MWANZA IJUMAA APRILI 6, 2012, HAKIMU Mkazi Mfawidhi Mkoani Mwanza , Angelo Rumisha, amejitoa kusikiliza kesi baada ya kutuhumiwa ndani ya mahakama hiyo kwamba alimtishia bastola mtuhumiwa katika viwanja vya mahakama, tuhuma ambazo hakimu huyo ameziita majungu.
Hakimu Rumisha amejitoa katika kesi ya jinai namba 81/2011; kesi ya kughushi nyaraka za serikali kwa ajili ya kujipatia kiwanja kwa njia ya udanganyifu na kesi hiyo kuhamishiwa kwa hakimu Godfrey Mwambapa, wa mahakama ya mkoa wa Mwanza.
Hakimu Rumisha alijitoa Aprili 2 mwaka huu baada ya wakili wa mshtakiwa kuieleza mahakama kwamba mteja wake, Shida Manyama (ambaye anadaiwa kutumia jina la Selemani Mabuba), hana imani na hakimu Rumisha kwa sababu aliwahi kumtishia kwa bastola katika varanda ya mahakama hiyo.
Kabla ya kujitoa kwa maandishi, hakimu Rumisha aliiambia mahakama kwamba madai hayo hayana ukweli wowote, ni majungu na kuongeza kuwa mtuhumiwa katika kesi hiyo ana lengo la kuchelewesha kesi inayomkabili.
“ Kwa ujumla hayo ni majungu ambayo lengo lake ni kutaka kuchelewesha maamuzi ya mahakama . Hata hivyo mimi ninajitoa kusikiliza kesi hii kwa sababu sioni sababu ya kuing’ang’ania,” Rumisha aliiambia mahakama huku akihoji iwapo mlalamikaji alishatoa taarifa kituo chochote cha polisi juu ya kitendo hicho.
Alisema kitendo kilichofanywa na mtuhumiwa siyo cha kiungwana kwa sababu kinalenga kumchafulia jina ndani ya jamii.
Wakili huyo, Deo Mgengele, aliieleza mahakama kwamba Rumisha alimtishia mteja wake wakati wakiwa kwenye korido ndani ya jengo la mahakama.
Katika hatua nyingine, Mgengele aliiomba mahakama hiyo isiendelee kusikiliza kesi hiyo kwa maelezo kwamba alishaandika barua ya malalamiko kwenda kwa jaji.
Kwa upande wake, hakimu Mwambapa alitupilia mbali ombi hilo kwa maelezo kuwa faili lake halikuwa na nakala ya barua hiyo na wala hakuna kifungu chochote cha sheria kinachoweza kuzuia kesi hiyo isiendelee kusikilizwa.
Hakimu Mwambapa aliitaja kesi hiyo hadi Aprili 30 mwaka huu.
Kesi hiyo ambayo imefikia hatua ya utetezi ndiyo imesababisha mtumishi wa ardhi katika halmashauri ya Jiji la Mwanza, Asubuhi Otieno, akamatwe na kufikishwa kortini kwa tuhuma za kutoa ushahidi wa uongo mahakamani.
Imeandaliwa na na Juma Ng’oko, Mwanza