Elimu bure imeongeza idadi ya wanafunzi, sasa ni wakati wa kutoa elimu bora

Jamii Africa

ZAIDI ya wanafunzi milioni tatu wamejiunga na masomo mwaka 2017 ikiwa ni idadi kubwa kulinganisha na miaka iliyopita, hatua ambayo inaelezwa kwamba imechangiwa na mpango wa serikali wa kutoa elimumsingi bila malipo.

Mpango huo, ambao umeanza kutekelezwa rasmi na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli tangu mwaka 2016 umekuwa mkombozi wa wanafunzi, wazazi pamoja na walezi, ambao awali walikuwa wakishindwa kuwapeleka watoto shule kutokana na gharama.

Takwimu za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zinaeleza kwamba, kwa mwaka 2017 wanafunzi 3,670,000 wamejiunga na masomo katika ngazi ya elimu ya awali, elimu ya msingi na sekondari.

Wanafunzi wakiwa darasani ambapo wengine wamekaa chini

Wakati akiwasilisha Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake Bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi, George Simbachawene, alisema wiki iliyopita kwamba, uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali kwa mwaka 2017 umeongezeka na kufikia wanafunzi 1,345,636 ambapo idadi ya wavulana ni 664,539 na wasichana 681,097 ikilinganishwa na wanafunzi 971,716 ambapo wavulana walikuwa 480,053 na wasichana 491,663 mwaka 2016, ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 38.5.

Uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa mwaka 2017 nao umeongezeka na kufikia wanafunzi 1,842,513 ambapo wavulana ni 931,674 na wasichana 910,839 ikilinganishwa na wanafunzi 896,584 mwaka 2016.

Kwa upande wa sekondari, wanafunzi waliokuwa wameandikishwa hadi kufikia Machi 2017 walikuwa 483,072, wakiwemo wasichana 244,707 na wavulana 238,365.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 86.9 ya wanafunzi waliokuwa wameripoti shuleni kati ya wanafunzi 555,291 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2017.

Aidha, jumla ya wanafunzi wenye mahitaji maalum walioandikishwa kwa elimu ya awali ni 4,337 na darasa la kwanza hadi Machi 2017 idadi ya wanafunzi ambao wameandikishwa ilikuwa ni 6,097.

Kwa upande wa elimu sekondari, wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wenye ulemavu wa viungo mbalimbali waliojiunga kidato cha kwanza imeongezeka na kufikia 1,117 ikilinganishwa na wanafunzi 648 walioandikishwa mwaka 2016.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 41 ya wanafunzi wenye mahitaji maalum walioandikishwa kidato cha kwanza katika shule zinazoandikisha wanafunzi wenye mahitaji hayo.

Kwa kuangalia hesabu, hayo ni mafanikio makubwa katika sekta ya elimu katika jitihada za serikali kufuta ujinga pamoja na kutekeleza Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs), fursa ambayo watoto wengi walikuwa wakiikosa kutokana na gharama ikiwemo ada na michango mbalimbali.

Watanzania wengi wa kipato cha chini na cha kati ambao walishindwa kuwasomesha watoto wao kutokana na gharama za hapo awali kutokana na kikwazo cha hali zao za kiuchumi sasa hawawezi kutafuta kisingizio cha kutowapeleka watoto wao shule.

Hata hivyo, pamoja na dhamira nzuri ya serikali katika utoaji wa elimumsingi bila malipo, bado kuna changamoto kubwa inayoikabili sekta ya elimu hasa suala zima la uhaba wa walimu, maslahi duni pamoja na mikakati ya dhati katika utoaji wa elimu bora.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, akiwasilisha Bajeti ya Ofisi yake kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 alisisiza kuwa Serikali itaendelea na mpango wa kutoa Elimumsingi bila malipo.

“Tangu utekelezaji wa mpango huu uanze, Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa TShs. 18.77 bilioni kila mwezi ambapo shule za msingi 16,088 na shule za sekondari 3,602 zimenufaika na mpango huo,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Hatua hiyo ni nzuri pia hata kama kiasi hicho hakitoshelezi mahitaji kutokana na  ukweli kwamba kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanafunzi tangu kuanza kwa mpango wa elimumsingi bila malipo.

Lakini hoja kubwa ni kwamba, kukosekana kwa walimu wa kutosha ni changamoto kubwa inayoweza kuathiri azma hiyo ya serikali na kama kweli kuna dhamira ya dhati, basi ni vyema serikali ikaajiri walimu na kuwasambaza nchini kote, hasa katika shule za vijijini na pembezoni ambazo ndizo zinazoathirika zaidi.

Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka 2015, unaohusu Elimumsingi bila malipo, unampa fursa mwanafunzi kusoma na kupata elimu bila mzazi au mlezi kulipa ada wala michango ya fedha iliyokuwa inatozwa shuleni hapo awali.

Lakini pia kuna Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016 unaohusu utekelezaji wa elimumsingi bila malipo nao unatoa mwongozo wa namna ya kutekeleza mpango huo wa Elimumsingi kulingana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyozinduliwa Februari 13, 2015 na Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 imeweka utaratibu wa elimu ya awali kuwa ya lazima  na  kutolewa  kwa  watoto  wenye  umri  kati  ya miaka  mitatu  hadi  mitano  kwa  kipindi  kisichopungua mwaka mmoja.

Aidha, Sera hiyo pia imebanisha kuwa Serikali ndiyo yenye jukumu la kuweka utaratibu  wa  elimumsingi  kuwa  ya lazima  kuanzia  darasa  la  kwanza  hadi  kidato  cha  nne ambayo inatolewa kwa miaka kumi, umri wa kuanza darasa la kwanza ukiwa kati ya miaka minne hadi sita kulingana na  maendeleo  na  uwezo  wa  mtoto  kumudu  masomo katika ngazi husika.

Ili kutekeleza Sera hiyo, yapo majukumu mbalimbali ambayo yanapaswa kutekelezwa na wadau wa sekta ya elimu ili mlengwa wa elimu ambaye ni mtoto aipate na kuweza kutimiza azma yake ambayo msingi wake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa kutazama miongozo hiyo ya Sera na nyaraka, utaona kwamba dhamira ya serikali ni nzuri, isipokuwa tu itakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa elimu bora kwa kuwa walimu waliopo hawatoshi na wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa vipindi.

Vilevile, kuna uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, hivyo tunaweza kufurahia watoto kupata elimu bila malipo halafu tukajikuta tukingeneza taifa la watu wasiojua hata hisabati na masuala ya sayansi, ambayo ni muhimu kwa ujenzi wa uchumi na maendeleo ya taifa.

Ziko shule ambazo zina mwalimu mmoja wakati wanafunzi ni wengi na nyingi kati ya shule hizo hazina mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia, jambo ambalo pia linachangia walimu wengi wanaopangiwa huko kushindwa kwenda na kuishia kuripoti na kuondoka.

Kama kweli tunataka kujenga taifa bora ambalo litaiwezesha Tanzania kufikia malengo ya uchumi wa kati kufikia mwaka 2025, basi ni lazima tujikite katika kutoa elimu bora na siyo tu kushangilia elimu bila malipo ambayo matokeo yake yanaweza kuwa kuwapeleka watoto kucheza lakini hawawezi kufuta ujinga.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *