DAWASCO, Mita za maji zitumike kuondoa kero kwa wateja

Jamii Africa

MFUMO ambao unatumiwa na Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salam (Dawasco) kusomaji wa mita kwa sasa, ni kupitia kwa mtu maalumu anayepita kwenye nyumba za wateja na kisha kuwajulisha wateja kiasi kinachodaiwa.

Hasara ya mfumo huu ni uwezekano wa kutajiwa kiwango cha pesa ambacho hakiendani na kiwango cha maji kilichotumika, lakini pia huchelewesha malipo ya ankara kwa baadhi ya wateja.

Lakini kuna mfumo wa kidigitali kama ulivyo ule wa LUKU, unaotumiwa na wateja wa umeme. LUKU ni mfumo unaohusisha malipo kabla ya kutumia huduma (kwa Kiingereza- “pre-paid”) na pindi kiwango cha pesa kikiisha, huduma hukoma.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO), Jackson Midala akionesha mita mpya za maji.

Ikiwa Dawasco watatumia mfumo huu, wanaweza kutatua changamoto ambazo zinaikumba kwa sasa – kubwa ikiwa malalamiko katika suala la malipo, ikiwemo foleni wakati wa kulipa ankara.

Mbunge Mnyika alalamika

Tangu mwaka 2010, kumekuwepo na malalamiko yakielekezwa kwa Dawasco kupitia aliyekuwa Mbunge wa Ubungo, sasa akiwa Mbunge wa Kibamba, John Mnyika. Sehemu kubwa ya malalamiko yake ni malipo ya huduma za maji.

Mwaka 2012, Mnyika alinukuliwa kwa kusema “Dawasco iache kuwatumia wafanyakazi wanaohusika na ukaguzi, kufanya kazi tofauti za kusoma mita na kugawa Ankara, badala yake wafanyakazi hao wafanye ufuatiliaji wa dharura wa ufanisi wa mtandao mzima wa maji katika maeneo mbalimbali.”

Kauli hiyo ilikuja kutokana na Dawasco kuwa na changamoto nyingi, ambazo bado zipo mpaka hivi sasa, kutokana na uzito wa matatizo ya ankara na mengine ya mfumo wa kusafirisha maji kwa wateja.

Hata mfumo wa maji machafu nao utawekewa mita mpya.

Endapo kungekuwa na mfumo wa kiielektroniki ambao hauitaji wakaguzi wa kusoma mita, basi watumishi hao wa Dawasco wangehamishiwa maeneo ya utatuzi, hasa kwenye mfumo wa usambazaji maji.

Hivi karibuni Dawasco ilianza kuziondoa kwa wateja, mita chakavu zipatazo 85,000. Lakini baada ya kubadilisha mita hizo, baadhi ya wateja kupitia mitandao ya kijamii, wanalalamikia mita hizo kwa kudai kiwango cha pesa ni kikubwa kulinganisha na kiwango halisi cha maji ambacho familia zao hutumia.

Zimbabwe watumia ‘LUKU za maji’

Mfumo wa mita za kiilektroniki unaweza kuondoa malalamiko yote hayo ya wateja, bahati nzuri ni kwamba mfumo huu umeweza kutumika kwenye baadhi ya nchi za Afrika ambazo hali ya uchumi sio nzuri.

Zimbabwe imefanikiwa kuwekeza kwenye teknolojia ya kutumia “LUKU za maji” katika miji ambayo haina miundombinu ya kuridhisha, hivyo Dawasco wanaweza kuiga huko.

Ili kupunguza malalamiko, kuondoa wadaiwa sugu wa ankara za maji, hii ndio mbinu pekee ya kisasa ambayo inamlazimu mtumiaji kulipa kabla ya kupata huduma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *