KWA Grace Ntambo, suala la kujiunga na vikundi vya akinamama au vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) ni msamiati mgeni kwani hajui kikundi chochote.
Grace (25), ambaye ni mfanyabiashara wa vyombo vya nyumbani katika Soko Kuu la Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga, anaongeza pia kwamba hofu ya kubwa ni kudaiwa madeni ya mikopo, jambo ambalo hataki kulisikia.
“Nimevisikia vikundi hivyo, lakini sikijui kikundi chochote na sina haja ya kujua, kwa sababu nimesikia maswahibu yanayowakumba watu wengi wanaojiunga navyo na kukopa. Sitaki kuishi kwa presha,” anasema.
Akiwa ameolewa na kujaliwa watoto wawili, Grace anasema ni vyema akajitahidi kudunduliza kwa mtaji wake tu kuendesha biashara, kwani anaamini siku hazifanani na ipo siku anaweza kuukuza mtaji huo.
Anasema ingawa biashara ni ngumu kwake inayohitaji mtaji mkubwa zaidi, lakini kuingia kwenye vikundi bila kujipanga ni sawa kujifilisi mwenyewe, kwa sababu mtu aweza kupata mkopo na kwa kukosa elimu akajikuta akizitumia fedha vibaya, hivyo kuingia kwenye madeni.
“Tatizo hakuna elimu ya kutosha, hasa kwa sisi wanawake. Hakuna vikundi vingi hapa, japokuwa nasikia vipi. Wanaoingia kwenye vikundi na kukopa wengi wamejikuta matatani kwa kuchukuliwa hata samani zao za nyumbani kutokana na kushindwa kulipa mikopo.
“Hii yote inatokana na ukosefu wa elimu ya ujasiriamali na pia watu kutojua wanakopa kwa sababu ya nini,” anaongeza.
WENGI WAOGA
Grace anasema kwamba, kukosekana kwa elimu na maswahibu yaliyowakumba baadhi ya watu walioshindwa kulipa mikopo, kunawafanya watu wengi – hasa akinamama – kuwa waoga kutafuta vilipo vikundi hivyo na kujiunga navyo.
“Huwezi kumpa mtaji mtu kabla ya kumpatia elimu ya kutosha kuhusu biashara anayotakiwa kuifanya. Sasa sisi wajasiriamali wadogo tunawezaje kushawishika kujiunga na vikundi hivyo vinavyotoa mikopo wakati hatujui hata nini maana ya hiyo SACCOS?” anahoji.
Anaongeza kwamba, bidhaa zake zinatokana na viwanda vidogo hasa SIDO na mtaji wake alioanzia wa Sh. 3 milioni miaka mitatu iliyopita bado haujakua na angependa awe na mtaji wa kama Sh. 10 milioni ili afanye biashara zake kwa ufanisi.
“Tunategemea zaidi kipindi cha mavuno ambapo wakulima wanakuwa na fedha na mzunguko wa biashara unakuwa mzuri. Sasa nikichukua mkopo ninatakiwa kulipa kama tulivyokubaliana bila kujali kama nimefanya biashara au la, kinyume chake watakuja kuchukua vyombo vyangu nyumbani, sidhani kama mume wangu anaweza kuruhusu hilo litokee,” anasema kwa mashaka.
Suala la kukopa benki nalo hataki kabisa kulisikia, kwani anasema huko kuna masharti magumu mno ambayo wananchi wa kawaida wanashindwa kuyamudu.
“Sijawahi kukopa huko na mtaji wangu ni juhudi zetu binafsi na mume wangu, ambaye naye ni Mmachinga. Naambiwa huko benki wanataka sijui uwe na hati ya nyumba na masharti mengine ya ajabu. Hiyo riba yake imewaacha wengi wakilia kwa sababu unakuwa kama unawafanyia biashara wenye benki. Wapi utakimbilia? Inabidi mimi niendelee kugangamala na kamtaji kangu haka,” anasema.
Lakini Grace ni miongoni mwa wananchi wengi, hasa wanawake, ambao pamoja na kuwa na nia ya kujiendeleza kiuchumi kwa kubuni miradi mbalimbali, bado hawajapatiwa elimu ya kutosha kuhusu vikundi vya ujasiriamali na SACCOS ambavyo vinatoa mikopo.
Hali hiyo imewafanya wanawake wengi waendelee kudumaa kimaendeleo huku wakifanya biashara ndogo ndogo zisizo na tija kubwa ili tu kuendeleza maisha yao ya kila siku.
VIKUNDI VINGI
Mkoa wa Rukwa una vikundi vingi vya akina mama wajasiriamali na kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, katika kipindi cha mwaka 2005/2010 jumla ya vikundi 341 vimekwishapatiwa kiasi cha Sh. 377,640,000.
Fedha hizo, kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rosweeter Kasikila (CCM) Bungeni hivi karibuni, zilitolewa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), ambapo vikundi 797 kati ya vilivyopatiwa fedha hizo ni vya wanawake.
Pamoja na wabunge wa Viti Maalum kutoka mkoani Rukwa, kama Rosweeter Kasikila na Abia Nyabakari wamekuwa wakiwahimiza akina mama wa mkoa huo kujiunga na vikundi vya ujasiriamali, lakini inaonekana elimu bado haijatolewa kwa kiasi cha kutosha, hivyo kuwanyima fursa wanawake wengi kufanya shughuli za maendeleo.
Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Sabas Katepa, anasema Halmashauri yake inajitahidi kulizungumzia suala la kuwawezesha akina mama hasa kwa kuwahimiza wajiunge na vikundi ili waweze kupatiwa mikopo, lakini bado juhudi ni ndogo.
“Tunajitahidi kuwahimiza akina mama, kupitia mikutano ya hadhara kwenye Kata zetu, wajiunge na vikundi ili wapatiwe mikopo, lakini naona zoezi hili bado linakwenda pole pole. Wapo walioanzisha vikundi na wanaendelea, lakini walio wengi bado kabisa,” anasema.
Hata hivyo, Katepa anasema kikwazo kikubwa ni kutokuwepo kwa elimu ya kutosha kwa akina mama ili waweze kujiunga na kuchukua mikopo itakayowakwamua kiuchumi na akahimiza taasisi zinazohusika ziweze kuwaelimisha wanawake badala ya kukimbilia kuwakopesha tu.
MKUU WA MKOA ANASEMAJE?
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, anasema lengo kubwa la serikali ni kumkwamua mwanamke kiuchumi, hivyo suala la kuwawezesha ni muhimu na linapewa kipaumbele.
Kuhusu kukosekana kwa elimu ya ujasiriamali, Manyanya anasema hiyo ni changamoto nyingine ambayo serikali yake inakabiliana nayo, lakini akaahidi kwamba juhudi zitafanyika kwa maendeleo ya wanawake na taifa kwa ujumla.