Chegeni asema anguko la CCM ni ujumbe toka kwa wananchi

Jamii Africa

ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Busega Wilayani Magu Mkoani Mwanza, Dk. Raphael Masunga Chegeni (CCM), ameinanga CCM huku akiitaka isitafute mchawi juu ya kushindwa kwake vibaya na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Jimbo la Arumeru Mashari na Kata mbali mbali kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Aprili mosi mwaka 2012.

Amesema, mchawi hasa wa aliyesababisha chama hicho kuangukia ‘pua’ katika uchaguzi huo mdogo ni CCM yenyewe, na kwamba matokeo hayo ni dalili mbaya ambapo yanaweza kukikumba chama hicho kikongwe katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kama hakitajirekebisha na kuwasikiliza wananchi wanataka nini.

Dk. Chegeni ameyasema hayo leo hii Jijini Mwanza, wakati alipokuwa akizungumza ana kwa ana na FikraPevu ofisini kwake, kuhusiana na tathmini yake ya uchaguzi mdogo uliompa ushindi mkubwa Joshua Nassari wa Chadema, na wagombea wengine wa nafasi ya udiwani na uenyekiti wa Kijiji cha Nyehunge Wilayani Sengerema mkoani hapa.

Alisema, kitendo cha ngome kuu za CCM kuanza kuchukuliwa na wapinzani, ni ishara ya wazi kwamba chama tawala kinatakiwa kujitathmini na kujisahihisha makosa yake, ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo mpya wa namna ya kumpata mgombea kupitia kura za uwiano ambazo zimekuwa zikitumika sana katika nchi ya Rwanda na Afrika Kusini.

“CCM tusitafute mchawi kwa kushindwa na Chadema huko Arumeru Mashariki pamoja na kata. Mchawi ni sisi CCM wenyewe!. Wakati umefika sasa chama kiondokane na mfumo wa kura za maoni wa kumpata mgombea, baadhi ya wagombea wanapitishwa lakini hawakubaliki kwa wananchi.

“CCM tunapaswa turuhusu kura za wawakilishi au kura za uwiano. Si haya tu, tunapaswa kusiangalie tulipoangukia bali tuangalie tulipojikwaa. Inauma na kusikitisha sana. Tusipojirekebisha, kipingo kingine tunaweza kukipata huko mbeleni.

“Kama ngome za CCM zimeanza kwenda na wapinzani kwa namna hivi, sasa hii ni hatari na ni dalili mbaya kabisa kwa chama changu katika chaguzi zijazo!. Viongozi wetu wajiulize, je ilani inatekelezwa sawasawa?. Je ahadi ya maisha bora imetekelezwa sawasawa?”, alisema Dk. Chegeni huku akieleza kusikitishwa na kitendo cha CCM kushindwa Arumeru Mashariki.

Hata hivyo, Dk. Chegeni ambaye alikuwa kampeni meneja msaidizi wa kura za urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, alisema ili kukinusuru chama hicho tawala alipendekeza mambo yafuatayo; kwanza viongozi wahakikishe wanakomesha makundi ndani ya CCM, chama kiache kujadili kashfa za watu binafsi badala yake kinadi sera na ilani yake visimamiwe vema.

Mambo mengine aliyopendekeza Dk. Chegeni ambaye kwa sasa anajishughulisha na mambo ya biashara ni kukomeshwa rushwa wakati wa kura za maoni, kudhibitiwa wizi wa kura, CCM itafute ushauri kwa wazee wakiwemo waasisi wa TANU na ASP, iwabane wabunge na madiwani wake katika utekelezaji wa ahadi zao kwa wananchi pamoja na kuacha kile alichokiita longolongo zisizo na maana kwa wananchi.

Alitolea mfano kwa Jimbo la Busanda Wilayani Geita ambapo alisema: “Wakati wa uchaguzi mdogo pale Busanda, Serikali yetu ya CCM ilipeleka harakaharaka nguzo za umeme ikitafuta ushindi, lakini jiulize umeme upo Busanda au haupo?. Jibu lake haupo…sasa unategemea nini huko mbeleni?.

Hata hivyo, mbunge huyo wa zamani wa Busega alikwenda mbali na kuiomba Serikali kuacha kutoa ruzuku kwa vyama vya siasa, badala yake vyama hivyo vijitegemee kutafuta vyanzo vya mapato ya fedha za kuendeshea vyama vyao.

“Haiingii akilini vyama vya siasa viendelee kupewa ruzuku kwa kuendeshea siasa. Kinachotakiwa sasa ni Serikali yenyewe kulitafakari hili na kuachana kabisa na mtindo huu mbaya wa kutumia fedha za walipakodi kuvilipa vyama.

“Naamini kama Serikali itasitisha utoaji huu wa ruzuku, hata utitiri wa vyama utapungua. Lakini kwa sasa inawezekana mtu akaamua kuanzisha chama kwa malengo ya kutafuta fedha, na si kuwasaidia Watanzania masikini”, alisema Dk. Chegeni huku akisisitiza CCM kujitafakari upya ili iepukane na vipigo vingine katika chaguzi zijazo.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.

2 Comments
  • Ni kweli CCM yapaswa kujisahihisha,lakini vipigo inavyopata havitakwepeka hata wakirudisha azimio la Arusha,kwa sababu kuu mbili.Kwanza,wameshachelewa sana,wamekua wakitoa ahadi ambazo hawakua na uwezo wa kuzitekeleza.Pili ni swala la wakati.Binadamu ana hulka ya kuchoka/kukinai,hata katika mambo mazuri.Walibya wana hali mbaya sasa kuliko alipokuwepo gadafi,vivyo hivyo kwa wamisri,nikitaja wachache.

  • Si shangai kusikia kauli za Chegeni kwakuwa ni mawazo yake, na pengine hii inatokana na kipigo alichokipata yeye kwenye kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi, kutoka kwa Dr. Kamani. Lakini kwa nini kauli hizi zinamtoka Chegeni wakati huuu ili hali tunaelewa amekuwepo kwenye Bunge kwa mda Merefu alishindwa nini kuwasilisha hoja Binafsi kupinga Posho hizo za vyama? Ama tuseme ile kauli kwamba Mfamaji haachi kutapatapa?

    Nimwambie hata hao wanaodhania kwamba, hivyo vyama vya siasa vitakuja na tumaini jipya ni watu wanaowaza kwa ufinyu kwakuwa, nchi hii ina tabia ya kupuuzia Mawazo ya wataalam na kuachia Wanasiasa wawe waamuzi wa Mambo yao.

    Kimsingi kinacho takiwa hapa ni dira ya Taifa, tusipo heshimu na kuwa na dira ya Taifa itakuwa ni ndoto za Alinacha kuuifikia tz yenye Neema.

    Ushauri wangu Turudi tutubu na kumuangukia Mungu wetu, na kujua ni wapi tulipoanguka, kwakuwa yeye ni mwingi wa rehema atatusamehe na kutuondolea Dhambi zetu.

    Ndugu zangu wanasiasa ningreomba ninyi mkae Pembeni kana Obsavers, na jukumu lenu liwe kuhimiza tuu na sio mnakuja na hili leo watu wa CCM, kesho TLP, kesho kutwa CHADEMA, na Mtondogoo Chama cha Mjomba Mtikila DP hakika nchi haita kwenda,

    Dira ya Taifa ni Muhimu sana…..!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *