Dhiki ya kunyimwa umiliki wa ardhi miongoni mwa mabinti wa kihehe

Mwaisumbe Tukuswiga

Kwa desturi ya kabila la wahehe mtoto wa kike tangu anapozaliwa anahesabiwa kuwa ni mpita njia katika familia yake (kwamba ni lazima ataolewa hapo baadae)  na atakwenda kuendeleza ukoo mwingine hivyo hana haja ya kuhesabiwa urithi nyumbani kwa baba yake.

Kama hiyo haitoshi, pia anapoolewa mume ndiye anakuwa mmiliki wa ardhi hata kama mwanamke ndiye ametoa hela za ununuzi wa kiwanja ama shamba.

Hakuna sababu za msingi katika hilo lakini wanaume wengi pengine kwa sababu wao ndio wamesoma shule, ama mfumo dume wamekuwa wakiandikisha majina yao tu katika hati za umiliki na kama mwanamke ana watoto atamwandikisha mtoto wa kiume kama ndiye mrithi.

Yapo madai kuwa maamuzi hayo yanatokana na endapo mwanamume atafariki basi yule mwanamke anaweza kuolewa na mwanaume mwingine na mali ikapotea.

Jambo la kusikitisha zaidi ni pale mwanamke anapofariki kwani kwa mila na desturi mwanamke haruhusiwi kuzikwa nyumbani alikozaliwa (kwao) mpaka mume aidhinishe ardhi ambayo mwanamke huyo atazikwa.

Mchungaji Agness Kulanga wa kanisa la KKKT anasema “ zipo kesi nyingi tu ambazo tumeitwa tukasuluhishe katika misiba kutokana na mzozo wa mahala pa kuzika hasa mwanamke anapofariki kwa sababu mwanaume hakumaliza mahari au alimchukua binti kinyume na taratibu.

“Hii ni mila inayomdhalilisha mwanamke kwani anayedhalilika ni yule mwanamke aliyefariki huu ni ukatili kwani hakuna mwanaume ambaye anafanyiwa kitendo kama hicho”

Kuhusu umiliki wa ardhi anasema hata Biblia imeruhusu watu wote kumiliki ardhi  katika Isaya 60:21 watu wako nao watakuwa wenye haki wote, nao watairithi nchi milele: Hivyo kumnyima mwanamke kumiliki ardhi ni kumkandamiza kijinsia .

Diwani wa kata ya Miyomboni katika manispaa ya Iringa Bi Jesca Msambatavangu anasema kuna haja ya wanawake kuamka na kuanza kutafuta ardhi ya kwao binafsi bila ya kujali kama wameolewa au la .

“Wanawake wanatakiwa kuamka na kuunda vikundi vya pamoja ili waweze kununua ardhi kidogo kidogo kwani wengi wanatamani kununua ardhi ila wanashindwa kutokana na kipato chao kuwa kidogo hivyo wakijiunga kwa pamoja wanaweza kununua shamba kisha baadae wakagawana hii itawasaidia wanawake kumiliki ardhi mmoja mmoja”anasisitiza Bi Msambatavangu

Bi Lucy Mgoba mkazi wa kitwiru (38) manispaa ya Iringa  baada ya kutelekezwa na mume wake na watoto wawili miaka miaka mitano iliyopita, aliamua kujipanga na kukabiliana na tatizo lililompata kwa kuanza kufanya biashara ndogondogo ya chakula na kujiunga na vikundi vya mikopo midogo midogo huku akijibanza na watoto wake nyumbani kwa mama yake.

Akiwa huko alianza kuweka akiba  kwa kila pesa ambazo alikuwa anazipata na kujinyima anasa ili watoto wake  wapate chakula na mahitaji ya shule.

Anasema alikuwa anaishi na mume wake Dar es salaam baada ya maisha kuwa magumu wakaamua kurudi nyumbani Iringa ambako alimtelekeza.

Anashukuru Mungu kwa sasa biashara zake zimemuwezesha kununua shamba nusu ekari  na kuanza maandalizi ya ujenzi wa nyumba.

Pamoja na kuwa na nyumba ya vyumba vitano anasema tatizo lingine wanalokutano nalo wanawake katika umiliki wa ardhi ni pamoja na uelewa mdogo wa sheria ya umiliki wa ardhi pamoja na mirathi kwa wanawake walio wengi.

Hili lipo wazi  zaidi kwa kuangalia yaliyomsibu Bi Tumaini Anelea Mgege (28) .

Mwanamke huyu ambaye alijenga nyumba ya vyumba vitatu baada ya kununua kiwanja eneo la Mtwivila kwa fedha ambayo ilitokana na kuuza ubuyu na maandazi shule ya msingi iliyo jirani na nyumba aliyokuwa amepanga, anasema aliporwa nyumba hiyo baada ya kumkaribisha mume wake waishi pamoja.

Alisema baada ya kuhamia katika nyumba hiyo mgogoro mkubwa ukaikumba ndoa yake jambo lililomfanya yeye kutoroka kwenda kwa dada yake: Kwa bahati mbaya kabla hajarudi nyumbani kwake, mume wake akapata ajali katika basi ambalo alikuwa ni kondakta akafa na hapo ndipo dhuluma ilipoanza dhidi yake.

Bi Tumaini anasema alipopata taarifa ya kifo akatoka kwa dada yake kwenda Ifunda kwa wazazi wa mume wake ambako mama mkwe alimpiga kwa madai ya kuwa yeye ndiye aliye muua mume wake kwa ushirikina.

Pamoja na ndugu zake kumtetea ilishindikana kushiriki hata mazishi ya mume wake.

Msiba ulipoisha alirejea nyumbani kwake Mtwivila na kupigwa butwaa pale alipokuta nyumba ile imewekwa wapangaji walioingizwa na wakwe zake.

Baada ya kuona mambo ni magumu aliomba msaada  kutoka kwa viongozi wa dini ambao walimpeleka ofisi za serikali ya mtaa ili kuweza kupata msaada wa sheria na baada ya upande wa pili kuitwa ikaamuliwa ile nyumba iuzwe  kwa shilingi laki mbili na pesa zigawanywe kwa wote.

Kwa kutojua sheria alikubaliana nao kwa shingo upande huku akijua kabisa kuwa ardhi na nyumba ni mali yake kiuhalali na pesa ambayo nyumba hiyo inauzwa haifikii hata nusu ya gharama ambayo imetumika kujengea.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake alisema kwa ufupi kwamba mwanamke huyo ni kweli alifika katika ofisi hiyo na walita baraza wakamsikiliza na akasaini mkataba wa mauzo na kudai kuwa kama yeye angejua kama anaonewa angekata rufaa wala asingeruhusu nyumba kuuzwa .

Kwa upande wake Bi Tumaini anasema kutokana na wakwe zake kumtishia kuwa wangeondoa uhai wake endapo angechukua hatua nyingine ya kuwafikisha mahakamani aliogopa na ndiyo sababu inaliyomfanya akubaliane nao na huku akijua kuwa mnunuzi wa nyumba hiyo ni ndugu wa mume na ndiyo sababu wametaja bei hiyo ndogo.

Wanaume waliohojiwa kuhusu umiliki wa ardhi kwa wanawake hofu yao inaonekana kuzidiwa na fikra mgando zenye desturi ambazo ni ngumu kuzifuta katika ubongo wao.

Bw Robert Kinisa  anasema hakuna haja ya mke wake kuwa na ardhi yake pekee ama kumwandikisha katika urithi  kwani ardhi aliyonayo ni yao wote japokuwa hati miliki zina jina lake  huku urithi akiwa amemwandikisha mtoto wao wa kwanza wa kiume .

“Hata nikifa leo mtoto wangu atamtunza mama yake lakini hati ikiandikwa jina la mke wangu pengine nikifa ataolewa na mwanaume mwingine na kuishi naye nyumbani kwangu na kuwanyima haki watoto wangu. “Lakini pia hofu nyingine mwanamke akijua umemwandikisha katika urithi wa ardhi anaweza kukuua ufe haraka ili arithi na wanawake wengine wana kuwa na kiburi na jeuri mara tu wanapokuwa wanamiliki ardhi.” Alisema.

Mwanasheria Asifiwe Mwanjala anasema sheria inatamka wazi kwa mwanamke na mwanaume wote wana haki sawa na kwa masharti yaleyale kumiliki ardhi; na kuwa ardhi kama rasilimali kuu ya kiuchumi na kijamii inasimamiwa na kuratibiwa na sheia ya ardhi ya mwaka 1999 na sheria ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999.

Lakini anasema changamoto kubwa si ukosefu wa elimu ya sheria lakini pia ni kuwa hata wale wanawake wenye uelewa wakati mwingine wanashindwa kupata haki yao kutokana na kushindwa kulipia gharama za kuweka mwanasheria na kukosa ushahidi kwani baadhi yao wanapofungua mashtaka wanashindwa kuwa na uthibitisho wa hati ama kumbukumbu zozote za kimandishi japo wakati mwingine wanaweza kupata msaada wa mashahidi.

Kuhusu mila potofu anasema kifungu 20(2) cha sheria ya ardhi ya vijiji ya 1999 inakataza matumizi ya kanuni ya mila kandamizi na kwamba umiliki wa kimila utakuwa batili kama unawanyima wanawake haki ya kupata umiliki wa ardhi.

Mila potofu ni pamoja na zile zinazopitishwa na wanafamilia wakati wa urithi ama wakati wa talaka kwani mila na tamaduni za kihehe si rafiki kwani hazitoi fursa kwa mwanamke kumiliki ardhi.

Diwani Elizabeth Mpogole  anasema kwanza yeye mwenyewe alikuwa hajui kama sheria inamruhusu kumiliki ardhi yake binafsi kwani ardhi aliyonayo ni ya mume wake hivyo sasa amepata mwanga na anadhani ipo haja kuwasilisha hoja katika baraza la halmashauri ili wanawake wapewe kipaumbele kwenye mgao wa viwanja vinavyouzwa na manispaa .

Vurugu zinaoztokea katika jamii ya wahehe kuhusu yumiliki wa ardhi ni kinyume na sheria za nchi, kwani Msingi wa  sera ya nchi ya Tanzania 1995  mwanamke  anaweza kupata ardhi kwa njia ya urithi kutoka kwa mume au wazazi wake kama kutakuwepo na wosia na mwanamke ametajwa katika wasio basi atakuwa na haki ya kurithi.

Kama hakutakuwa na wosia basi katika mgawanyo wa mirathi mwanamke anayo haki ya kurithi ardhi pia.

Pia Mwanamke anaweza kupata ardhi kwa kugawiwa na Serikali, anaweza kuomba ardhi katika ardhi ya jumla au ya kijiji.

Sheria za Tanzania hazimnyimi mwanamke haki ya ardhi ila mfumo wetu wa kijamii hautoi fursa kwa mwanamke.

Kukabili tatizo hilo ni vyema kukaanzishwa kampeni kwa wanawake na wanaume  kufahamu haki za urithi kwa mwanamke ili kila mmoja awe  katika nafasi nzuri ya kutetea haki za wanawake wakati wa urithi na katika kuendesha maisha ya kawaida.

2 Comments
  • Hongera sana dada kwa kufungua njia ya kuwafanya wanyonge(hasa mabinti wa Kihehe) kuanza kutambua hali zao, hasa katika eneo la umiriki wa ardhi. Nikutakie kazi njema na endelea hivyohivyo inawezekana ndiyo likawa eneo lako unalotakiwa kujikita zaidi.
    Hata mimi nimepata kitu kipya sana ahsante
    Rev.Kurwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *