Chadema wasiposhinda Arumeru viongozi wajiuzulu

Jamii Africa

Rekodi ya uongozi wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) linapokuja suala la uchaguzi mdogo ni rekodi mbaya na ambayo ingetosha kabisa kusababisha uongozi huo kujiuzulu mapema zaidi. Hadi hivi sasa kumekuwepo na chaguzi ndogo Tunduru, Tarime, Kiteto, Busanda, Biharamulo, Mbeya Vijijini, Igunga na Uzini. Uchaguzi wa Arumeru Mashariki utakuwa ni uchaguzi mdogo wa tisa (kama sitokuwa nimesahau nyingine) na rekodi ya CDM hadi hivi sasa ni 1-7. Endapo CDM itashindwa Arumeru Mashariki viongozi wote wa kitaifa wa chama hiki ni lazima wajiuzulu mara baadaya kushindwa huko kuthibitika.

Freeman Mbowe


Uchaguzi mdogo pekee ambapo Chadema iliweza kushinda ulikuwa ni wa Tarime kufuatia kifo cha Chacha Wangwe. Lakini miezi michache baadaye kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 Chadema ilishindwa kutetea kiti hicho na kikarudishwa CCM. Rekodi hii ni mbaya! Haiwezi kuelezewa na kukubaliwa au kufafanuliwa na kuridhisha. Unapoenda na timu au uongozi wa timu ambao unaenda kwenye mechi 8 za kimataifa na katika hizo zote timu inafungwa kuendelea na kocha na uongozi wa timu hiyo hiyo ni jambo la kushangaza. Unaweza vipi kwenda kwenye mechi nyingine ukiwategemea watu wale wale, makocha wale wale na wenye uwezo ule ule? Hata mkishinda mechi moja watu bado hawatoamini – watasema “kipofu kaona mwezi”.

Chaguzi zote ndogo zimefanyika chini ya uongozi huu huu wa CDM

Matokeo ambayo nimeyagusia tu hapo juu yametokea baada ya uongozi wa Chadema kutumia njia, mikakati, mbinu na ujuzi wao wote. Yaani kama ni makocha wametumia mbinu zote za kuhamasisha wachezaji wao na kila aina ya mbinu ya kuizidi CCM lakini bado matokeo yamekuwa ni yale yale 1-7. Kwa ufupi matokeo haya yanasema kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo chini ya uongozi wa sasa hakijapata mbinu na njia ya kushinda chaguzi hizi.

Hata tunapoangalia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010 matokeo hayakuwa mazuri kama tulivyotarajia. Wengi ambao tuliunga mkono na wale ambao ni mashabiki wa CDM tulitarajia kwa CDM kufanya vizuri zaidi. Tayari tuliona matatizo ya maandalizi pale ambapo baadhi ya majimbo ambayo CDM ilitarajiwa kufanya vizuri wagombea wake wakijitoa dakika za mwisho na hivyo kusababisha chama kukosa wawakilishi. Tuliona kule Mbeya kwenye uchaguzi mdogo jinsi CDM walivyojikuta kwenye hali mbaya baada ya mgombea wake kuvuruga ujazaji wa fomu!

Dk. Willibrod Slaa


Kwa mwitikio wa wananchi waliokuwa nao mwaka 2010 CDM ingeweza kufanya vizuri sana kama wangekuwa wamejiandaa na kujipanga kufanya vizuri. Bahati mbaya sana uongozi karibu mzima wa taifa wote ulikuwa unagombea nafasi mbalimbali!

Freeman Mbowe (Mwenyekiti) alikuwa anagombea Hai
Said Arfi (Makamu Mwenyekiti) alikuwa anagombea Mpanda Mjini
Wilbrod Slaa (Katibu Mkuu) alikuwa anagombea Urais
Zitto Kabwe (Naibu Katibu Mkuu) alikuwa anagombea Kigoma Kaskazini
John Mnyika alikuwa anagombea Ubungo

Tundu Lissu alikuwa anagombea Singida Mashariki na wengine ambao ni maafisa makao makuu lakini nao walitaka kujaribu kutupa karata zao kwenye Ubunge.

Sasa kwa haraka haraka tu mtu anaweza kuona kuwa mkakati wa kuwapeleka majenerali wote vitani ulikuwa ni mkakati mbaya na wenye gharama kubwa sana kwa chama hasa kwenye suala la kusimamia kampeni, kusimamia mikakati na kujibu mashambulizi. Na tuliona sana matokeo haya siku ya uchaguzi na masaa yaliyofuatia pale ambapo kwa utaalamu mkubwa (na kama tulivyotarajia) CCM iliamua kuweka presha kwenye majimbo yote ya viongozi wa makao makuu ili kuwazuia kurudi mara moja makao makuu kujipanga. Matokeo katika majimbo yote ya wagombea wa makao makuu yalicheleweshwa ili wagombea wasirudi mara moja! Gharama yake ilikuwa kubwa. Hata wabunge waliopata kwa kiasi kikubwa tunaweza kusema washukuru sana kwa sababu wengi ni wale ambao watu waliwajua na kuwakubali.

Zitto Kabwe


Lakini walipata majimbo ambayo hata hayakutarajiwa kabisa na kama yalitarajiwa ni kwa sababu ya mgombea maarufu aliyekuwa CCM akajiunga na CDM. CDM ilichukua Ukerewe, Biharamulo Magharibi, Bukombe, Meatu, Mbulu, na Mbozi Magharibi. CDM ikaonesha kuwa ni chama kinachokubalika nchi nzima na siyo cha Kaskazini kama ambavyo kilikuwa kinatuhumiwa. Ni wazi kabisa kama uongozi wa kitaifa ungekuwa umejipanga vizuri na kuamua kuweka msisitizo wa kushinda viti zaidi badala ya wao wenyewe kugombea CDM ingeweza kujikuta inafanya vizuri kupita hivyo. Lakini pamoja na matokeo yale bado hakuna kuwajibika kwa sababu wapo walioamini kuwa matokeo yale yaliakisi kweli hali halisi.

CCM, NEC na Serikali kulaumiwa

Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa madai ya kuwa CCM na serikali inawaonea na kuwa inachakachua yana nguvu kwenye uchaguzi mmoja au miwili lakini kwenye chaguzi nane madai haya sasa yamepoteza nguvu. Inakuwaje timu inaenda kucheza na timu ile ile wanafungwa na kila siku wanalalamikia refarii? Wakati kila wakati wanajua refarii ni nani na wanaenda wakiamini labda atakuwa amebadilika? Hivi, Tume ya TAifa ya Uchaguzi imebadilishwa lini? Inaongozwa vipi? Uchaguzi wa Arumeru ni uchaguzi ambao utasimamiwa na tume tofauti lakini ikiwa na sheria ile ile na tamaduni zile zile na hili CDM wanalifahamu!

Sasa sisemi kuwa hakuna vitendo vibaya vinafanyika au CDM kuonewa na TBC au na vyombo vya serikali; hili lote sote tunalijua. Hakuna geni katika hili. Itashangaza kuona vyombo hivi vikiwa huru wakati vinategemea uwepo wake kwenye CCM. CDM inajua NEC haiwezi kuwa huru kabisa, CDM inajua televisheni ya taifa haiwezi kuionesha kwa mwanga mzuri; na inajulikana kabisa kuwa polisi hawawatendei CDM kama wanavyowatendea CCM. Lakini mara zote nane (tisa ukijumlisha uchaguzi mkuu) CDM wameshariki uchaguzi chini ya viongozi hawa hawa!

Viongozi hawa hawa wa kitaifa wameendelea kukubali kupeleka timu kwenye mechi ambayo wanajua kabisa ni vigumu sana kwao kushinda. Na wakishindwa waanze kulalamikia uwanja, marefa, washangiliaji n.k. Hili halina mashiko tena. CDM imekubali kushiriki mchezo chini ya sheria zilizopo na chini ya marefa waliopo CDM iwe tayari kukubali matokeo yake. Kama haitaki kuonewa CDM isishiriki – hili haliwezekani kufanyika. Hadi leo hii CDM haijawahi kufungua kesi yoyote ya kikatiba kupinga sheria hizi mbaya au hata kujaribu kuzuia uchaguzi usifanyike – na kwa kweli sasa hivi ni ngumu kwao kuweza kusema hili wakaonekana wanaaminika. Iweje waone ubaya wa tume, sheria au polisi baada ya chaguzi nane?

John Mnyika


CDM haiwezi kushinda kwa kujifananisha na CCM

Mojawapo ya matatizo ambayo tumeyaona kwenye chaguzi hizi ndogo ni kuwa CDM inajaribu kuwa kama CCM. Wakati CCM na mashabiki zake wanatumia nguvu zaidi – za dola na vinginevyo ili kushinda CDM nayo inajaribu kuwa kama CCM. Matokeo yake ni kuwa katika hilo CCM inakuwa na ujiko zaidi. Kwa mfano tunapoona mashabiki wa CCM wanakuwa wakorofi basin a wao wanataka kuwa wakorofi lakini wanafanya hivyo wakijua kabisa kuwa msajili wa vyama vya siasa na polisi na hata baadhi ya vyombo vya habari vitatangaza mambo ya CDM kwa ubaya zaidi kuliko ya CCM!

Leo tumeshuhudia jinsi – katika hali ya kuchanganyikiwa – viongozi wa juu wa CCM wakitumia mbinu za kashfa za kutunga na kushambulia watu badala ya hoja na matokeo yake CDM nao wanaanza kujibu hivyo hivyo. Lakini msajili anapokuja kuzungummza anazungumza kana kwamba CDM ndio wabaya na kwa kufanya hivyo anaipigia debe CCM kiaina. Angalia Mkapa anasema vitu vya ajabu kuhusu Vincent Nyerere lakini ni Vincent anayeonekana kukosa adabu huku Waziri wa Serikali akitumia ujiko wake kusema mambo ya ajabu zaidi!

Ndugu zangu, viongozi wa kitaifa wanapoacha Chama kishindane katika mazingira haya ni wao wanawajibika! Ni wao ndio waliwateua viongozi wa kampeni huko Arumeru Mashariki na tena wakawatumia wabunge wapya kabisa wakati wakongwe wa kampeni kama kina Zitto, Mnyika, Mbowe na hata Dr. Slaa wanabakia kama waunga mkono. Kampeni ya Arumeru ilitakiwa kuwekwa chini ya kamanda wa kitaifa ambaye angepiga kambi huko. Kina Msigwa na Nyerere wangekuwa makamanda wa vikosi maalum (special forces). Nitaliacha hilo kwa siku nyingine inshallah.

Kwa ufupi CDM inatakiwa ishinde Arumeru kwa kuwashangaza CCM kwa kwenda kinyume na matarajio ya CCM. Natumaini viongozi hawa wa taifa watatafuta na kupata mbinu ambayo hatujaiona katika chaguzi nane ndogo zilizopita za kuweza kuishangaza CCM. Sasa hivi vyama hivi vinafanana sana kwenye mikakati yake na kampenzi zake kiasikwamba kimahesabu matokeo bado yanaipendelea CCM! Haijalishi maelfu ya watu wanaotokea, haijalishi watu wanaonyosha vidole viwili na haijalishi maneno ya kujiamini uchaguzi unashindwa kwa mikakati na mbinu! Huwezi kushinda vita kwa mavazi na nyimbo bali kwa mikakati na mbinu. Kama mavazi peke yake yangekuwa yanashinda vita hakuna jeshi lililokuwa linaonekana vizuri kama jeshi la Gaddafi! Fikiria!

CHADEMA ina kila sababu ya kushinda Arumeru Mashariki

CDM ina nafasi kubwa zaidi ya kushinda Arumeru Mashariki kuliko labda majimbo mengine mengi yaliyowahi kuwa na uchaguzi mdogo. Arumeru Mashariki iko karibu na Jimbo la Arusha Mjini ambalo tayari linashikiliwa na CDM; liko karibu na Hai, na Moshi Mjini majimbo ambayo yote yanashikiliwa na CDM. Kwa ufupi jimbo hili limekaa katika eneo ambalo ni ngome ya kaskazini ya chama wakati ngome ya Magharibi ina Mwanza, Mara na Shinyanga wakati ngome ya Kusini ina Mbeya na Iringa. Kukaa huku kwa kijiografia kunaifanya Arumeru Mashariki kuwa na nafasi ya upendeleo kulinganisha na Uzini, Tarime, Biharamulo, Busanda, Mbeya Vijijini n.k

Sababu nyingine kubwa hata hivyo ni historia ya Arumeru Mashariki. Eneo la Meru ni eneo ambalo lina historia ya aina yake katika harakati za uhuru wa nchi yetu. Kwa haki kabisa huwezi kuzungumzia kupigania haki za wananchi wetu kabla ya uhuru bila kugusia Meru katika ule Mgogoro wa Ardhi Meru. Wameru walitambua kuwa haki zao zilikuwa zimevunjwa na utu wao kudharauliwa. Hawakuwa tayari kupiga magoti mbele ya watawala wa zama hizo. Siyo chini ya tishio la bunduki za Wajerumaini au kutii utawala wa Mwingereza. Walijitahidi kupinga na walipinga kweli kweli. Hata hivyo mwangwi wa maamukzi yale ya kikoloni bado unasikika katika tanuru hili la historia hadi hivi sasa.

Hivyo, mbegu ya upinzani kwa Meru ni mbegu ya asili. Kukataa kuburuzwa na watawala na wenye nguvu imo ndani ya Wameru tangu walipokataa wamishionari wa Kilutheri wa wakati huo! HIvyo, kuna tabia ya kukataa ambayo ni ya asili. Kwa namna fulani Wameru wanafanana na Wairaqw wa maeneo ya Mbulu na Karatu ambao nao upinzani uko ndani ya damu yao. Wameru hawahitaji kushawishiwa na watu wengine juu ya ubaya wa sera za CCM za ardhi au kushindwa kwa sera ya maji na mambo mengine. Wanajua na kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri nafasi ya kutuma ujumbe kwa watawala kama wenzao wa Mbulu, Mbozi, Mbeya Mjini, Biharamulo Mashariki na sehemu nyingine walivyofanya.

Chadema jukumu lao ni kuongoza nguvu hii ya mabadiliko na hili linahitaji uongozi wa pekee wa viongozi wa taifa na mikakati ya hali ya juu. Kushindwa Arumeru katika mazingira mazuri kama haya ni kushindwa kwa uongozi wa taifa. Hatuwezi kabisa kuwalaumu kina Nyerere, Msigwa, au viongozi wa Arumeru. Hatuwezi kuwalaumu viongozi wa chini bali viongozi wa juu wa taifa. Lakini kuwalaumu tu haitoshi tena – watatakiwa wawajibike na ninaamini wakishindwa CDM ifanye kile ambacho CCM ilifanya – kujiuzulu kwa Kamati Kuu nzima lakini iende mbele kwa kujiuzulu kwa viongozi wote wa taifa ili chama kiwe na viongozi wapya kujiandaa kuelekea 2015 na kwa chaguzi nyingine ndogo zinazokuja.

Kujiuzulu ni kuwajibika na kutoa nafasi kwa wengine kuonesha njia
Ninaposema kujiuzulu kwa viongozi wa taifa simpunguzi yeyote katika kuwajibika huku. Wote ambao wanaitwa “viongozi wa taifa” kwa maana ya kuwa ofisi zao zinahusiana na utendaji wa taifa au makao makuu watapaswa kujiuzulu endapo CDM itashindwa Arumeru. Na hapa nazungumzia kujiuzulu nafasi hizi za kitaifa na wale ambao ni wabunge waendelee na nafasi zao za Ubunge na vyeo vyao vya Ubunge. Na wale utakapoitishwa uchaguzi wa kujaza nafasi hizo mpya wale wote wenye nafasi za Ubunge wasigombee na wakitaka kugombea wawe tayari kuachia Ubunge.

Kwanini?
Lengo ni kuhakikisha kuwa Uongozi wa Taifa wa chama haufungwi tena na majukumu ya Kibunge. Hili halihitaji mabadiliko ya Katiba yanahitaji maamuzi ya pamoja ili wale wasio wabunge washike nafasi za uongozi wa chama. Hii itakuwa na faida katika kusimamiana na kuwajibishana . Lakini pia itafungua chama kutumia watu wengine ambao tayari wapo makao makuu au sehemu nyingine nchini ambao wangeweza kushika nafasi hizo za uongozi bila kuwa na wasiwasi wa kila baada ya wiki kukimbia jimboni kuangalia mambo yalivyo. Kazi za utendaji wa chama zifanywe na watendaji wa chama na wanasiasa wafanye kazi za siasa. Ukifiria utaona kuwa hili linawezekana kufanyika hata baada ya ushindi na hiyo ikawa ni zawadi ya uongozi wa sasa kwa viongozi wengine.

Mashabiki wakigeuka wapiga kura CDM itashinda!

CDM ina kila sababu ya kushinda lakini haitoshinda kwa kunuia au kuombea. CDM haiwezi kushinda kama wapiga kura wa Arumeru Mashariki hawatojitokeza kwa maelfu yao kwenda kupigia kura. Hawawezi kushinda kama watu wanafikiria “wengine” wataipigia kura. Haitoshi kujitokeza kwenye majukwaa na kushangilia mgombea au kumshangilia Dr. Slaa au Zitto au Mbowe! Haya yote yanafurahisha kwenye picha na kwenye luninga lakini yote hayana maana kama hawa wote wanaojitokeza kwa maelfu kwenye mikutano hawana kadi za kupigia kura na kama wanazo hawajui zilipo.

Binafsi napuuzia kabisa picha na mikutano ya maelfu kwani kwangu haina maana yoyote ile. Sote tunajua hata kikija kikundi cha wachekeshaji watu watajaa, ikitokea ajali watu wanajaa, ikitokea umbea fulani watu watajaa. Haijalishi watu wanaojaa kwenye mikutani kwani kwa wengi hizo ni nafasi za kuwaona viongozi wanaowasoma na kuwasikia kwenye radio au kuwaona kwenye luninga. Kwa wengine hiyo ni nafasi nyingine ya kukutana na watu mbalimbali baada ya kazi kwani hakuna mambo mengi ya kufanya – kama isingekuwa kampeni labda watu wangeenda kwenye mpira, burudani n.k Kwa hiyo kampeni ni muda wa kuburudika tu. Watu wakishangilia na kupiga kelele za “people’s power” haisaidii kumchagua Nassari!

Kuna namna moja tu ya kumfanya Nassari kuwa Mbunge – kupiga kura! Siyo kuzomea, siyo kulumbana, siyo kulipiza kisasi, siyo kukashifu wengine – kupiga kura. Kashfa haipigi kura, kuzomea hakupigi kura na malumbano hayapigi kura. Chama ambacho kitahamasisha mashabiki wake kupiga kura kwa wingi ndicho kitakachoshinda. Ngoja niwape mahesabu ya haraka haraka: Mgombea wa CCM mwaka 2010 marehemu Jeremiah Sumari alipata kura 34,661 wakati mgombea wa CDM ambaye anagombea sasa Joshua Nassari alipata kura 19,123. Tofauti kati yao ni kura 15,538.

Hii ina maana CCM inahitaji kuhamasisha mashabiki wake wale wale kujitokeza kumpigia kura mgombea wake na wakijitokeza hata wakiwa 25,000 CCM itakuwa kwenye mazingira mazuri ya kushinda. CDM hata hivyo haiwezi kutegemea wale wale waliompigia kura Nassari wajitokeze tena. Kwani hata wote wakijitokeza bado watashindwa! CDM inahitaji watu wengi zaidi na hasa wana CCM waliochoshwa na sera za CCM kuja upande huu! Ikumbukwe hata Dr. Slaa Arumeru alipata kura 21,330 wakati Rais Kikwete alipata kura 32,257. Kimahesabu tu CDM iko katika hali ngumu zaidi kuliko watu wanavyoweza kujiaminisha. HIvyo, mashabiki wa CDM Arumeru Mashariki wasidhani CDM itashinda kirahisi.

Kuna mambo ambayo wanaweza kufanya ili kuipa nafasi CDM ishinde:

a. Kwanza, watafute vitambulisho vyao vya kupigia kura. Kama hauna kitambulisho – tayari umepunguza kura!

b. Kama una kitambulisho hakikisha kiko salama. Kitambulisho cha kupiga kura ni kitambulisho cha haki yako kuzungumza na kusema. Kumbuka watawala hawaelewi Kiswahili wala Kiingereza! Wanaelewa kura tu! Kama hutopiga kura hawatajua umesema nini!

c. Muulize rafiki yako, ndugu na jamaa yako kama ana kitambulisho chake. Hakikisha kimepatikana kama. Kamwe usiuze au kumpa mtu mwingine kitambulisho chako. Kumpa mtu mwingine kitambulisho chako cha kupigia kura ni kumpa mtu sauti yako! Fikiria unampa mtu sauti yako halafu anaamua kutukana au kutozungumza kabisa! Usikubali mtu mwingine achukue kitambulisho cha ndugu au rafiki yako hata kama ikibidi kupigana pigana kutetea kitambulisho chako. Hakuna kiasi cha fedha katika dunia hii kinachoweza kulinganishwa na haki yako ya kuzungumza. Anayekubali kuuza kitambulisho chake ni mtumwa! Kwani ni mtumwa peke yake ambaye hana sauti mbele ya mtawala!

d. Siku ya kupiga kura usiondoke peke yako; hamasisha ndugu zako na jamaa zako na hata ikibidi kusaidiana usafiri kwenda kupiga kura. Hakuna ubaya kwa watu ambao mnampigia kura mtu mmoja kwenda pamoja, sheria haikatazi. Hata hivyo, unapoenda kwenye eneo la kupigia kura unaenda mwenyewe na utakapopiga kura utapiga mwenyewe! Usifikirie mwingine atapiga kura unayotamania wewe!

Lakini mwisho wa siku kama nilivyosema uongozi wa CDM unatakiwa uwe umefanya mabadiliko muhimu kujipanga vizuri ili kushinda Arumeru. Lakini kama wataenda wanavyoenda sasa na kwamba hivi wanavyofanya ndio kikomo cha uwezo wao basi wakishindwa – NI LAZIMA WAJIUZULU. Na hapa nina maana wote lazima wajiuzulu kutoa nafasi nyingine kwa viongozi wengine kuinuka kuweza kuongoza kuelekea 2015. Jamani, hata kocha anayefungwa kila mechi anafukuzwa. Ikumbukwe hawagombei “kura nyingi” kuliko uchaguzi wa 2010 – wanagombea kushinda!

Binafsi nakataa kabisa ushindi wa kimaadili (moral victory). Hakuna ushindi wa uadilifu tu – CDM inahitaji kushinda na kuchukua jimbo na kitu kingine chochote chini ya hapo ni kushindwa na uongozi mzima wa taifa utatakiwa na kwa kweli unapaswa kujiuzulu wenyewe. Chaguzi nane ndogo zilizopita zimeshatuonesha; hii ni nafasi ya mwisho kwa wao kuonesha wanaweza kushinda uchaguzi mdogo. Wakishinda, CCM kwa mara kwanza itachanganyikiwa kwani kile ambacho mganga aliseme hakiwezekani kwao kitakuwa kimewazekana.

CDM wakichukua Arumeru Mashariki – kutasababisha kile kile Kesi ya Ardhi ya Meru kilisababisha katika siasa za Tanganyika miaka sitini iliyopita! Kukatawaliwa kwa watawala na wananchi wao waliowafikiria siyo kitu.

Haijalishi wanamleta nani kufanya kampeni.
Na. M. M. Mwanakijiji


Niandikie:
[email protected]

http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/235733-more-pressure-cdm-wasiposhinda-arumeru-east-uongozi-mzima-wa-taifa-lazima-ujiuzulu-6.html

3 Comments
  • Viongozi hawaamui wao kushinda, though sera za chama ndizo zinazo fanya wananchi wakichague, sasa tatizo usimamizi wa maamuzi ya wananchi kwa kupiga kula ndilo tatizo. lakin mi sina shaka na sera za vyama, shaka kubwa ni mtu wa kusimamia sera hizo zitekelezwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *