Benki ya Dunia (WB) imesema Tanzania ni miongoni mwa nchi kumi duniani ambazo uchumi wake unakua kwa haraka lakini inapaswa kudhibiti ongezeko la deni la taifa ili kukuza pato la ndani na kuboresha maisha ya wananchi.
Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia juu ya makisio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2018 inaiweka Tanzania miongoni mwa nchi sita za Afrika na kumi za dunia ambazo uchumi wake umeimarika na maboresho ya sera za kifedha yakifanyika zina uwezekano mkubwa wa kufikia uchumi wa kati.
Uchumi wa Tanzania ambao unakua kwa asilimia 6.8 katika nafasi ya tisa ikifuatiwa na Ufilipino (6.7) huku Ghana akichukua nafasi ya kwanza (8.3%) na kufuatiwa na nchi za Ethiopia, India, Ivory Cost, Djibouti, Cambodia, Bhutan na Senegal. Ukuaji huo unachangiwa na kuimarika kwa uzalishaji na soko mafuta, gesi na bidhaa nyingine za kilimo.
Kutokana na ukuaji huo, inatabiriwa kuwa mwaka 2018 utakuwa mzuri kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo WB inasema uchumi wa Afrika utaongezeka hadi kufikia asilimia 3.2 kutoka 2.4% mwaka 2017. Pia imetabiri uchumi kukua hadi 3.5% mwaka 2019.
Ukuaji huo utategemea zaidi kuimarika kwa bei ya bidhaa na utekelezaji wa mabadiliko ya kiuchumi yanayopendekezwa na mashirika ya kimataifa likiwemo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Lakini WB inafikiri kuwa anguko la bei ya bidhaa, usimamizi mbovu wa madeni kwa baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania inaweza kuwa kikwazo kwa uchumi kuimarika na kukua kwa muda mrefu ujao.
Hata hivyo, taasisi ya Brookings katika ripoti yake ya 2018 juu ya makisio ya uchumi inaeleza kuwa uchumi wa nusu ya nchi za Afrika utakua zaidi ukilinganisha na hali ilivyo kuwa mwaka 2014 ambapo kulikuwa na anguko kubwa la bei ya bidhaa.
Ukuaji wa uchumi wa Afrika umefikia asilimia 5 ukiondoa nchi tatu zenye uchumi mkubwa; Nigeria, Angola na Afrika Kusini ambazo zinafaidika na kupanda kwa bei ya mafuta.
NCHI 10 AMBAZO UCHUMI WAKE UNAKUA KWA HARAKA
Benki ya Dunia na Brookings zimeonya kuwa nchi za Afrika bila kujali ukubwa na ukuaji wa uchumi zinapaswa kuwa makini na jinsi zinavyosimamia madeni kwa mwaka 2018. Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Christine Lagarde akihojiwa na vyombo vya habari vya kimataifa aliweka bayana kuwa nchi husika zinapaswa kurekebisha sera za upokeaji wa mikopo ili kuziepusha na riba isiyolipika.
Deni la Afrika limefikia asilimia 56 mwaka 2017 kutokana 40% mwaka 2013 na limezidi 25% ya nchi zinazotegemea mafuta. Kwa Tanzania deni la ndani limeongezeka kutoka trilioni 10.01 hadi trilioni 12.37 Septemba 2017.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango akiwa bungeni mwezi Novemba mwaka jana alikiri deni la taifa kuongezaka kutoka Dola za Marekani bilioni 22.3 mwaka 2016 hadi kufikia dola bilioni 26 mwezi Juni 2017 ambapo ni ongezeko la asilimia 17 chini ya kiwango cha kimataifa cha kutokupesheka cha asilimia 56. Fedha za mikopo zinaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo inayoratibiwa na serikali katika maeneo mbalimbali nchini.
Serikali imeendelea ni mikakati ya ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge), mtandao wa barabara, ujenzi wa viwanja vya ndege na mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar Es Salaam ambapo itakuza uwekezaji nchini, biashara kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.
Lagarde na Brookings wanaamini kuwa kutakuwa na masharti magumu ya sera za kiuchumi kwa nchi zilizoendelea kwa miezi ijayo ambapo zitaathiri uchumi wa Afrika kwa kupanda kwa viwango riba ya kubadilisha fedha na mikopo inayotolewa na nchi hizo.
Nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania zimetakiwa kuchukua tahadhari mapema kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi na matumizi mazuri ya fedha ili kukabiliana mabadiliko ya kiuchumi katika nchi zilizoendelea.
IMF yaionya Tanzania tena
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) mwishoni mwa wiki lilijitokeza tena kuionya Tanzania kuhusu kusinyaa kwa uchumi wa Tanzania ambapo limesema serikali inatakiwa kuchukua hatua muhimu ikiwemo kutengeneza mazuri ya kufanya biashara, kuimarisha sekta binafsi, kuboresha miundombinu ya usafiri na mfumo wa kodi ili kuongeza mapato katika sekta za uzalishaji.