Asimilia 43 ya watanzania kukimbilia ughaibuni wakipata fursa

Jamii Africa

Imebainika kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 6 za Afrika ambazo raia wake wanapenda kuhama na kwenda kuishi nchi zingine hasa Marekani na Ulaya ikiwa watapata fedha na fursa zitakazowawezesha kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa  Matokeo ya Utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew (2017) yanaonyesha kuwa asilimia 43 ya watanzania waliohojiwa walisema kuwa kama wangepata fedha na fursa wangependelea kuachana na nchi yao na kwenda kuishi zingine.

Hiyo ina maana kuwa, mtanzania 1 kati ya 4 kama atapata fedha au fursa anaweza kuondoka nchi na kuhamia nchi nyingine anayoipenda.

Nchi zingine ni Ghana ambayo ilishika nafasi ya kwanza kwa kupata asilimia 75, ikifuatiwa na Nigeria (74) na ya tatu ilikuwa Kenya (54). Nafasi ya nne ilishikwa na  Afrika Kusini (51), Senegal (46) na nafasi ya sita ilienda kwa Tanzania kwa asilimia 43.

Asilimia (%) ya Waafrika wanaotaka kwenda Ughaibuni

 

Maoni ya watu wa nchi ambazo wanasema wanataka kuishi nchi zingine yanafanana na tafiti zingine kama Afrobarameter  uliofanyika Nigeria na Ghana,  ambao uliuliza swali la uwezekano wa kuhama. Ukilinganisha na maeneo mengine duniani, utafiti wa  ‘Gallup polls’  ulibaini kuwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, zina idadi kubwa ya watu ambao wanapenda kuondoka katika nchi zao.

Watafiti hao waliuliza washiriki wa utafiti huo juu ya mipango ya miaka 5 ya kuhama nchi zao. Kutokana na  shauku ya kwenda kuishi nje ya nchi, asilimia 8 (sawa na kusema mtanzania 1 kati ya 8) ya watanzania walisema miaka 5 ijayo watakuwa wanaishi nje ya nchi. Huku raia wa Senegal kwa 44% ambayo ni kiwango cha juu Afrika wana mipango ya kuishi nje ya nchi yao.

Kundi ambalo linaonekana zaidi kuzikimbia nchi zao ni la vijana ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi. Kundi hili ni muhimu kwa nguvu kazi ya taifa, lakini halitulii likihaha huku na kule kutafuta fursa za kuboresha maisha.

Mipango yao itafanikiwa? Wengi wao hawatafanikiwa kuondoka katika nchi zao. Mfano, mwaka 2015, raia milioni 1.7 (sawa na 6% ya raia wote wa Ghana) walituma maombi ya Visa ya kwenda Marekani, huku idadi ya watu wanaotakiwa kupata Visa hiyo kila mwaka ni 50,000 tu duniani kote.

Kwasababu program hiyo ya Visa inawaruhusu watu wenye elimu ya juu ya Chuo, vijana wengi wanaotuma maombi wanakosa sifa hiyo. Kwa muktadha huo wanakosa sifa ya kuingia Marekani.

                      Wahamiaji wa Afrika wakiwa kwenye jahazi kuelekea Ulaya

 

Sababu zinazowasukuma kuziacha nchi zao?

Sababu zinazowasukuma watu kuziacha nchi zao za Afrika na kuamua kwenda kuishi ughaibuni zinatofautiana baina ya nchi moja na nyingine; pia kutoka mtu mmoja na mwingine.

Kwanza, wakati uchumi wa Afrika ukikua kwa kiwango cha kuridhisha, nchi nyingi za bara hilo zinakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na malipo madogo kwa walioajiriwa. Hata hivyo, soko la ajira halionyeshi kuimarika siku za karibuni, jambo linalozidisha ushindani katika sekta ya ajira. Tatizo hilo pia linachangiwa zaidi na kutokuwepo kwa mipango ya kudhibiti ongezeko la idadi ya watu.

Hali hiyo huwasukuma vijana kukimbilia nchi ambazo zina mazingira mazuri ya kufanyia kazi ili kujihakikishia usalama wa kipato na maisha.

Machafuko ya kisiasa ni sababu nyingine inayowasukuma Waafrika kukimbilia nchi zingine. Mathalani, watu ambao wamepoteza makazi na kuwa wakimbizi katika nchi zao imeongezeka mara dufu hadi kufikia milioni 9 katika kipindi cha mwaka 2010 na 2016, hii ni kwa mujibu wa Shirika la wakimbizi duniani (United Nations High Commissioner for Refugees (UNHCR) estimates.

Pia idadi ya wakimbizi wa Afrika wanaoishi kwenye nchi zingine za Afrika imeongezeka hadi kufikia watu milioni 2.3 katika kipindi hicho. Katika kipindi hicho, ripoti zinaonyesha kuwa watu hao kati ya 400,000 hadi milioni 1 wanapatikana Libya; baadhi yao wanauzwa kama watumwa na kuwekwa jela kama vifaa.

Sababu nyingine ambayo ina nguvu, ni kwamba watu wanaotaka kwenda nchi za nje hasa Marekani na Ulaya ni kwasababu wana ndugu au marafiki wanaoishi katika nchi hizo. Mathalani, asilimia 13 ya watanzania walisema wana ndugu katika nchi za Ulaya, huku 18% walisema wana ndugu au marafaiki nchini Marekani.

Wanapendelea kwenda nchi zipi?

Nchi ambazo watu hao wanapendelea kwenda ni zile za Ulaya na Marekani. Kwa nchi za Ulaya, wahamiaji ambao wamekimbia vita katika nchi zao hupendelea kwenda huko kwasababu ni rahisi kufikika kuliko Marekani.

Utafiti wa Pew umebaini kuwa asilimia kubwa ya wahamiaji hao wanapendelea kwenda Marekani kuliko Ulaya. Kwa mfano 42% ya raia wa Ghana ambao walisema wanapanga kwenda ughaibuni kwa miaka 5 ijayo, wanne kati ya 10 (41%) walichagua Marekani kama eneo la kufikia.

Inadaiwa kuwa hadi mwaka 2017, kulikuwa na watanzania wasiopungua 50,000 wanaoishi nchini Marekani. Kulingana na Idara ya Marekani ya Usalama, inaeleza kuwa kati ya mwaka 2010 hadi 2017, Waafrika 400,000 waliingia Marekani.  Kati ya hao 110,000 walikuwa wakimbizi, 190,000 walipata vibali vya kuishi kutokana na mafungamano ya kifamilia zinazoishi huko. Na 110,000 waliingia kupitia program ya  visa

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *