Zitto: Taifa Msibani, Umoja wetu na Utu wetu shakani

Jamii Africa

Jana asubuhi tarehe 10 Septemba 2011 Taifa liligubikwa na habari za kushtusha za maafa. Mwanzoni taarifa zilisambaa kwamba zaidi ya watu 2,000 walikuwa kwenye Boti MV Spice Islander lililopinduka na kuzama mbele kidogo ya Nungwi likielekea kisiwani Pemba.

Habari hazikuwa za uhakika sana kwani vyombo vyetu vya habari na hasa Televeshini ya Taifa havikuwa vikitoa habari juu ya ajali hii. Habari zilisambaa kupitia mitandao ya intaneti na kufuatia uchu wa habari nilianzisha #ZanzibarBoatAccident katika mtandao wa twitter ili tuweze kufuatilia kwa karibu habari zote za ajali hii.
Habari zilisambaa kuwa Televisheni ya Taifa ilikuwa inaonyesha muziki wa Taarab na Baadaye vipindi vingine vya kawaida bila kutoa habari kwa Umma kuhusu msiba huu.

Watanzania waliokuwa wakiwasiliana kupitia twitter na facebook walikuwa na hasira sana na kituo cha TBC1 kutoonyesha au kupasha habari juu ya ajali hii. Mpaka saa moja jioni kituo hiki cha Televisheni ya Taifa kilikuwa kinaonyesha watu wakicheza muziki wa Kongo, wanawake wakikatika viuno na hata ngoma za asili. ‘Hallo, washa TBC1 uone Televisheni yenu inachoonyesha’ yalikuwa ni maneno ya Mwakilishi Ismael Jussa Ladhu aliponipigia kuonyesha kusikitishwa kwake na kituo hiki.

Hadi jioni tulikuwa tumepata taarifa kuwa Watanzania wenzetu 198 walikuwa wamepoteza maisha. 570 hivi walikuwa wameokolewa. Binafsi nilipotembelea Hospitali ya Mnazi Mmoja niliweza kumwona Binti aliyeitwa Leyla, akisoma darasa la Nne huko kisiwani Pemba. Leyla alipona, aliokolewa. Nilimwambia Leyla atapona na kurudi shuleni.

Mpaka ninapoandika tumeambiwa kuwa Watanzania 240 wamegundulika kupoteza maisha na zaidi ya 600 wameokolewa. Napenda kuwapongeza sana waokoaji wetu, wavuvi wa kijiji cha Nungwi na vijiji jirani, wamiliki wa mahoteli waliojitolea vifaa vyao kwenda kuokoa watu na wanajeshi wetu wa majeshi ya ulinzi na usalama kwa kazi hii kubwa ya kuokoa. Kwa kweli tumeokoa watu wengi kuliko ilivyotarajiwa. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejitahidi sana, ilitulia na kuonyesha uongozi dhabiti katika juhudi za uokoaji.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akafuta ziara yake huko Canada, ziara iliyokuwa imeandaliwa muda mrefu na kwa gharama. Lakini Rais aliona ni vema kupata hasara kuliko kuwa nje ya Nchi kipindi hiki. Hakutaka hata kumtuma Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Alifuta. Akatangaza siku 3 za kuomboleza.

Hata hivyo waandaaji wa Miss Tanzania waliona hasara kubwa kuahirisha shindano la Urembo usiku huo. Wangepata hasara! Hata wafadhili wao Kampuni ya simu za mkononi ya VodaCom ambao miongoni mwa waliofariki wamo wateja wa VodaCom, waliendelea na shindano hili. Jumatatu, tarehe 12 Septemba 2011 ni siku ya khitma ya kuwaombea marehemu wetu. Nimeamua kutotumia simu yangu ya Voda kwa siku nzima, sina njia ya kuiadhibu Kampuni hii isipokuwa kugoma kutumia simu yao japo kwa siku moja kuonyesha kutoridhishwa kwangu na uamuzi wao wa kutojali msiba huu kwa Taifa.

Misiba huweka jamii pamoja. Msiba huu uliotokea Zanzibar ni jaribio kubwa kwa Umoja wa Taifa letu. Shirika la Utangazaji la Taifa limeshindwa jaribio hili la kudhihirisha Umoja wetu katika kipindi hiki. Nataraji wakubwa wa Shirika hili linaloendeshwa kwa kodi watawajibika au kuwajibishwa!

Jumla ya Majeruhi na marehemu sasa inafikia zaidi ya abiria 800! Asubuhi ya jana 10 Septemba 2011 tuliambiwa na Serikali kwamba uwezo wa Boti la MV Spice Islander ilikuwa ni abiria 500 na wafanyakazi 12. Pia tumejulishwa kuwa boti hili lilikuwa la Mizigo na sio la Abiria. Natumai mara baada ya kumaliza maombolezo haya ya siku tatu Wakuu wa Mamlaka zinazohusika na usafiri wa Majini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar watawajibika au kuwajibishwa. Mkuu wa Bandari ya Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe na Waziri wa Miundombinu Hamad Masoud wanapaswa kufukuzwa kazi mara moja kama hawatawajibika wenyewe kwa kujiuzulu.

Kufukuzwa kwao kazi hakutarudisha ndugu zetu duniani bali itakuwa ni somo kuwa hatutarudia tena kufanya makosa yaliyoleteleza ajali kama hii.

Mwenyezimungu atupe subira wakati huu wa msiba mkubwa katika Taifa letu. Alaze roho za marehemu wetu mahala pema peponi na awape unafuu wa haraka majeruhi wetu.

Makala haya yameandikwa na Mhe. Zitto Z. Kabwe (kama raia) na kusambazwa kwa vyombo vya habari

8 Comments
  • well said.binafsi nimeumizwa sana kihisia na media za bara! i hope soon nitasikia habari za kuwajibishana au kuwajibika kwa wahusika wa mamlaka zilizoshindwa kusimamia sheria.

  • Mamlaka za kusimamia usafiri nadhani hawawezi kazi zao, miaka 15 baada ya MvBukoba tulipaswa kujua jinsi ya kukabiliana na tatizo la kuzidisha uzito kwenye vyomba vya usafiri hasa wa kny maji!sasa kama wakati wa mvBukoba tulipata ajali kama hii kwa nini leo kuna mamlaka kubwa tu bado tatizo liwe kubwa kama miaka 15 iliopita.

  • Sisi huku Zanzibar tumekerwa sana na hiki kitendo cha wenzetu kutojali maafa yaliyotufika. Sio televisheni tu hata baadhi ya makampuni ya simu kama vile VODCOM Tanzania wametukwaza sana kuendelea na uchafu wao wa miss Tanzania tena live bila ya aibu wanaonesha vichupi na kucheza kiduku wakati sisi tuna majonzi. Huu si uungwana hata kidogo.

  • Binafsi si shangai mapepo na kitendo kiovu cha VODACOM wala WAANDAAJI WA MISS TANZANIA wengine,hata hivyo VIJI Miss wendawazimu,kwani jamaa hawa wanatumika na masheteni wa Freemanson kwakujijua na kwakutojijua.ki vipi?Labda niweke wazi tu makampuni mengi ya simu ni ma Agent(washirika)wa Lusifa chunguza mtaji mkuu umetokea wapi utajua.

    Angali mashindano yenyewe ni ya kuwaweka nusu uchi dada zetu na wao wanakubali kwani wamepofushwa fikra na hata watazamaji pia.Kweli ni watu wengi wanazini kwa kutamani wanawake katika mashindano hayo,.hakuna tofauti na BIGBROTHER,
    Shetani lazma angetaka shoo yake ifanyike ili afanyishe watu zambi tu, yeye hajali.

    Tanzania inahitaji mapinduzi ya KIFIKRA watu waoshwe akli,hasa wasomi wa mishahara na ubinafsi.

    Ma Miss wamesoma elimu ya makaratasi ndo maana hawajitambui kifikra ndo maana elimu ya Tz ni makapi,mtu ha jiulizi,si mzalendo, n.k

    Zitto nakupongeza kufungamanisha hili swala na umoja wetu na utu pia,kweli banadamu niwanyama ni sawa na kuku au paka utu na utashi hakuna tena.TBC ipo chini ya serikali dhalimu,hivyo inaweza ikawa iliogopa kurusha sababu ya woga wa kuiumbua serikali zembe.

    MWENYEZI MUNGU tunakuomba uzilaze roho za marehemu mahali pema peponi,AMENI”sambamba na kuwatazamia wahanga.

  • kwa upande wangu napenda kutoa pole kwa watanzania wote kwa hii ajali iliyo tukumba tumwombe mungu awape nguvu majeruhi waweze kurudia kwenye hali yao ya awali mungu bariki taifa letu

  • poleni ndugu zetu mungu awape subira na faraja katika wakati huu mgumu jueni kila jambo litokealo ni mpango wa mungu kwani alilopanga halipingiki.na hao vodacom sio wao ni ubinadamu kazi hivyo mshukuruni mungu kwa kila jambo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *