CDA yajieleza viwanja vya Dodoma

Sifa Lubasi

CHANGAMOTO kubwa ya upatikanaji wa viwanja ni miongoni mwa masuala yanayowasibu wakazi wa Dodoma.

Hali hiyo imepelekea malalamiko mengi miongoni mwa wananchi huku Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ikitupiwa lawama kedekede.

Kukiwa na wingi wa Madalali wa viwanja ambapo baadhi yao hushinda nje ya Ofisi za CDA wakiwa na ramani za viwanja, hati za viwanja na risiti kunazidi kuleta malalamiko yanayoonesha kuwa walio na fedha nyingi ni rahisi kwao kupata viwanja kuliko wananchi wa kawaida.

Mkazi wa Dodoma Josephine Mwaluko anasema unapokwenda CDA kwa ajili ya kuulizia namna ya kupatiwa kiwanja jibu unalopata ni kuwa kiwanja hakuna

“Cha kushangaza madalali wamekuwa na msururu wa viwanja vinavyouzwa hali inayotia mashaka kwani baadhi ya wafanyakazi wa CDA wanaingia kwenye biashara na madalali pindi viwanja vinapotolewa“ anasema.

Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa CDA, Pascas Muragili anasema kuwa, wajibu wa CDA katika mpango wa kuendeleza Mji wa Dodoma, ilikuwa kwanza kutengeneza mpango mji ili kuepusha mji wa Dodoma kujengwa kiholela na kutokana na hilo Kutokana na hilo, Serikali ilitenga maeneo ndani ya Manispaa ya Dodoma  ambayo yangepimwa kwa ajili ya makazi na shughuli
nyingine.

Anasema kuwa, CDA ililenga utayarishaji wa Mpango Kabambe wa uendelezaji Mji Mkuu na baada ya kuandaa mpango huo Mamlaka ilianza kazi ya usanifu, upimaji na ugawaji wa maeneo mbalimbali ya Mji Mkuu.

Muragili anataja lengo lingine lilikuwa ni pamoja na kupima ardhi yote ya mji wa Dodoma, kusimamia ujenzi wa nyumba za Serikali kwa vile wizara kwa ajili ya kuhamia Dodoma pamoja na kuweka miundo mbinu ya barabara jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limefanikiwa.

“Moja ya malalamiko hayo ya wananchi ni CDA kuchelewa kutoa hati za viwanja, wananchi kutopimiwa viwanja badala yake wanabomolewa nyumba zao na kuhamishwa” anasema.

Anataja malalamiko mengine ya wananchi ni upotevu wa hati na kukithiri kwa madalali wa viwanja.

Muragili anasema kuwa, suala la kutopatikana kwa viwanja ni malalamiko ya muda mrefu na kero kubwa kwa wananchi, kwani kumekuwa na utamaduni wa muda mrefu wa wananchi kulipia viwanja kwa gharama kidogo sana kwani miaka ya nyuma gharama ya kiwanja ilikuwa ni Shilingi 20,000 katika mazoea hayo lazima wananchi sasa watambue kuwa mamlaka haipimi
viwanja mpaka ipate fedha kutoka Serikali kuu.

Muragili anasema kuwa, madalali ni tatizo kubwa katika utendaji wa mamlaka hiyo kutokana na mara kwa mara kuwa na taarifa za wananchi kutapeliwa viwanja.

“Mara kadhaa wananchi wamekuwa wakihoji kama CDA haitoi viwanja madalali wanapata wapi viwanja hivyo” akahoji Muragili.

Anasema kuwa amepiga marufuku kwa madalali kuingia  ndani ya ofisi za CDA na tayari amepata majina ya watu 12 na ametoa agizo kuwa watu hao wakifika lazima wahudumiwe na wakurugenzi ili wakijulikana wametumwa basi wahusika wafike na si wawatume wao na kama ni shida yao wamaliziwe siku hiyo na kuondoka ili wasionekane tena maeneo hayo.

“Binafsi sijakamata viwanja hewa lakini kwa hili ni lazima tusaidiane kama kuna mtu anahisiwa au kuhusika atolewe taarifa ili aweze kufuatiliwa” anasema.

Anasema kuwa, kwa sasa wameomba msaada kutoka Jeshi la Polisi ili kuweza kukamata madalali hao wa viwanja ambao wamekuwa wakitembea na ramani, hati na risiti.

Anasema kuwa katikakupunguza tatizo la rushwa ndani ya mamlaka hiyo, kila mtumishi anatakiwa kuhakikisha rekodi zake zimekaa vizuri na hata pale faili linapokuwa halionekani inabidi mhusika ajieleze na kutokana na hilo tatizo la kupotea kwa mafaililimepungua sana kwani hata baadhi ya wafanyakazi tayari wamewajibishwa.

Muragili anasema kuwa wamepiga hatua kwa kufanya mawasiliano na manispaa ili kuiongozi wa eneo husika awe na wajibu wa kuhoji uendelezaji wa eneo lake.

“Sasa taarifa ziende kwa viongozi husika, madiwani wawe na ramani za sehemu husika, mwaka jana tulifanya mkutano na Madiwanikuzungumzia utendaji kazi wa pamoja na viongozi wa mitaa, vitongojui na tulifanya hivyo kwa ajili ya kuelekezana ili kuwe na utendaji shirikishi” anasema.

Hata hivyo anawataka wananchi wa mkoa wa Dodoma kuacha kutumia madalali na badala yake kufika ofisi za CDA ili kupata maelezo na taarifa mbalimbali juu ya upatikanaji wa viwanja.

1 Comment
  • Jamani Kikuyu kuna migogolo ya maeneo ambayo wananchi walikatakata na kuanza kilima CDA wakaja na kusema maeneyo hayo ni ya misitu lakini baada ya siku kazaa wakaja kupima wakadi kwamba kunamwekezaji ananunuwa eneo kahiyo wakachaguwa eneo la kalibu na balabala nikubwa sana nambaka sasa wameisha Pima wanasema mpaka utowe hela ndo upewe kiwanja naalikata mwenyewe kwanini asichangie pesa ya upimaji huyu mwana nchi ila CDA wanataka pesa nyingi ili mwana nchi ashindwe kutowa na itabidi shame wenyewe wapate maeneo je hili nalo mnaliangaliaje ninyi kama viongzi wamkowa was Dodoma au waandishi /haki za binadamu ?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *