Asilimia 40 ya vyanzo maji vimeharibika, serikali kuvuna maji ya mvua kukidhi mahitaji ya wananchi

Jamii Africa
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo amesema serikali imeanzisha mfumo wa kulipia maji unaofanana na mfumo wa kulipia umeme (LUKU) unaotumiwa na TANESCO. - Ameeleza mpaka sasa Mamlaka ya Maji Iringa imeshawafungia wateja 800 na Mamlaka ya Maji Tanga imeshakamilisha kwa wateja 100. Hii itasaidia kutatua tatizo la wateja ambao hawalipi madeni yao kwa wakati.

Kutokana na ukuaji wa miji na viwanda, mahitaji ya maji nchini yameongezeka na kusababisha changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya vijijini na mijini, hali inayotishia kukwamisha juhudi za serikali kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Changamoto kuu ya upatikanaji wa maji maeneo ya mjini ni  usambazaji usio wa uhakika na gharama kubwa za kuyapata maji hayo. Hali hiyo husababishwa na ongezeko la watu ambalo haliendani na miundombinu ya usambazaji iliyopo ambayo haikidhi mahitaji ya wananchi.

Katika kukabiliana na changamoto ya maji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akiongea katika kipindi cha ‘Njoo Tuongee’ kinachorushwa na runinga moja nchini, amesema serikali inatambua kuwepo kwa changamoto ya maji lakini inashirikiana na wadau wa maendeleo kuwekeza katika miradi inayolenga kufikishia wananchi  maji safi na salama katika maeneo yao.

Amekiri kuwa kuna ongezeko la watu ambalo haliendani na vyanzo vya maji, “Maji tuliyonayo katika nchi hayaongezeki wakati idadi ya watu inaongezeka, lakini pili kwasababu ya shughuli zetu za kibinadamu tumeathiri baadhi ya vyanzo vya maji”.

“Kazi kubwa tuliyonayo ni kuhakikisha tunaelimisha wananchi kutunza na kuendeleza vyanzo vya maji”, amesema Prof. Mkumbo.

Kulingana na Utafiti wa Twaweza 2017 unaonyesha kuwa upatikanaji wa maji usio wa uhakika katika maeneo mengi ya vijijini ni matokeo ya umbali na uchache wa vyanzo maji  ambapo wananchi hutembea umbali mrefu kuyafuata maji. Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha usambazaji wa uhakika wa maji maeneo ya mjini ni asilimia 37, huku umbali wa vyanzo vya maji kwa maeneo ya vijijini ni asilimia 39.

 

Matatizo ya upatikanaji wa maji vijini na mjini  yanachangiwa na uharibifu wa vyanzo vya maji ambao unatokana na shughuli za binadamu ikiwemo kilimo, ufugaji na ujenzi wa makazi. Lakini mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yamesababisha kupungua kwa mvua za msimu na maeneo mengi ya nchi kukabiliwa na ukame.

 

Kwa mujibu wa Kituo Huru cha Takwimu za Serikali ( ) zinaonyesha asilimia 40 ya vyanzo vya maji nchini vimeharibika na havitoi maji kabisa. Kwa muktadha huo asilimia 60 iliyobaki ya vyanzo vya maji ndio vinafanya kazi. 

Juhudi za serikali kufufua na kuboresha vyanzo vya maji sio za kuridhisha ikizingatiwa kuwa  bajeti ya inayoelekezwa katika sekta ya afya ni ndogo kuweza kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali. Hali hiyo inakwamishwa na utashi mdogo wa kisiasa  ambao unaathiri vipaombele vya serikali hasa mipango na matumzi ya serikali.

Kulingana na takwimu za Shirika la Watoto Duniani (2016) zinaonyesha kuwa bajeti ya Tanzania katika sekta ya maji imeshuka kutoka bilioni 622 (4.4% ya bajeti yote) mwaka 2011/2012 hadi kufikia bilioni 574 (2.4%) mwaka 2015/2016.  Hii ni udhihirisho kuwa serikali haina nia ya dhati kutatua tatizo la maji ambalo limekuwa likikwamishwa maendeleo ya wananchi hasa wa vijijini.

Mkakati wa serikali

Serikali kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo imesema changamoto ya upatikanaji wa maji ni mbadiliko ya hali ya hewa ambayo husababisha baadhi ya maeneo kukosa mvua na kuwa na vipindi virefu vya ukame.

Amesema wanakusudia kutekeleza mradi wa uvunaji wa maji ya mvua katika Halmashauri nchini ili kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa maji wakati wote.

“Katika sera yetu ya maji tumelenga kuvuna maji ya mvua. Kama serikali tumepeleka mwongozo wa uvunaji wa maji kila Halmashauri ya Wilaya na tumewaelekeza namna ya kufanya”, amesema Prof. Mkumbo na kuongeza kuwa,

“Vilevile katika wizara yetu ili sasa kutoa mfano tumekubaliana katika kila jengo la wizara lazima kuwe na miundombinu ya uvunaji wa maji”.

 Pia amesema wataendelea kuboresha miundombinu ya maji kwa kuongeza bajeti ya maji. Pia kushirikiana na sekta binafsi kutekeleza miradi ya maji, “Tunaendelea kupambana, mpango wa kushirikisha sekta binafsi kwasababu serikali peke yake itachukua muda mrefu kufikia mahitaji yote ya maji”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *