Ekari 250 za kijiji zamilikiwa na mwekezaji kwa uzembe wa viongozi

Jamii Africa

UJIO wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mlambalasi katika Kijiji cha Kiwere wilayani Iringa umeibua nongwa baada ya wananchi kuwatuhumu viongozi wao wa zamani kugawa ekari 250 za ardhi kwa mwekezaji tangu mwaka 2003.

Hata hivyo, ekari hizo 250 zinazoelezwa kwamba zinapitiwa na skimu hiyo haziwezi kurudi tena mikononi mwa kijiji kwani zilipata pia baraka za wanakijiji wote katika vikao halali.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonesha kwamba, mgogoro huo ulioibuka mwaka 2013, umesababishwa na kujengwa kwa skimu hiyo ya umwagiliaji yenye uwezo wa kumwagilia jumla ya hekta 500, kwa makadirio ya kuzalisha tani 2,500 kwa awamu moja.

FikraPevu imetembelea eneo hilo na kuona mfereji wenye urefu wa kilometa 6.5 kutoka maingilio kwenye Mto Ruaha ambao una ukubwa wa meta moja na uwezo wa kupitisha meta moja ya ujazo ya maji kwa sekunde (sawa na lita 1,000 kwa sekunde), ambao ulijengwa na kampuni ya APE Engineers ya mjini Iringa.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wanalalamika kwamba serikali ya kijiji ilifanya makosa kumpatia eneo hilo mfanyabiashara wa mjini Iringa, Abdallaziz Salum Hezhez, kwa madai kwamba hakustahili kupewa eneo kubwa kiasi hicho, hivyo kutafuta namna ya kutaka mfanyabiashara huyo anyang’anywe na lirudishwe kwa wananchi.

Tayari mwekezaji huyo amekwishalikatia hatimiliki ya miaka 99 shamba.

‘Presha’ za wananchi hao zinadaiwa kusababisha Mwenyekiti wa Kijiji, Ramadhan Ng’anguli, kujiuzulu uongozi mwishoni mwa mwaka 2012 wakimtuhumu yeye na viongozi wenzake wa wakati huo kuwahadaa wananchi.

Shamba linalolalamikiwa na wananchi hao lipo katika eneo la Muhunga, mpakani na Kijiji cha Luganga, ambalo hata hivyo kwa miaka yote ulikuwa msitu mkubwa ambao haukuwa ukitumiwa na wananchi hao kwa shughuli zozote za uchumi.

Taarifa zinaeleza kwamba, wananchi wa kijiji hicho kwa ridhaa yao ndio waliotoa eneo hilo kwa Hezhez ambaye aliomba ukaazi kijijini hapo tangu Aprili 9, 2003 kwa barua ya utambulisho iliyosainiwa na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kitanzini/Miyomboni, Lucas Wikes.

FikraPevu imefanikiwa kupata nyaraka zinazoonesha kwamba, mkutano wa hadhara uliofanyika Juni 26, 2003 na kuhudhuriwa na wananchi 319, pamoja na wajumbe 14 wa Halmashauri ya Kijiji, chini ya uenyekiti wa Ramadhan Ng’anguli, ndio ulioridhia kutolewa kwa eneo hilo na kukabidhiwa kwa mwekezaji huyo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Muhtasari wa mkutano huo ulioandikwa Juni 27, 2003 na kusainiwa na Mwenyekiti Ng’anguli na Ofisa Mtendaji wa Kijiji Fedinanti Sungu unaonyesha kwamba, agenda ya shamba hilo ilikuwa ya 5.

Agenda hiyo inasomeka hivi: “Shamba la Muhunga: Mwenyekiti aliwaeleza wananchi kuwa ndugu Abdallaziz S. Hezhez aliomba shamba kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha umwagiliaji, sisi kama serikali tuliamua kumpa eneo hilo kwa sababu amekaribisha kilimo cha umwagiliaji. Sisi kama serikali tulitoa eneo hilo, nyinyi wananchi mnasemaje? Wananchi wote walitoa eneo hilo kwa pamoja na kwa mikono miwili…”

Mkutano huo wa hadhara ulikuwa umetanguliwa na kikao cha Serikali ya Kijiji kilichofanyika Juni 14, 2003, ambacho pamoja na mambo mengine, kilijadili suala hilo lililokuwa katika agenda namba 6, ambapo iliamuliwa kwamba apewe eneo hilo.

Aidha, taarifa zinaonyesha kwamba, Juni 29, 2003, yaani siku tatu baada ya mkutano wa hadhara uliotoa eneo hilo kwa kauli moja, Kamati ya Huduma za Jamii ya Kijiji cha Kiwere iliyokuwa na wajumbe watano na wajumbe wawili wa Kamati ya Maliasili (Mema) walikwenda kuonesha mipaka ya shamba hilo huku Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji wa Kijiji wakiwa ndio viongozi wa msafara.

Wakati huo, Kamati ya Huduma za Jamii ilikuwa na Yustin Lipita (Mwenyekiti), Abdul Chang’a (Katibu) na wajumbe Ajentina Mpogole, Waridi Luvanda na Jose Nkenja, wakati wajumbe wa Kamati ya Mema walikuwa Samson Fuko (Katibu wa Maliasili wa Kanda) na Zuhura Mpagama (Katibu wa Maliasili Kijiji cha Kiwere).

Wakati ambapo aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii, Lipita, alikiri kutambua umiliki wa Abdallaziz katika shamba hilo, katibu wake, Abdul Chang’a alisema yeye ndiye aliyeongoza wenzake katika kutambua mipaka ya shamba pamoja na kuandika muhtasari wake.

Viongozi hao wa zamani walisema, kwa nyakati tofauti, kwamba wakati huo walikuwa wanatimiza wajibu wao tu na kwamba Sheria ya Ardhi ya Vijiji (Sheria Namba 5 ya 1999), ambayo hata hivyo haikuwa inafahamika na wengi, haikuweka kikomo kwa serikali ya kijiji katika ugawaji wa ardhi.

“Wengi hatukuwa tunafahamu thamani ya ardhi wala sheria za ardhi wakati huo hazikuweka kikomo, zaidi sisi tulikuwa tunatimiza wajibu kama viongozi, kwa sababu wananchi wenyewe ndio hasa walioitoa ardhi hiyo,” alisema Lipita katika mahojiano.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kijiji hicho aliyejiuzulu, Ramadhan Ng’anguli, alisema aliamua kuachia madaraka kwa sababu mbalimbali, ikiwemo hiyo ya shamba la Muhunga, lakini akabainisha kwamba, wananchi wenyewe ndio waliolitoa eneo hilo.

Ng’anguli alisema kwamba, ujinga wa kutojua thamani ya ardhi wakati huo ndio uliowafanya wananchi wakatoa eneo hilo kubwa, lakini baada ya marekebisho ya sheria ya ardhi yaliyofanywa mwaka 2007 na serikali kubainisha thamani ya rasilimali ardhi ndipo baadhi ya wananchi walijitokeza kuanza kuhoji suala hilo.

Hata hivyo, FikraPevu inafahamu kwamba, marekebisho ya mwaka 2007 Sheria ya Ardhi hayawapi mamlaka viongozi wa vijiji kugawa eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 50, bali mamlaka hayo anayo Kamishna wa Ardhi.

“Tatizo lilikwishamalizika muda mrefu, halmashauri yenyewe ilikwishatoa tamko lake, lakini inaonekana kuna baadhi tu ya vijana ambao wanakwenda kumtishia mwekezaji (Abdallaziz Hezhez) kwa lengo tu la kutaka wapate chochote.

“Kimsingi hakuna mgogoro, wananchi wenyewe ndio waliotoa eneo hilo, ingawa sasa wanatulaumu sisi viongozi kwamba huenda tulipewa rushwa na mwekezaji huyo ndipo tukampatia, jambo ambalo siyo kweli,” alisema Ng’anguli.

Ng’anguli alibainisha kwamba, suala hilo limekwisha kitambo na kama kuna makosa yalifanyika, basi wanapaswa kujilaumu wananchi wenyewe.

Aidha, alikanusha madai kwamba mojawapo ya masharti aliyopewa mwekezaji huyo ni kuwajengea mfereji kwa ajili ya umwagiliaji.

“Siyo kweli, hakuna mahali popote tulipokubaliana. Huyu mwekezaji shamba lake lipo mbali kutoka mahali ambapo alitaka kuchukulia maji ya umwagiliaji, hivyo akasema kwa kuwa anataka kuanzisha kilimo cha umwagiliaji na kwamba atachimba mfereji, basi maji hayo yatawanufaisha na wananchi wengine mahali mfereji huo utakakopitia,” alifafanua.

Hata hivyo, suala hilo ambalo liliibuliwa tena na baadhi ya wananchi mwaka 2012, lilifafanuliwa vyema na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa barua yenye Kumb.  Na. IDC/D.30/8/32/59 iliyosainiwa kwa niaba yake na G. R. Kaluwa.

“Kwa mujibu wa sheria za Ardhi za wakati huo (2003) (mwekezaji) alifanya upimaji na kupewa Hati ya kumiliki kwa miaka 99… kwa maana hiyo Serikali ya Kijiji haina mamlaka juu ya shamba hilo (kwani ilishalitoa) na kuwa Ardhi ya Kawaida (General Land).

“Kwa hiyo wananchi wawe waangalifu pale wanapotoa ardhi kwa watu ambao ni wageni kutoka nje ya kijiji. Waheshimu maamuzi yaliyofanywa na serikali zilizopita kwani ni halali na yanasimama kisheria. Ni vyema wananchi wakafuata kanuni, taratibu na sheria zinazolinda upatikanaji na ugawaji wa ardhi,” ilisema barua hiyo ya Mkurugenzi.

Kwa upande wake, Hezhez alisema anashangazwa na watu wanaomchafua na kusema amepora ardhi yao wakati ambapo anamiliki shamba hilo kisheria na alilipata kwa njia halali.

“Ninazo hati zote, na niseme ukweli mbele za Mungu, sikutoa rushwa ya aina yoyote kwa serikali ya kijiji ama mwananchi yeyote ili nipatiwe shamba hilo. Niliomba kama wanavyoomba wananchi wengi, tena ilichukua muda mrefu kupata,” alisema Hezhez.

Mfanyabiashara huyo alisema kama kuna mtu yeyote anayedhani kwamba shamba hilo alilipata isivyo halali na akawa na ushahidi, basi ni vyema akaenda kwenye vyombo vya sheria badala ya kuendelea kumzushia kwamba amepora ardhi yao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *