema tangu wakiwa darasa la tano, hivyo wanaposhindwa kupewa elimu ya namna ya kujihifadhi wengi huamua kubaki nyumbani na kukosa masomo mpaka wanaporejea katika hali ya kawaida,” amedokeza mmoja wa walimu ambaye hakupenda kutajwa kwa kuwa si msemaji.
Mwalimu huyo ameiambia FikraPevu kwamba, ni vigumu kwa walimu wa kiume kuzijua changamoto za watoto wa kike, lakini kama wangalikuwepo walimu wanawake ingekuwa rahisi hata kuwapatia elimu ya afya pamoja na suala zima la uhusiano ili kuepusha mimba za utotoni.
Aidha, amedokeza kwamba, ingawa shule hiyo haina rekodi za mimba, lakini ni muhimu ikiwa wanafunzi hao wakapatiwa uelewa ili waweze kujitunza.
“Mwalimu wa kike ndiye anayeweza kuwanasihi kwa kina kwa sababu ya uzoefu alionao kama mwanamke, anaweza kuwaelimisha hata namna ya kujitunza wanapokuwa katika hedhi, lakini ni vigumu kwa sisi wanaume kuketi na watoto wa kike na kuanza kuwaelewesha suala hilo kwa ufasaha,” alisema mwalimu wa shule hiyo, ambayo iko umbali wa kilometa 155 kutoka Mpwapwa mjini.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Boniface Massawe, alikiri kwamba ukosefu wa walimu wa kike ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wasichana ambao kwa mazingira ya vijijini, wengi wao wanapokuwa kwenye hedhi hujihisi kama wagonjwa na baadhi hutega masomo kwa kuwa hawajui jinsi ya kujihifadhi.
“Tuko walimu saba tu, wote wa kiume, na sijawahi kusikia kama alikuwepo mwalimu wa kike kwa miaka ya karibuni,” alisema Mwalimu Massawe.
Takwimu ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, Wilaya ya Mpwapwa ina jumla ya walimu 1,283 ambapo kati yao 670 ni wanaume na 583 wanawake.
Bosco Paulo Mwaluga ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji anayekaimu pia nafasi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Malolo, ambaye anabainisha kwamba kukosekana kwa walimu wa kike kunaleta ugumu wa kutambua hata watoto wanaopata ujauzito ingawa anasema hakuna kesi zozote za mimba.
“Kesi za mimba hakuna, kwa sababu ni lazima kuwepo na ushahidi… ingewezekana kuwagundua watoto waliopewa ujauzito kama wangekuwepo walimu wa kike,” anasema.
Ofisa Mtendaji huyo anasema, tetesi kadhaa zimewahi kuwepo kuhusu baadhi ya wanafunzi wa kike kuwa na ujauzito, lakini hakuna iliyothibitishwa.
“Mwaka jana kulikuwa na tetesi kwamba watoto wawili walikuwa na mimba, lakini baada ya uongozi wa shule kuwapeleka kupima walikutwa hawana, inawezekana kabisa wazazi ama jamaa zao waliwatoa mimba hizo kwa sababu mpaka mwanamume uone dalili kwamba huyu ana mimba, maana yake mama wa watoto tayari watakuwa wamegundua mapema na kuchukua hatua hata za kutoa mimba hizo.
“Ingekuwa rahisi kugundua mapema kama wangekuwepo walimu wa kike maana wao wanazijua dalili tangu mapema,” anasema Bosco ambaye anakiri kwamba tangu alipohamia kijijini hapo mwaka 2011 hajawahi kuona mwalimu wa kike akiletwa shuleni.
“Nimehamia mwaka 2011, sikukuta wala sijaona mwalimu wa kike akiletwa, taarifa nilizonazo ni kwamba hata wanakijiji wenyewe hawajui ni lini aliwahi kuwepo mwalimu wa kike, pengine kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita,” anasema.
Mwaluga anasema, changamoto ya ukosefu wa nyumba za walimu ni kubwa na huenda ndiyo kikwazo cha kutoletwa kwa walimu wa kike shuleni hapo.
“Kuna nyumba tatu tu na walimu saba ukiacha mmoja aliyeko masomoni, nyumba hazitoshi, tena afadhali wanaume wanaweza kujibana au hata kupanga uraiani, lakini kwa wanawake ni shida na unahatarisha usalama wao ikiwa utawaacha wakaishi uraiani, hasa kama hawajaolewa,” anasema Mwaluga.
Uhaba wa walimu
FikraPevu, ambayo ilizuru kwenye Kata hiyo hivi karibuni, inafahamu kwamba, shule hiyo ni moja kati ya shule tatu za msingi katika Kata ya Malolo ambapo nyingine ni Idodoma na Nzugilo, ambazo zote zimekuwa zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu bila kujali jinsia.
Mwalimu Massawe anasema kwamba, kwa miaka mitatu iliyopita shule hiyo ilikuwa na walimu wanne baada ya mmoja kwenda kusoma, ambapo mzigo wa ufundishaji ulikuwa mkubwa na hivyo kukwamisha maendeleo ya kitaaluma.
“Mimi nimefika hapa Januari, lakini kuna walimu wengine wawili wameongezwa ambapo mmoja ametoka Shule ya Mtejeta iliyoko mjini Mpwapwa na mwingine amejihamisha mwenyewe kutoka Shule ya Kimagai,” alisema.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, licha ya kuongezeka kwa walimu hao watatu, bado shule hiyo inahitaji walimu wawili wa ziada kwani kwa sasa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi shuleni hapo ni watoto 56 kwa mwalimu mmoja, tofauti na uwiano wa kitaifa wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40.
Maendeleo ya kitaaluma shuleni hapo yanaonekana pia kuwa duni, kwani kati ya watoto 54 waliomaliza darasa la saba mwaka 2016, ni 21 tu ndio waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Malolo, Bosco Mwaluga, anasema ukosefu wa walimu kwenye shule za msingi za kata hiyo ni changamoto kubwa ambayo inakwamisha maendeleo ya elimu.
“Hapa Malolo ameletwa Mwalimu Massawe ambaye alikuwa Nzugilo, Mwalimu Selemani Saidi kutoka Mtejeta na Mwalimu Emmanuel Kagali, ambaye amejihamisha mwenyewe kutoka Kimagai ili arudi hapa kijijini kwake,” anasema Bosco.
FikraPevu imebaini kwamba, Shule ya Msingi Idodoma yenye wanafunzi 314 inao walimu wanne tu kwa mwaka wa nne sasa, ambapo uwiano ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 79.
Aidha, Shule ya Msingi Nzugilo yenye wanafunzi 507 ina walimu nane ukiwa ni uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 63.
Nyumba za walimu
“Tuna changamoto kubwa pia ya nyumba za walimu, hapa Malolo zipo nyumba tatu tu ambazo haziwatoshi walimu saba waliopo, zinahitajika nyumba nyingine nne,” anasema Mwalimu Massawe.
Hali hiyo, anasema, imewafanya walimu wengine kwenda kupanga mitaani kwa gharama zao wenyewe, jambo ambalo linawaongezea mzigo na gharama za maisha.
Anaongeza kwamba, kukosekana kwa nyumba za uhakika ni kikwazo kingine kinachoweza kukwamisha kuletwa kwa walimu wapya, hasa wa kike, hivyo kuiomba Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha makazi ya walimu yanapewa kipeumbele.
Akizungumzia masuala mengine, Mwalimu Massawe alisema changamoto ya ukosefu wa vitabu vvya kiada na ziada bado ni kubwa, ambapo kwa sasa kitabu kimoja za ziada kinatumiwa na wanafunzi nane badala ya wanafunzi watatu kama Sera ya Elimu inavyoelekeza.
Lakini Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) unatambua kwamba kuwapatia nyumba walimu wanaoajiriwa na kupelekwa maeneo ya vijijini na yasiyofikika, ni moja ya motisha kwao.
Suala la afya na usafi nalo ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975, ambapo ina matundu nane tu ya vyoo.
“Ni changamoto kubwa kwa sababu kuna wanafunzi 189 wa kiume na 197 wa kike, matundu haya hayatoshi kabisa,” alisema Mwalimu Massawe.
FikraPevu inatambua kwamba, kwa watoto wa kiume, tundu moja linatakiwa kutumiwa na wanafunzi 25 wakati wasichana 20 wanatakiwa kutumia tundu moja, jambo ambalo katika shule hiyo halipo kwa kuwa wastani tundu moja linatumiwa na wanafunzi 48 bina kujali jinsia.