NJAA sasa inainyemelea Wilaya ya Tarime, Mara kutokana na mdudu mharibifu wa mahindi.
Ikiwa mavuno ya mahindi hayatakuwa ya kuridhisha msimu, huu, basi wakazi wa wilaya hiyo, wataathirika kwa kukosa chakula na fedha.
Anayesababisha hofu ya kukosekana kwa mavuno ya kutosha msimu huu ni mdudu aitwaye- funza wa mabua. Kwa lugha ya Kiingereza anaitwa Stalk borer.
Mkazi wa Mtaa wa Kebikiri Kata ya Turwa wilayani Tarime Lea Joseph akionesha jinsi mdudu funza wa mabua alivyoharibu mahindi.
FikraPevu imefanya uchunguzi na kutembelea mashamba mbalimbali na kubaini mashamba mengi ya mahindi yakiwa yameliwa na wadudu.
Mashamba yaliyoshambuliwa na wadudu hao hadi sasa, yanakadiriwa kufikia hekta 135 za mahindi, ambayo endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, wakulima wataingia hasara.
Katika kukabiliana na wadudu hao, FikraPevu imeshuhudia baadhi ya wakulima wasio na uwezo wa kununua dawa za kuua wadudu, wakitumia njia mbadala za kienyeji kunusuru mazao, kwa kunyunyizia majivu na udongo.
Wakulima hao wanafanya hivyo kwa kuepuka gharama za dawa za dukani (kemikali au viuatilifu), ambapo njia hizo za kienyeji wamedai zimesaidia kuzuia wadudu kuvamia mahindi.
Katika mahojiano yake na FikraPevu, Daniel Chacha mkazi wa Kijiji cha Borega kata ya Ganyange anasema: “Kwakweli wakulima saa hizi tunalia, mahindi yameingiliwa na wadudu wakati huohuo mvua yenyewe ni ya kusuasua. Yaani mwandishi wewe umeshuhudia wadudu walivyoshambulia mahindi ambayo mengi hata hayajaweka watoto,” anasema.
Anaongeza, “mashamba ni makubwa, watu wanaona kununua dawa ni gharama sana, dawa zenyewe unaweka siku chache wadudu wamerudi tunachokifanya tunatibu kwa kienyeji.
Tunayanyunyizia majivu au udongo, kwakweli imesaidia maana baada ya kugundua wadudu wameingia kwenye mahindi ilibidi sasa tuyawahi mahindi ambayo bado hayajaingiliwa na wadudu na kuyanyunyizia udongo mlaini na majivu na imesaidia.
Tunaomba serikali itusaidie wakulima waone tatizo hili ni kama janga tupatiwe dawa za kuuwa wadudu”.
Lucy John, mkazi wa Sirari anasema kuwa kitendo cha wadudu kuharibu mahindi kimewaingiza hasara, “Tumegharamia uandaaji shamba, kupalilia, dawa bado mazao mengine yamekauka kwa kukosa mvua na ukifanikiwa bado kwenye kuvuna na usafirishaji kutoka shambani ni gharama, bado uyauze kwa bei ya hasara yaani ni shida”.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Matongo, Daniel Irondo ameimbia FikraPevu kuwa chanzo cha kuwepo kwa wadudu hao ni kutokana na ukame wa muda mrefu, ambao umechangia wadudu hao kuingia kwenye mahindi.
Aidha, anasema kuwa kunapokuwepo na mvua za kutosha, wadudu hao huwa hawaonekani.
FikraPevu imebaini baadhi ya mahindi yaliyoliwa na wadudu ni mbegu za mahindi za kutoka nchini Kenya zinazouzwa sh 12,000 kwa mfuko wenye ujazo wa kilo mbili zinazopandwa na wakulima walio wengi ambazo ni Hybrid Na.H6213, Na. H614, Na. H517, Na. H625, Na. H614, Na. H626, na DK. 8031 pamoja na mahindi mengi yaliyoshambuliwa sana ni mbegu ya kienyeji inayopandwa hususan maeneo ya vijijini iitwayo Maria.
Kushamiri wadudu hao
Perusi Samwel, mkazi wa Kenyamanyori anasema kuwa serikali isipochukua hatua kuhakikisha utatuzi wa wadudu huo unapatikana, wakulima wengi watakula hasara.
Anasema gharama ya kunyunyizia dawa ambayo ni sh. 9,000 kwa ekari ni kubwa kulinga na ukubwa wa mashamba wananchi waliyolima, kwavile watahitaji madawa mengi na gharama kuwa kubwa.
Recho John anasema kwakuwa wadudu hao wameathiri mashamba mengi ya mahindi, hatua za kunusuru mazao yaliyosalia endapo hazitachukulia, watakosa chakula na pengine bei ya mahindi itapanda zaidi kutokana na mahindi yatakayozalishwa kuwa kidogo.
Kwa upande wake, Paul Mwita, mkazi wa Mtaa wa Gamasara anaiambia FikraPevu kuwa, pamoja na wakulima wengi kutumia majivu na udongo katika kukabilia na wadudu hao, dawa hizo za kienyeji zinafaa tu pale kabla mdudu hajaingia ndani ya mmea, akishaingia tu majivu hayasaidii.
Suluhisho la kuwaondoa kabisa funza wa mabua ni kutumia dawa za kemikali tu ambazo wakulima wengi hawawezi kumudu.
Mtara Marwa, mfanyabiashara wa mahindi mkazi wa Mtaa wa Rebu, Kata ya Turwa anasema “mimi mwenyewe nusu nzima ya heka ya mahindi wameingiliwa na wadudu na sijui ni aina gani za dawa natakiwa kuweka.”
Anauliza, “kwanini serikali isitupatie dawa ili kutunusuru wakulima? Hili walione kama janga kubwa kwa wakulima.”
Anaendelea, “sasa tukisema mkulima mwenyewe anunue dawa, sidhani kama wote watatekeleza hilo maana uchumi ni mgumu, pesa hakuna hata yakula inakosa, hiyo ya dawa itatoka wapi?’’.
Akizungumza na FikraPevu, Kaimu Afisa kilimo wa Halmashauri ya Mji Tarime, Sadock Lundi anasema kuwa katika msimu wa masika uzalishaji wa zao la mahindi umekumbwa na wadudu aina ya Stalk borer ambao wameathiri hekta 12.8 na wakulima wameshauriwa kutumia dawa ya maji ya kuuwa wadudu ambayo ni Supereron na Duducron.
Lundi anasema kuwa Halmashauri iliweka malengo katika mwaka 2016/2017 kulimwa hekta za mahindi 3,663.75, huku mavuno yakikisiwa kuwa tani 13,922.25; hata hivyo zililimwa hekta 1,552, makisio ya mavuno yakiwa tani 5,897.6. Asilimia 20 ya hekta hizo sawa na hekta hekta 310.4 ziliathiriwa na ukame.
Kaimu Afisa kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Stanley Kubalila, anakiri kuwepo kwa wadudu hao ambao wameharibu hekta 123 katika halmashauri hiyo na kwamba chanzo cha wadudu hao ni ukame na ili kuwaondoa kabisa wakulima wanatakiwa kutumia dawa za kemikali .
“Dawa za kienyeji za udongo na majivu zenyewe ni kinga tu. Husaidia mdudu asiweze kuingia kwenye mahindi maana anapoingia ukaa katikati ya muhindi ndani anapokuwa ameingia kwenye mmea tiba ya kuuwa mdudu huyo ni dawa za kemikali.
Kubalila amewataka wakulima kutumia dawa za kuua wadudu ambazo ni Thiodan dust, Sumithion dust, Thionex dust na Malathion dust zinazouzwa kati ya Sh. 9,000 hadi Sh. 12,000 na kwamba serikali haitoi ruzuku ya dawa za kuua wadudu zaidi ya ruzuku ya pembejeo za kilimo na mbolea.
Kubalila anaiambia FikraPevu kuwa hakuna ruzuku ya dawa za wadudu kutoka serikalini huku akibainisha hali halisi ya uvunaji wa zao la mahindi kwa msimu wa vuli 2016/2017 mavuno tegemewa zao la mahindi ilikuwa hekta 8,115 na kuvuna tani 35,706, lakini hekta zilizolimwa ni 6,898 huku mavuno halisi yakiwa tani 24,143.0.
“Msimu wa Masika malengo yalikuwa hecta 10,633, huku mavuno yaliyotegemewa ni tani 43,595 katika msimu wa Masika 2016/2017.
Hili la mdudu ameshambulia mazao ya mahindi, nawashauri wakulima ambao wameshindwa kupulizia dawa watumie njia za kienyeji kwa kuweka udongo laini na majivu kwenye mahindi, husaidia kuuaa mdudu,’’ anasema Kubalila.