CHADEMA yaisambaratisha ngome ya CCM, CUF

Jamii Africa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimezisambaratisha ngome za CCM na CUF, Wilayani Magu Mkoani Mwanza, baada ya viongozi wake ngazi ya wilaya wakiwemo makada zaidi ya 97 wa CCM na CUF kurudisha kadi za vyama vyao na kutangaza kujiunga rasmi na Chadema.

Miongoni mwa viongozi wa CUF aliyeyeongoza makada wenzake kutimkia Chadema ni Katibu wa chama hicho wilaya ya Magu, na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa (CUF), Dominic Bubeshi ambaye alitangaza jana jioni kujiunga rasmi na Chadema, katika mkutano mkubwa ulioongozwa na aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba wilayani Magu.

Mbali na kiongozi huyo wa CUF ambaye alisema amechoshwa na sera mbovu za chama hicho za kuungana na CCM, wafuasi wengine wa CCM waliongozwa kuhamia Chadema na kada maarufu wa chama hicho tawala wilayani Magu, ambaye pia aliwahi kugombea udiwani katika kura za maoni mwaka 2010 na kutoa upinzani mkali, Samuel Moma.

Katika mkutano huo mkubwa uliokuwa na kaulimbiu ya ‘Vua gamba, Vaa gwanda’, wananchi hao wa Magu walimhakikishia Lema na viongozi wote wa Chadema kwamba, wameungana nao katika safari na mchakamchaka wa chama hicho kikuu cha cha upinzani katika kuelekea kuingia madarakani mwaka 2015.

Akihutubia maelfu ya watu waliohudhuria mkutano huo, Lema ambaye aliongozana na makada mbali mbali wa chama chake alisema, Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete imeshindwa kabisa kuwasaidia wananchi wake katika suala zima la kuondoa umasikini, badala yake rais Kikwete amegeuka kuwa ombaomba mkubwa duniani.

Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (kushoto), akimkabidhi kadi ya Chadema, Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho, Dominic Bubeshi, ambaye alirudisha kadi ya CUF na kitambulisho chake cha Ukatibu, kisha kujiunga na Chadema kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Sabasaba mjini Magu, Mwanza, jana

Alisema, badala ya Rais Kikwete na Serikali yake kujikita kushughulikia matatizo makubwa yanayowakumba Watanzania, ukiwemo kuondoa kama si kupunguza mfumuko wa bei, umasikini wa kutupwa, ukosefu wa dawa hospitalini, maji, barabara na mambo ya ufisadi yanayoielemea nchi, kiongozi huyo ameonekana kuwa shujaa wa kuratibu safari za kwenda Bara la Ulaya kuomba asaidiwe vyandarua.

“Peoples….!, Power….!. Wananchi wa Magu leo nimekuja kuwaeleza chanzo cha tatizo la umasikini unaowaangamiza Watanzania na ninyi mkiwemo. Serikali ya CCM akiwemo mbunge wenu Dk. Festus Limbu, ndiyo wanaochangia kuwadidimiza na umasikini wa kutupwa.

“Rais Kikwete kila kukicha yeye na safari kwenda Marekani kwa Bush na Obama. Amekuwa ombaomba mkubwa, anaenda hadi kuomba neti Marekani huku akiacha madini yetu yanaibiwa na Wazungu.

“Kikwete amekuwa akipishana na ndege angani zilizobeba madini yenu, yeye anatoka Ulaya anawaletea nei. Kama si kushindwa kuongoza ni nini?. Nawaombeni njooni mjiunge Chadema tupige pamoja mwendo wa kuwakomboa Watanzania ifikapo uchaguzi wa 2015”, alisema Lema kisha kushangiliwa na umati mkubwa huo wa watu.

mkutanoni-magu

Lema anamsikiliza Bubeshi baada ya kumkabidhi kadi ya Chadema, kisha kuanza kumwaga sera za kuiponda CUF kukubali kuwa CCM ‘B’.

Hata hivyo, Lema ambaye alikuwa amevalia kombati nyeusi siku hiyo imegundulika kiasi cha sh. trioni 9 kutoka Wizara mbali mbali hapa nchini zimeibwa na wajanja, jambo ambalo alisema Chadema haitavumilia ufisadi wa kutisha namna hiyo, na kwamba hadhani kama Rais Kikwete na Serikali yake atamaliza miaka yake ya Kikatiba iliyobaki madarakani.

“Trioni 9 zimeibwa katika Wizara tofauti ndani ya Serikali hii ya CCM. Kwa hali hii ni lazima wananchi muamke na kuanza kuikataa kabisa CCM na kuiondoa madarakani mwaka 2015. Ni afadhali vita inayotafuta haki na usawa, kuliko kuishi maisha ya kipumbavu!”, alisema kisha kushangiliwa tena, huku maelfu ya watu hao wakisikika wakisema: “CCM kwisha, na hapa Magu hatuna mbunge…aliyepo ni wa viti maalumu”.

Kwa upande mwingine, Lema ambaye pia alitumia muda mwingi kueleza maovu na uonevu alioukuta gerezani baada ya kukataa dhamana na kuridhia kwenda mahabusu kwa hiari yake, alimtaka Rais Kikwete na chama chake cha CCM kuwashinikiza kujiuzulu ubunge Mawaziri wote walioachwa kwenye Baraza jipya la Mawaziri, la sivyo wafungwa na mahabusu wote waliojela kwa tuhuma za wizi, wajiuzulu nao wizi na waachiwe huru kama ilivyokuwa kwa Mawaziri hao.

Awali, aliyekuwa diwani wa kata moja mjini Arusha, Alfonce Mawazo (CCM), aliyehamia Chadema hivi karibuni, aliwataka wananchi wa Magu kutofanya makosa ya kuichagua tena CCM katika uchaguzi ujao, kwani kufanya hivyo ni sawa na kujipiga kitanzi wenyewe, maana chama hicho tawala kimepoteza kabisa mwelekeo wa kuwaongoza vema wananchi.

Kwa upande wake, Katibu wa CUF wilaya hiyo ya Magu ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu taifa wa chama hicho, Bubeshi, aliyetimkia Chadema na kukabidhiwa kadi na Lema mkutanoni hapo, aliwashambulia kwa maneno viongozi wa CUF, na kusema viongozi hao wamekosa mwelekeo, kwani wamejitumbukiza ndani ya CCM na kuwa CCM ‘B’.

Bubeshi alisema, akiwa mwanasiasa aliyekomaa na anayeijua CUF, ameamua kuhamia Chadema ili kwenda kusaka madiliko ya kweli katika safari ya kuwakomboa Watanzania, hivyo alimkabidhi Lema kadi ya CUF na kitambulisha chake cha Ukatibu.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma, FikraPevu – Magu

18 Comments
  • Napenda kuwatangazia umma wa Watanzania kuwa mwisho wa CCM a.ka chama cha mafisadi umefika.

  • ni kipindi cha mabadiliko haina haja ya kuendelea kushikwa masikio,vijana pekee ndo tutakao ikomboa nji na sio wengne

  • Kwa kifupi nimechoka kusikia ccm maana imetudhalilisha sana, zamani mtu akiokota makopo tulisema amelaaniwa au kichaa. siku hizi na hali ambavyo imekuwa watu kibao tunaokota makopo! haijulikani nani mzima nani kichaa, hii yote ni kwa sababu ya ufisadi na mfumo mbaya wa ccm. wacha CCM IKUFILIE MBALI.

  • Muhimu ni uadilifu na kuwa na uchungu na nchi yako…haijalishi umetoka chama kipi kwenda chama kipi, kwa sababu kuhama chama pekee is not a guarantee kwamba kutaleta mabadiliko though kunaweza saidia endapo wahamaji wenyewe watafanya hivyo kwa nia ya dhati kabisa ya kuleta changes……na sio bora tu wamehama alafu baadae kujikuta wanakuwa disaster kwa kuvurugana wao kwa wao!!

    Nawapongeza CHADEMA kwa kuwa chachu ya awareness kwa wananchi walio wengi!!

  • Kesho kutwa kampeni vua gamba vaa gwanda inaingia mikoa ya pwani..hakika ukombozi unako njiani

  • Ama kweli CCM imeshikwa kila kona na najaribu kuona katika maono ikianguka vibaya kuliko sanamu la Saadam Huseini

  • ccm= chai chapati na maandazi wakimwona kobe juu ya mti wanadhani kapanda mwenyewe. Francois Hollande amepunguza mshahara wake na wa mawaziri wake kwa asilimia 30 halafu bwana mkubwa hapa nyumbani anafuja mali na kuomba misaada huko. ni jambo la kipumbavu kudhani kwamba nchi yetu itaendelea kwa misaada na sijui ni linni kikwete atakoma kutupeleka kwenye kwapa za marekani?

  • TUSIPOUTAMBUA UKWELI IPO SIKU UKWELI HAUTATUTAMBU, MAKAMANDA WPO NDAN YA GWANDA WANANCHI ACHENI KUGANDA MOVEMENT FOR CHANGE ILIZALIWA ARUSHA TUNAOMBA WANANCHI MUIPOKEE MABADILIKO YA KWELI YANAKUJA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *