Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Mashinji kuhojiwa na DCI

Jamii Africa
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Vincent Mashinji ametakiwa kuripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinani(DCI). . Inadaiwa ameitwa ili aendelee na mahojiano kuhusu tuhuma za kutoa lugha za uchochezi alipozungumzia hali ya afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu. Dkt. Mashinji anakwenda kuripoti kipindi ambacho Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa chama hicho, Kigaila Benson anaendelea kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Katika kile kinachotajwa ni kamata kamata ya viongozi wa upinzania, leo Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dkt. Vicent Mashinji  ametakiwa kuripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai (DCI)kwa ajili ya mahojiano.

Hatua hiyo inakuja siku mbili baada Mkurugenzi  wa Operesheni na Mafunzo wa chama hicho, Kigaila Benson kulipoti Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa kadhaa ambapo ameendelea kushikiliwa na Jeshi hilo mpaka sasa.

Inaelezwa kuwa viongozi hao wa Chadema kwa nyakati tofauti walitoa kauli zenye viashiria vya uchochezi katika mikutano na vyombo vya habari Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni. Pia wamekuwa wakielezea maoni yao juu ya afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake Dodoma.

Hivi karibuni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Saimon Sirro akiwa mkoani Mbeya aliwaonya wanasiasa kuacha kuendeleza mjadala wa suala la kushambuliwa kwa Lissu na waliachie Jeshi la Polisi lifanye kazi yake ya upepelezi na kutoa majibu ya uhakika.

 Wakili wa Chadema, Fredrick Kiwhelo alipokuwa akihojiwa na chombo kimoja cha habari leo amesema bado wanashughulikia dhamana ya Kigaila na hatima yake itajulikana baadaye.

Akizungumzia suala la kuhitajika kwa Dkt. Mashinji, Wakili huyo amesema amepata taarifa hiyo leo na anaelekea katika ofisi ya DCI.

Kushikiliwa kwa viongozi hao wa Chadema ni muendelezo wa kamata  kamata ya viongozi wa vyama vya upinzania nchi ambao wengi wao wanatuhumiwa kwa vitendo vinavyodhaniwa kuwa ni vya uchochezi.  Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa viongozi hao juu ya kuzuiwa kufanya mikutano ya kisiasa, kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni na bunge kutokuonyeshwa  kwa wananchi.

Waliowahi Kukamwatwa

Septemba 24 mwaka huu, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa alikamatwa na Polisi wakatia akifanya mkutano wa hadhara katika jimbo lake na baadaye aliachiwa kwa dhamana. Wengine waliowahi kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za uchochezi ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Wengine ni Mbunge wa Arusha Mijini, Godbless Lema, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Said Kubenea (Ubungo) na  Tundu Lissu (Singida Mashariki) ambaye anakabiliwa na kesi zaidi ya 4 za uchochezi dhidi ya Jamhuri.

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *