UTARATIBU wa kununua dawa kwa mzabuni binafsi zinapokosekana Bohari Kuu ya Dawa (MSD), unasababisha uhaba wa dawa, vifaa vya tiba kwenye zahanati na hospitali wilayani Mafia mkoani Pwani.
Kulingana na utaratibu huo, zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma, haziruhusiwi kununua dawa kwa mzabuni binafsi hadi zipate hati ya ununuzi yenye orodha ya dawa zilizokosekana MSD.
MSD Walaumiwa
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa, utaratibu huo unachangia kuzifanya zahanati na hospitali ya wilaya kukosa dawa ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Mafia , Erick Mapunda anasema MSD, huchangia zahanati na hospitali wilayani humo kukosa dawa, kwani inachukua muda mrefu kutoa orodha ya dawa zilikosekana, hivyo kuchelewesha ununuzi kwa mzabuni binafsi.
Erick Mapunda, DED, Mafia
Anaieleza FikraPevu kuwa, MSD huchukua kati ya mwezi mmoja hadi mmoja na nusu kufikisha hati ya ununuzi yenye orodha ya dawa na vifaa tiba zilizosekana ndipo mchakato wa kununua dawa kwa mzabuni binafsi uanze.
“MSD wakati mwingine wanakuwa hawana dawa, hawatoi taarifa mapema na utaratibu unatutaka kabla ya kununua dawa kwa mzabuni binafsi tupate hati yenye orodha ya dawa au vifaa tiba zilizokosekana kwao,” anasema.
Kauli yake inaungwa mkono na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mafia, Dkt. Abdallah Bhai, akiutaja utaratibu huo ni kikwazo kwa hospitali kutumia vyanzo vyake vya ndani kununua dawa zilizokosekana katika bohari ya serikali kwa wakati.
Anasema mbali na kutotoa taarifa kwa wakati, MSD pia haiweki dawa zote zilizokosekana kwenye hati ya ununuzi, hivyo kuikwamisha hospitali kununua dawa hizo kwa mzabuni binafsi.
Dkt. Bhai anafafanua kuwa, idara ya ugavi hainunui dawa au vifaa vya tiba kwa mzabuni binafsi kama hazijaoneshwa kwenye hati kwamba zimekosekana MSD.
Anasema kununua bila kuwapo kwa taarifa ya kukosekana kwa dawa kutoka MSD ni kosa kulingana na utaratibu wa ununuzi.
“Kuna wakati tuliagiza dawa MSD za shilingi milioni tisa, tulipata dawa za shilingi laki mbili, nyingine za shilingi milioni nane zilikosekana na fedha hairudishwi kwa kuwa watakupatia dawa wakiwa nazo,” Dkt. Bhai anaieleza FikraPevu.
Mganga Mfawidhi huyo anaongeza kuwa, “hata baadhi ya dawa ambazo hatukupata MSD hawakuziweka kwenye orodha ya zilizokosekana, tulikosa hadi paracetamol na tukashindwa kuzinunua kwa kuwa, ukienda halmashauri watu wa manunuzi wananunua dawa zilizopo kwenye orodha ambazo zilizokosekana.
Waruka kihunzi
Ofisa Uhusiano Mkuu wa MSD, Etty Kusiluka anasema bohari hiyo hutoa taarifa ya dawa na vifaa vya tiba vilivyokosekana mara oda inapowasilishwa na mhusika kabla ya kurejea kituoni kwake anafahamu dawa zilizokosekana.
Kuhusu madai kwamba baadhi ya dawa zilizokosekana haziwekwi katika orodha anafafanua kuwa, hali hiyo huweza kutokea iwapo ofisi za kanda zimeishiwa, lakini dawa hizo zipo MSD makao makuu, ambapo mteja hupewa baadhi, huku mchakato wa kuzipata zilizokosekana ukifanyika kati ya ofisi ya kanda na makao makuu.
“Kuna wakati baadhi ya dawa zinakosekana katika ofisi za kanda, lakini dawa hizo zipo katika bohari ya MSD makao makuu, hivyo mteja hupewa dawa zilizopo na wakati huo huo utaratibu hufanywa kati ya kanda na makao makuu kupata dawa au vifaa tiba vilivyokosekana, kitaalamu tunaita back order, zikipatikana mteja hupewa taarifa akazichukue,” Kusiluka anaieleza FikraPevu.
Anaongeza kuwa, ili kuhakikisha tatizo la dawa katika vituo vya tiba vya umma katika wilaya ya Mafia linapatiwa ufumbuzi MSD itatoa kipaumbele kwa wilaya hiyo kutokana na mazingira yake ya jiografia.
Mafia ambacho ni kisiwa katika Bahari ya Hindi ni moja ya wilaya za Mkoa wa Pwani, ina kata nane, tarafa mbili na watu 46,438 kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Huduma za matibabu zinatolewa kwenye zahanati za umma 16 na hospitali moja ya wilaya.
Wananchi washauri
Swalihu Mohamedi, mkazi wa Kigamboni kisiwani hapo anaishauri MSD kufungua duka la dawa kisiwani humo kuwawezesha wananchi kununua dawa kwa gharama nafuu zinapokosekana katika zahanati na hospitali ya wilaya.
Sharifa Abdu mkazi wa Bondeni, Mafia
“Hapa kwetu dawa ni tatizo kubwa, zinazokuja ni chache kuliko mahitaji ya wananchi wa Mafia. Naishauri serikali ifungue maduka ya MSD, tununue dawa kwa bei nafuu kuliko maduka binafsi wanauza aghali sana,” anaeleza Mohamedi kupitia FikraPevu.
Anasema dawa ambayo hospitalini inapatikana kwa Sh. 1,000 kwenye maduka binafsi huuzwa kati ya Sh. 3,000 hadi 4,000.
Hata hivyo, Kusiluka anasema bohari hiyo haiendeshi maduka ya dawa katika hospitali na kwamba maduka hayo yanafunguliwa na kuendeshwa na halmashauri wao wanakuwa wawezeshaji.
Mkazi wa Bondeni, Sharifa Abdu anashauri halmashauri ya wilaya ya Mafia kufanya kila linalowezekana kuanzisha duka la dawa wilayani humo ambalo litakuwa mkombozi pindi wananchi wanapokosa dawa katika zahanati na hospitali ya wilaya.