Boti za Karume zapotea Ndagoni-Pemba

Maryam Talib

MSAADA wa aliyekuwa rais wa awamu ya sita wa serikali ya Zanzibar, Abeid Amani Karume, umepotea katika mazingira ya kutatanisha.

Msaada huo ni boti mbili za kuvulia samaki zilizokabidhiwa kwa Kamati ya Uvuvi ya Shehia ya Ndagoni, wilaya ya Chake Chake, Pemba.

Boti hizo za injini pamoja na makokoro mawili, zilitolewa kupitia Idara ya Uvuvi Pemba, zikilenga kukuza maendeleo ya sekta ya uvuvi katika shehia hiyo na kuinua kipato cha wananchi.

Sherehe ya kukabidhi vifaa hivyo ilifanyika kwenye uwanja wa michezo wa Gombani, kisiwani Pemba, Oktoba 2005.

Katibu wa kamati ya uvuvi, Haji Hamad Kwale amethibitisha kupewa zana hizo za uvuvi; lakini anasema hawakupewa stakabadhi.

“Kwa sasa boti zote “zimekufa, zimepotea baharini na mashinemoja imekufa. Imebaki moja tu,” anaeleza Kwale.

Amesema mashine moja iliyobaki imekodishwa kwa mwanakamati mwenzao, akiongeza kwa sauti ya kusononeka, “Japo hilo halikuwa lengo la zana hizo.”

Sheha wa shehia ya Ndagoni Masoud Ali Muhammed pamoja na kukiri kuwa alikuwa shuhuda wa makabidhiano na kwamba kamati iliyokabidhiwa vifaa ilikuwa ya watu 11, anasema hajui vilipo vifaa hivyo.

Amesema akiwa mwenye dhamana ya maendeleo ya shehia hiyo, ameshafuatilia kila mahali alipoambiwa na kamati hiyo kwamba vifaa vimewekwa, ikiwa ni pamoja na ufukweni vinakopashwa kuegeshwa, lakini hajavipata.

Bali anakiri kuona mshine moja anayosema aliambiwa kuwa imekodishwa. Hakuona mashine ya pili, boti wala nyavu.

Kuhusu uwezekano wa kufa au kupotea kwa vifaa hivyo, sheha huyo alisema hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha kufa au kupotea kwa vifaa hivyo kwa sababu havikuripotiwa katika chombo chohote cha usalama wala idara ya uvuvi, jambo ambalo linatia shaka juu ya ukweli wa kauli zinazotolewa na wanakamati ya uvuvi.

Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi kisiwani Pemba, Sharif Muhammed Faki amesema kamati hiyo ilipatiwa zana za uvuvi ili wafanye kazi kwa maslahi ya jamii yao ya Ndagoni kwa lengo la kupunguza umasikini.

“Walitakiwa kuvitumia vifaa hivyo kuvua bahari kuu ili kipato kitachopatikana kisaidie kulipa kazi waliyofanya na ziada ifunguliwe akaunti benki ili iweze kununua vifaa zaidi na kuwanufaisha wavuvi wengi zaidi wa shehia hiyo,” ameeleza Faki.

Hata hivyo, amesema hadi sasa hana taarifa yoyote ya maendeleo ya mradi huo katika kijiji cha Ndagoni na ameahidi “kufuatilia.”

Katibu wa kamati ya watu 11 ya uvuvi (jina) alipotakiwa kuonesha zilipo boti zilizokufa ili mwandishi azipige picha, alisema “…ziko mbali mno si rahisi kwa mtu kama wewe kufika huko. Naweza kukupeleka huko siku nyingine.”

Hata hivyo, ufuatiliaji uliofanywa na mwandishi kupanga “siku nyengine” ya kuziona boti hizo haukufanikiwa kutokana na muhusika kusema kuwa yuko nje ya kisiwa cha Pemba.

Mkazi wa kijiji hicho, Ali Said ambaye ni mwalimu katika Skuli ya Msingi ya Ndagoni, ameeleza wasiwasi wake kwamba huenda kamati hiyo iliuza vifaa hivyo ili kujitafutia vyombo vyao binafsi vya uvuvi.

Mwandishi alipotaka kujua ana ushahidi gani kuhusiana na hili, Said alisema, “…jukumu la kutafuta ushahidi ni la polisi.”

Kuhusu suala la kutunisha mfuko wa shehia kutokana na kipato kilichopatikana kwa kazi za uvuvi zilizofanywa na wanakamati kwa niaba ya wanakijiji cha Ndagoni, wanakamati Mohammed Mmanga na Ali Mohammed Kwale wanadai kuwa kwa muda wote waliokuwa na boti hizo, hawakuwahi kupata kipato cha kufungulia akaunti au kuweka akiba yoyote.

Mmanga amesema walichopata kilikuwa kinatosha tu kulipia kazi za uvuvi za wanakamati na hapakuwepo na ziada.

Naye Kwale amesema walishindwa kujipatia kipato cha akiba kwa sababu walipopatiwa boti hizo walitakiwa kufanya uvuvi wa bahari kuu wakati wao walikuwa wamezoea kufanya uvuvi wa dagaa, mambo ambayo yanatofautiana sana.

Amesema maisha yake binafsi na kipato alichopata wakati wakisimamia boti hizo, kilikuwa duni zaidi kuliko sasa ambapo anaendesha kazi zake nje ya kamati ya uvuvi kwa kutumia mtumbwi wake binafsi.

“Toka nilipokabidhiwa zana hizo za uvuvi sikuwa na raha. Watu walikuwa na matarajio makubwa na walikuwa hawaachi kunibugudhi mtaani,” ameeleza Kwale.

Anasema anakaribia kusema “bora zilivyokufa;” angalau sasa anatumia uvuvi wake wa mtumbwi na anaendesha maisha yake.

Kwale anadai hajui thamani ya boti anazodai kupotea wala vifaa vingine vya uvuvi walivyopewa. Anadai pia kuwa hajui hasara halisi waliyopata.

Wanachojua kama kamati ya uvuvi, anasema ni “hati ya makabidhiano, zana za uvuvi zikiwa ziko kamili lakini bila kupewa risiti yoyote ya ununuzi.”

Amesema kwa sasa njia pekee ya kuingiza fedha kupitia mradi huo, ni mashine moja iliyokodishwa kwa mwanakamati mmoja anaejulikana kwa jina la  Muhammed Mmanga.

Naye Mmanga amekiri kukodi mashine hiyo na kuwapa ndugu zake kuifanyia kazi katika kisiwa cha Unguja. Amesema analipa Sh.100,000/= kwa mwezi kwa kamati ya kiji.

Kinacholeta utata ni kwamba hakuna mkataba wa aina yoyote wa kukodisha mashine, kati ya Kamati na yule aliyekodisha.

Wajumbe watano wa kamati waliohojiwa, hawakujua nani anakusanya fedha hizo kila mwezi; kama zinakusanywa kwa stakabadhi na jinsi zinavyotumika.

Lakini Mmanga naye ameshindwa kueleza nani anamlipa hizo Sh.100,000/=. Haikufahamika wapi zinawekwa fedha hizo, ikizingatiwa kuwa kamati haikuwahi kufungua akaunti benki.

Nae mkuu wa idara ya kifugo na maendeleo ya uvuvi Mayasa Faki alisema yeye hana taarifa ya hizo boti kupotea kwake lakini hata zingelikuwa zipo zingelikuwa hazifanyi kazi kwa kuona muda wa miaka sita zilipotolewa kuona ni mkubwa.

Msaada wa rais umeteketea. Wakazi wa Ndagoni wanaendelea kusota katika umasikini usioisha. Bado hakujaonekana hatua zozote za kukabiliana na tukio la ama uzembe au ubadhilifu katika mradi huu.

 

 

1 Comment
  • viongozi walokabidhiwa boti wote walikuwa hawana nia ya kunufaisha jamii, na mimi naungan na mwalimu ali said pia inawezekana kwamba wameuza vifaa na kama vipo kwa nini washindwe kuonyesha hata kama ni vibovu.(nasema hivi kwa kuwaelewa vizuri tu viongozi hao)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *