JUMLA ya watu 48,695 wamekufa na wengine 282,194 kujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani zilizotokea nchini Tanzania katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi 2015.
Uchunguzi wa FikraPevu umeonyesha kwamba, katika kipindi hicho cha miaka 16, jumla ya ajali 302,875 zilitokea na kati ya hizo ajali mbaya zilizosababisha majeruhi na hata vifo zilikuwa 41,690.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, idadi hiyo ya ajali ni wastani arwa ajali 18,930 kwa mwaka ambayo pia ni wastani wa ajali 52 kwa siku.
Aidha, FikraPevu imebaini pia kwamba, wastani wa watu 10 hufariki dunia kila siku nchini Tanzania kutokana na ajali hizo.
Taarifa kutoka Ofisi ya taifa ya Takwimu pamoja na Jeshi la Polisi zinaeleza kwamba, mwaka 2013 ndio uliokuwa na majanga kutokana na kurekodi jumla ya ajali 24,480 ambapo kati ya hizo, ajali mbaya zilikuwa 3,545 ambazo zilisababisha vifo 4,091.
Kwa mujibu wa takwimu hizo ambazo FikraPevu inazo, makosa ya usalama barabarani yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kutoka makosa madogo 148,169 mwaka 2000 hadi kufikia makosa 1,381,705 mwaka 2015, likiwa ni ongezeko la mara tisa zaidi.
Kuhusu ajali, nazo zimeonekana kupanda na kushuka kutoka 15,577 mwaka 2000 hadi 8,777 mwaka 2015 lakini ajali mbaya zilizosababisha vifo zimeongezeka kutoka 1,525 mwaka 2000 hadi 2,909 mwaka 2015.
Aidha, idadi ya watu waliokufa kwenye ajali imeongezeka maradufu kutoka 1,812 mwaka 2000 hadi 3,574 huku idadi ya majeruhi ikipanda na kushuka kutoka 15,123 mwaka 2000 hadi 9,993 mwaka 2015.
Pamoja na kupungua kwa idadi ya ajali, bado watu wengi wanapoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na nchi zilizoendelea au zinazodhibiti ajali.
FikraPevu inatambua kwamba, idadi ya vifo vinavyosababishwa na magari ni vingi, vinafukuzana na vifo vinavyotokana na malaria ambao ni ugonjwa unaoangamiza zaidi watoto wa chini ya miaka mitano.
Tangu mwaka 2000 hadi 2015, jumla ya makosa madogo ya usalama barabarani yaliyoripotiwa yalikuwa 4,761,760.
Matukio ya kutisha ya ajali
Aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, ACP Mohammed Mpinga akiongea na waandishi wa habari mwaka 2015, alisema ongezeko la ajali ni kubwa kwa sasa ambapo juhudi za makusudi zisipofanyika hali itakuwa mbaya.
“Kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu Januari hadi Machi 2015 kumetokea vifo 866 na majeruhi 2,370 kutokana na ajali 2,116, hii ni hatari sana,” alisema.
FikraPevu inafahamu kwamba, katika mwezi Januari 2015 pekee zilitokea ajali 823 zilizosababisha vifo 273 na majeruhi 876, mwezi Februari zikatokea ajali 641, vifo 236 na majeruhi 726 na mwezi Machi mwaka huo huo zilitokea ajali 652, vifo 357 na majeruhi 761.
Matukio makubwa ya ajali hizo kwa mwaka 2015, ni pamoja na ajali mbaya iliyotokea Machi 11, 2015 katika Kijiji cha Changarawe, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa iliyohusisha magari mawili likiwamo basi la Majinjah na lori la mizigo na kuua watu 50 na majeruhi 22.
Basi la Majinja likiwa limefunikwa na kontena na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40 huko Mafinga, mkoani Iringa.
Kumbukumbu ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, Aprili 9, 2015 katika eneo la Mkata mkoani Tanga ilitokea ajali iliyosababisha vifo 10 na majeruhi 12.
Aidha, Aprili 12, 2015 ilitokea ajali mbaya mkoani Morogoro katika eneo la milima ya Iyovi na kusababisha vifo 19 na majeruhi 10, ambapo 13 waliteketea kabisa kwa moto wakati basi la Nganga kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam lilipoteketea baada ya kugongana na Fuso kwenye kona kali za milima hiyo.
Mnamo Aprili 17, 2015 ajali ya basi dogo la abiria lililotumbukia mtoni wilayani Rungwe mkoani Mbeya ilisababisha vifo vya watu 20 na kuacha majeruhi kadhaa.
Matukio mengine ya kusikitisha ya ajali ni vifo vya watu 24 na majeruhi 51 kufuatia ajali mbaya ya basi la Chatco iliyotokea Januari 2011 mkoani Tanga.
Aidha, watu 26 walikufa papo hapo na wengine 45 kujeruhiwa mkoani Tabora mwaka 2011 kufuatia kuanguka kwa basi la AM Cooach lililokuwa linatokea Arusha kwenda Mwanza.
Mnamo Machi 2011, abiria wote 11 waliokuwa katika gari dogo aina ya Toyota Hiace (Kipanya) walikufa baada ya kufunikwa na lori la mafuta eneo la Kibamba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Ni mwezi huo huo ambapo wasanii 13 wa kundi la muziki la Five Stars Modern Taarab walipoteza maisha katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro baada ya dereva wa basi dogo aina ya Toyota Coaster lililowabeba wasanii hao kuparamia lori la mizigo lililokuwa limeegesha pembeni mwa barabara kuu ya Iringa–Morogoro.
Inaelezwa kwamba, asilimia 78 ya waathirika wa ajali za barabarani ni abiria na watu wanaotembea kwa miguu, ambapo kwa mujibu wa takwimu za kuanzia miaka ya 2000, asilimia 40 ya wanaokufa kwenye ajali ni abiria ndani ya magari hayo na zaidi ya asilimia 38 ni watembea kwa miguu.
Vyanzo vya ajali
Jeshi la Polisi limesema kwamba kukua kwa uchumi na kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara na kukua kwa kipato kwa baadhi ya Watanzania kumeongeza vyombo vya moto vya usafiri.
Gari la Taqwa likiovateki malori katika kona mbaya ya Mlima Kitonga mkoani Iringa.
Hata hivyo, ongezeko hilo halijaenda sambamba na elimu ya utumiaji wa barabara kwa madereva na waenda kwa miguu, hali ambayo imefanya kuwepo kwa ukiukaji wa sheria za barabarani kwa madereva pamoja na waenda kwa miguu.
Hali hiyo, limeeleza Jeshi la Polisi kwamba, imesababisha kuongezeka kwa ajali za barabarani ambazo siyo tu zimesababisha upotevu wa nguvu kazi, lakini pia kuongeza uharibifu wa miundombinu na mali, na kusababisha vifo na majereha kwa manusura.
Sababu zinazochangia ajali za barabarani zimetajwa kuwa ni sababu za kibinadamu, uchakavu au ubovu wa vyombo vya usafiri, na sababu za kimazingira.
Takwimu ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, sababu za kibinadamu zinachangia ajali nne kati ya tano, ukiwa ni wastani wa asilimia 82.5.
Miongoni mwa sababu hizo za kibinadamu ni udereva wa uzembe, mwendokasi, uzembe wa wapanda baiskeli na pikipiki, mifugo kuvamia barabara, uzembe wa waenda kwa miguu na wenye mikokoteni pamoja na ulevi.
Ubovu ay uchakavu wa magari pamoja na baadhi ya magari kutokuwa na taa ama kuwa na taa hafifu ni sababu zinazochangia pia ajali hizo.
Sababu za kimazingira zimetajwa kuwa ni moto, vizuizi vya barabarani, ubovu wa barabara, vivuko vya reli na uzembe wa abiria.
Yohana Sinkala, mkazi wa Kilyamatundu wilayani Sumbawanga, alisema ajali nyingi zinatokana na uzembe kwa madereva wanaokwenda kasi bila kujali kiwango cha mwisho kinachoelekezwa hata na alama za barabarani.
“Dereva anakanyaga mafuta kana kwamba anataka gari lipae kama ndege, hajali kama kuna matuta, mashimo wala kona na anapenda kuyapita magari mengine bila tahadhali… ajali ikitokea hawezi kujihami,” alisema Sinkala.
Hata hivyo, Ripoti ya Mwaka 1994 kuhusu hali ya usafiri nchini Tanzania iliwahi kubainisha kwamba japokuwa kuna vitu vitatu vinavyosababisha ajali – dereva, gari na barabara – lakini madereva hasa ndio wanaochangia ajali kutokea.
Kulingana na Ripoti hiyo, sababu kubwa ya ajali nchini Tanzania hutokana na madereva wenyewe ambapo ajali za namna hiyo ni kiasi cha asilimia 76.
“Umahiri na umakini wa kuendesha unatokana na mafunzo sahihi na utahini usiopendelea; dereva kujiandaa vya kutosha kabla ya safari; asiendeshe huku amelewa au amechoka; afuate sheria za barabarani; na uwezo wa dereva kubaini endapo gari lake lina udhaifu au kasoro,” alisema Born Again Pagan, Mtanzania aishiye nchini Marekani.
“Madereva wengine ni walevi; hupenda kunywa vileo kabla ya safari na wakati mwingine kupumzika safarini kwenye visima vya ulevi.” Alisema Mwalimu Pagan na kuongeza; “Kuna pia baadhi ya abiria wenye kutaka kufika mapema kungali na jua kule waendapo. Abiria kama hao huhimiza dereva aendeshe kwa kasi. Madereva wengine nao wanapenda sana kuendesha kwa kasi ili wapate muda wa kupumzika, na kupata angalau “moja baridi” au kuwaona wapenzi wao huko waendapo au mwisho wa safari.”
Mwalimu Pagan anasema, madereva wengine, hasa kwenye barabara zisizo na lami, wanapenda kutangulia kuepuka au kuogopa mavumbi yanayoachwa na gari liliotangulia.
“Huwa ni mashindano. Kuna wengine, hasa wamiliki, hupenda sana kushindana kuwa wa kwanza kuchukua abiria au shehena kabla ya wenzao. Tabia hii ni ya kawaida kwenye barabara zetu nyingi.”
Hata hivyo, wananchi wengine wanashusha lawama kwa askari wa usalama barabarani kwamba wanachangia kutokea kwa ajali kutokana na kusimamisha magari ovyo bila kujali eneo walilopo na hata mwendo wa gari wanalolisimamisha.
“Matrafiki wengi wanajificha pembeni ya barabara, gari likitokea likiwa kasi wanajitokeza ghafla na kulisimamisha, yote hiyo ni kutaka kuwatoza faini ama kuchukua fedha ambazo hazipelekwi kokote, ni hatari sana,” alisema Jaffari Kauzeni, mkazi wa Mlowa mkoani Dodoma.
Kauzeni alisema pia kwamba, wamiliki wa magari na madereva wamewaweka baadhi ya wakuu wa trafiki wa wilaya na mikoa mikononi, ambapo yapo madai ya baadhi ya maofisa hao kupelekewa ‘bahasha’ kila wakati ili ‘kuyalinda’ magari yao barabarani hata kama yatafanya makosa.
“Hata kama ofisa wa trafiki mdogo akimkamata mhalifu, kesi yake itafutwa na “wakubwa”.”
Lakini Ripoti hiyo ya 1994 inaelezea kuwa asilimia 7 ya ajali husababishwa na matatizo ya barabara.
Katika kukabiliana na wimbi la ajali hizo, mwaka 2015 Jeshi la Polisi lilitangaza kufuta leseni kwa madereva wote watakaosababisha ajali kwa uzembe, zikiwemo ajali zilizotokea hivi karibuni.