Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bara) Bw. Zitto Kabwe amesema kuwa uamuzi wa Waziri Mkuu kuendelea kuhalalisha posho ni kinyume na uamuzi wa baraza la mawaziri na unakinzana na mpango wa maendeleo wa miaka mitano uliopitishwa na Bunge hivi karibuni. Kutokana na hayo Bw. Kabwe ametaka Waziri Mkuu Bw. Mizengo K.P. Pinda afukuzwe kazi na Rais Kikwete au yeye mwenyewe aamue kujiuzulu.
Akiandika katika ukurasa wake wa Facebook muda mfupi uliopita Bw. Zitto amesema kuwa “Nasikitika kuwa W-Mkuu amerejesha suala la posho za vikao kwenye mjadala ilhali lilimalizwa baada ya Bunge kupitisha Mpango wa maendeleo wa miaka 5.” Akielezea kitendo hicho cha Waziri Mkuu Bw. Zitto amesema kuwa “Kitendo cha W-Mkuu kulilia posho kinaonyesha jinsi asivyo tayari kusimamia na kutetea sera za serikali anayoongoz(a)”
Hivi karibuni Bw. Zitto alikuwa ni mbunge wa kwanza kutangaza hadharani kukataa kuchukua posho za vikao ambazo wabunge hulipwa kila siku wanapokuwa katika vikao vya Bunge au vikao vinavyoendana na kazi zao Ubunge.
Katika barua yake ya tarehe 7 Juni, 2011 kwenda kwa Katibu wa Bunge ambayo imepata umaarufu mkubwa Bw. Zitto aliandika kuwa “posho ya kikao haistahili kulipwa kwa Mbunge na mtumishi mwingine yeyote wa serikali kwani kuhudhuria kikao ni sehemu ya kazi yangu” na kutokana na hoja hiyo alielekeza kuwa hadi utaratibu mpya utakapokuwa umewekwa posho hiyo ielekezwe kwenye taasisi ya Kigoma Developmnet Initiative ambayo yeye ni muasisi wake.
Uamuzi huo hata hivyo nao ulionekana kuleta taswira isiyo sahihi na baadhi ya watu walikosoa uamuzi huo wa kukataa posho kwenda kwake binafsi lakini kukubali posho hiyo iende kwenye taasisi yake. Hata hivyo katika majibu ya Ofisi ya Bunge kwa hoja ya Zitto ambayo yalitolewa tarehe 10 Juni Bunge lilikataa kutekeleza maelekezo hayo ya Zitto na kumuambia kuwa utaratibu wa Bunge ni kumlipa Mbunge na huyo mbunge ataamua kufanya nini na posho hizo.
Kutokana na uamuzi huo wa Bunge Bw. Zitto alimuandikia tena Katibu wa Bunge na kwa kuweka mstari mpya wa uwajibikaji alitangaza kukataa posho hizo moja kwa moja. “Ninakupa taarifa bora kukataa stahili hii. Hivyo ninaelekeza ofisi yako isinilipe stahili ya posho za vikao (sitting allowance) kuanzia leo tarehe 8 Juni, 2011” alisema Bw. Zitto.
Uamuzi huo umesababisha mgongano kati ya upinzani na chama tawala hadi kulazimisha Waziri Mkuu kutolea tamko ambalo halikupokelewa vizuri na watu wengi hasa alipotangaza kuwa baadhi ya posho hizo zinalindwa kikatiba na kuwa haziwezi kuondolewa bila kubadilisha Katiba. Lakini kinachoonekana kuwagusa watu vibaya ni madai kuwa posho hizo ni muhimu kwani zinatumiwa na wabunge kutoa misaada mbalimbali kwa watu wanaowaomba hivyo ni muhimu kuendelea.
Pamoja na msimamo huo mpango mwingine wa maendeleo wa serikali ya CCM unaonesha kuwa ni kusudio la serikali kuondoa posho mbalimbali ambazo hazina ulazima ili kuleta nidhamu zaidi katika matumizi ya fedha.
Hata hivyo katika ukurasa wake wa Facebook ambao Bw. Zitto hajaonesha kama anakusudio la kupeleka hoja yake hiyo nzito mbele zaidi au ilikuwa na lengo tu la kuonesha kutokufurahishwa na msimamo wa Waziri Mkuu kwani kama kweli anaamini Waziri Mkuu aidha ameenda kinyume na maamuzi ya Baraza la Mawaziri au kinyume na Bunge anaweza kabisa kuleta hoja Bungeni ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.
Zitto ni shujaa mwingine tunayejivunia lakini hivi hizo pesa siokwamba unazitoa mkono wa kushoto na kuziweka mkono wa kulia?
jamani hawa waheshimiwa wabunge wa chama tawala mi siwaelewi hivi kweli mwalimu aliyeko masomoni anazuiliwa mshahara kiduchu alionao kwa kupindisha mkataba. lakini nyie mnataka muendele kulipo posho ambayo ni sawa na mshahara wa huyo mwalimu.Haiwezekani kabisa siungi mkono hoja , nakubaliana na zito.