TANGU mwaka 2010 Wilaya ya Magu mkoani Mwanza inayopakana na Ziwa Victoria imekuwa ikishuhudia matamko mengi ya wanasiasa na viongozi wa serikali wakitoa ahadi za upatikanaji wa maji.
Lakini pamoja na matamko hayo mengi, FikraPevu inatambua kwamba, mpaka sasa tatizo la maji wilayani Magu limeendelea kuwa sugu na kuwapa shida wakazi wa wilaya hiyo.
Viwango vikubwa vya bajeti zinazohusiana na uwekezaji wa maji wilayani Magu vimekuwa vikitamkwa mara kwa mara, na wananchi kuahidiwa kuwa tatizo hilo lingefikia kikomo baada ya kipindi kifupi, lakini hayo yote yameendelea kuwa historia.
Kumbukumbu za FikraPevu zinaonyesha kwamba, mwaka 2013 aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Binilith Mahenge, wakati akijibu swali la Mbunge wa Magu, Dk. Festus Limbu, alisema usanifu wa miundombinu ya maji ulifanyika kwenye baadhi ya miji ya Mkoa wa Mwanza, ukiwemo Mji wa Magu na kwamba ulitarajiwa kukamilika Juni 2013.
Alisema miradi hiyo ya Mji wa Magu na miji mingine ingehudumiwa kwa msaada wa wafadhili kwani walitarajiwa kutoa kiasi cha Shs. 214 bilioni, ambapo kati ya hizo, Shs. 24 bilioni zingegharamia miradi iliyomo ndani ya Wilaya ya Magu.
Lakini katika hali ya kushangaza tatizo la maji wilayani Magu limekuwa ni kama sehemu ya maisha, kwani limeendelea kuwa kubwa huku taarifa za Mkoa wa Mwanza zikionyesha ni 53% tu ya wakazi wa mkoa huo wanaopata maji safi lakini hali ni mbaya zaidi wilayani Magu.
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015, msemaji wa chama kimoja cha siasa alitoa kauli kwa kuwaasa wananchi wa Magu kuchagua kiongozi mwenye uwezo wa kutatua matatizo ya jamii likiwemo suala la ukosefu wa maji linaloikabili wilaya hiyo.
Hii inadhihirisha kwamba wakazi wa Magu wamekuwa wakiishi kwa matumaini huku tatizo la maji likigeuzwa kama mtaji wa kisiasa kwa vile kila wanapowachagua wawakilishi wao wanaoahidi kutatua kero hiyo, hakuna linalotekelezwa baada ya kuchaguliwa.
Kuna mipango mingi ya kibajeti ambayo imekuwepo kuanzia ngazi za halmashauri hadi taifa, lakini yote haijatekelezwa kwa miaka mingi na kuzidi kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kutopatikana kwa urahisi huduma muhimu ya maji.
Mnamo mwezi Machi 2016, Mbunge mpya wa Magu, Bonaventure Kiswaga, alinukuliwa akikiri kuwa tatizo la maji wilayani humo bado ni kubwa, huku akibainisha kwamba zimetengwa Shs. 12 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, kauli ambayo ni tofauti na iliyotolewa na Naibu Waziri Mahenge wakati wa kikao cha Bunge mwaka 2013 kwamba zilikuwa zimetengwa Shs. 24 bilioni ili kutekeleza miradi ya maji kutokana na taarifa za usanifu uliofanyika mwaka 2011.
FikraPevu inaona kwamba kuna mkanganyiko katika kauli za viongozi hao wa kisiasa, kwani katika hali ya kushangaza mbunge huyo alinukuliwa akisema upembuzi yakinifu ulitarajiwa kufanywa na kampuni COWI ambayo ilitarajiwa kukamilika mwezi Machi 2016, wakati taarifa za miaka ya nyuma zilisema upembuzi yakinifu ulikwishafanyika tangu Septemba 2011.
Kiwango cha fedha kilichotajwa na mbunge wa sasa ni tofauti karibu mara mbili ya kile cha mwaka 2011, je, hiki cha sasa kinatosheleza kuhudumia miradi yote ya maji wilayani magu? Je, nani mkweli kati ya upembuzi yakinifu uliofanywa na COWI au ule wa mwaka 2011 uliofanywa na mtaalam wa wizara? Je, kulikuwa kuna harufu ya ufisadi?
Mhandisi wa Maji wa Jiji la Mwanza, Warioba Sanya, alikaririwa mwezi Desemba 2016 akisema kwamba Wilaya ya Magu ilikuwa imetengewa Shs. 3.9 bilioni katika kutekeleza miradi ya maji, kiwango ambacho ni pungufu mara tatu zaidi ya kile kilichotajwa na mbunge. Sasa hapa nani mkweli?
Kama kauli ya Mhandisi wa Maji jijini Mwanza ni ya kweli, basi kuna uwezekano mkubwa wa maeneo mengi ya wilaya ya Magu kuendelea kutaabika na shida ya maji kuliko ilivyotegemewa, kwani ahadi na matamko mengi ya viongozi wa kisiasa hayajaleta tija yoyote kwao.
Watendaji wa serikali na wawakilishi pamoja na watu waliopewa mamlaka wanapaswa kuelewa kuna zaidi ya 46% ya wakazi wa Jiji Mwanza ambao hawapati huduma ya maji safi, achilia mbali wilaya nyingine za mkoa huo ikiwemo Magu.
FikraPevu inaona kwamba, ahadi za wanasiasa zinapaswa kutekelezwa kwa vitendo badala ya matatizo ya wananchi kutumika kama mitaji ya kujipatia kura na madaraka.