Hatari: Asilimia kubwa ya Watanzania kuugua uchizi, saratani. Wauguzi, wanafunzi, madereva wako hatarini zaidi

Jamii Africa

NI majira ya saa 11.40 alfajiri wakati ninapoparamia daladala kuelekea ofisini baada ya kumsindikiza binti yangu awahi shule kutokana na shida ya usafiri, si kwa wanafunzi bali hata kwa wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam.

Nimejijengea utaratibu wa kuondoka mapema kila siku za wiki ninapokwenda kazini tangu binti yangu huyu alipochaguliwa kujiunga na shule moja ya sekondari katikati ya jiji, ambapo kwa mazingira ninayoishi, nalazimika kumsindikiza mapema hadi nihakikishe amepata usafiri.

Kwa mantiki hiyo, huwa sioni sababu ya kurudi tena nyumbani, badala yake huamua kuunganisha kuwahi ofisini, kwa sababu ya kuogopa adha ya kugombea daladala pamoja na kukwepa foleni ambazo mara nyingi huwachelewesha watu wengi katika shughuli zao za kila siku.

“Brother usinichanganye kabisa, mimi pia nimepinda na nayajua matusi, nataka unipe fedha yangu kwa sababu umegeuka na gari, kama ulitaka nauli halali ungesubiri upande wa pili katika kituo cha kwenda mjini,” sauti ya kondakta inasikika wakati gari hili likielekea kituo cha mwisho ili ligeuze kwenda mjini.

Mara nyingi abiria wamekwishazowea kugeuka na gari ili kupata siti pamoja na kuwa na uhakika wa usafiri, kwani ukisubiri kwenye kituo chako wakati linarejea kuelekea mjini unaweza usipate nafasi hata ya kusimama kutokana na magari mengi kujaza hasa kipindi hiki cha asubuhi.

Kwa hiyo hulazimika kulipa nauli mara mbili ili kupata uhakika wa safari.

“Bwana wewe hunibabaishi, sikupi fedha yako kwa sababu nauli ninayokupa ni halali ya kwenda mjini, kama unataka nenda polisi,” abiria yule anamjibu kwa jeuri na dharau kondakta ambapo ghafla wanaanza kutukanana na kukwidana mashati.

Msamaria mmoja anaamua kumlipia nauli abiria mwenzake huku wengine wakiwaamua, lakini lugha za matusi bado zinaendelea.

Kondakta, ambaye uso wake unaonyesha makunyanzi na tongotongo kuashiria kwamba hata uso hajanawa anaonekana kushikwa na ghadhabu dhidi ya abiria huyo aliyevaa kinadhifu kabisa na kuniga tai shingoni.

“Watu wengine bwana, wewe kama umegombana na mkeo nyumbani usilete hasira zako kwenye kazi za watu, hii ni ofisi kama zilivyo ofisi nyingine,” kondakta anasema.

“Kati ya kazi na hii nayo ni kazi bwana, ni machizi tu wanaoweza kufanya kazi kama hii,” kauli iliyokosa chembe ya ustaarabu inamtoka abiria huyo kabla ya abiria wengine kuingilia kati na kumuonya kwamba siyo vyema kudharau kazi za watu.

Matukio kama haya ni ya kawaida kabisa kutokea kwenye usafiri wa daladala, iwe asubuhi, mchana au usiku, hasa katika Jiji la Dar es Salaam lenye mchanganyiko wa watu wenye tabia tofauti na shughuli tofauti pia.

“Unajua tunakoelekea ni kubaya sana, siyo ajabu machizi wakaongezeka jijini Dar es Salaam kuliko mahali pengine nchini Tanzania na uchizi siyo lazima uokote makopo, kauli yako tu inaweza kukuonyesha kwamba wewe hauko sawa,” abiria mmoja aliyeketi pembeni yangu ananieleza.

Abiria huyo, ambaye baadaye alinieleza kwamba ni daktari katika hospitali moja katika Manispaa ya Kinondoni, akasema kwamba, msongo wa mawazo unaosababishwa na ugumu wa maisha pamoja na kukosa usingizi ndiyo matatizo yanayowakabili wakazi wengi wa jijini humo.

Dar es Salaam ni mji wenye wakazi wengi zaidi nchini Tanzania na mara nyingi wanaonekana kuwa 'busy' na shughuli za uchumi kiasi kwamba baadhi yao huwa hawapati usingizi wa kutosha ikilinganishwa na mikoa ama miji mingine.

Hata hivyo, tatizo hilo linaweza kuwakumba wananchi wengi ambao hujinyima usingizi kwa sababu mbalimbali, ama wale wanaotumia muda mwingi kulala bila sababu.

“Mimi ni mtaalam wa saikolojia, nimemtazama abiria mwenzetu, japokuwa yuko nadhifu lakini anaonekana kukabiliwa na msongo wa mawazo, huyu kondakta naye anaonyesha kabisa hajapata usingizi wa kutosha, na yawezekana analala muda mfupi kabla ya kurejea tena barabarani, haya ni matatizo makubwa,” ananiambia daktari huyo ambaye anajitambulisha kwamba anaitwa Noel Peter.

Dk. Noel ananieleza kwamba, kutopata usingizi wa kutosha kuna madhara makubwa kiafya na kunaweza kumfanya mtu yeyote kubadilika kitabia hata ndani ya familia.

“Anaweza kuwa mkali bila sababu za msingi, anaweza kutoa lugha chafu bila kutegemea ingawa baadaye anaweza kujutia na matatizo mengine ya kiafya, hasa kiakili, tena basi kukosa usingizi kunafupisha umri wa kuishi,” anasema.

Kauli ya Dk. Peter haina tofauti na utafiti uliofanywa na Daniel Kripke na wenzake katika Kituo cha Scripps Clinic Sleep Center mjini La Jolla, California nchini Marekani mwaka 2002, ambaye anasema zaidi ya vifo milioni moja vya watu wazima vilivyotokea nchini Marekani, vilisababishwa na kukosa usingizi.

Tafiti kadhaa zinaonyesha kwamba, watu wanaolala kwa muda wa kati ya saa 6.5 hadi 7.5 kwa usiku mmoja wanaweza kuishi muda mrefu na kwamba wanaolala kwa muda wa saa 8 au zaidi, au wanaopata usingizi kwa chini ya saa 6.5, wanaishi muda mfupi.

Wataalam wamekuwa wakishauri kulala kwa walau saa 8 ili kujenga afya, jambo ambalo linaepusha matatizo mengi ya kiafya.

FikraPevu inafahamu kwamba, kukosa usingizi (Sleep deprivation) ni hali ya kukosa usingizi kwa kiwango kinachotakiwa ambapo wakati mwingine husababishwa na matatizo binafsi ya ukosefu wa usingizi (sleep disorders).

Dk. Peter anasema kwamba, kukosa usingizi kunaweza kusababisha matatizo ya kimaumbile, kisaikolojia na kadhalika.

“Ukosefu wa usingizi kwa ujumla unaweza kusababisha maumivu ya misuli, uoni hafifu, msongo wa mawazo, upofu usio rasmi (colour blindness), kusinzia mchana, uwezo mdogo wa kufikiri na kutafakari na hata kutojitambua,” anasema Dk. Peter.

Aidha, anasema hali hiyo husababisha pia kudhoofisha kwa kinga ya mwili, kuzimia, kuchanganyikiwa, kuona mauzauza, kuvimba mikono, kuumwa kichwa, hyperactivity, hypertension, kutokutulia, kuwashwa, kuota ndoto za kutisha kama za majinamizi, kupoteza kumbukumbu, kichefuchefu, kushindwa kutoa uamuzi kwa haraka, kutoa kauli mbovu, kuvimba koo, kupungua ama kuongezeka uzito kusiko kwa kawaida, na kuongezeka kwa hamu ya kufanya tendo la ndoa.

Wanajamii ambao wako hatarini kupata magonjwa mbalimbali kutokana na kukosa usingizi ni wanafunzi ambao wanatumia muda mwingi kujisomea hasa nyakati za usiku, wafanyakazi wa vyombo vya usafiri hasa madaladala, watu wanaolinda nyakati za usiku kwa siku kadhaa mfululizo bila kupokelewa.

Hamad Ibrahim ni kondakta wa daladala linalofanya safari zake Mbagala-Kawe jijini Dar es Salaam ambaye anakiri kwamba huwa hapati usingi wa kutosha na daima hulala kwa muda wa saa 2 au tatu kabla ya kuamka tena.

“Ninawajibika kuamsha gari saa 9:30 alfajiri, nakuja nalo kituoni ambako dereva ananifuata na kunikuta, tunafanya kazi mchana kutwa, kama kupumzika basi ni wakati wa chakula cha mchana.

“Ili tutimize hesabu ya tajiri na sisi tupate posho lazima tufanye kazi kwa bidii, lakini wakati mwingine foleni zinakwamisha malengo yetu, hivyo tunalazimika kufanya kazi hadi saa 4 au saa 5 usiku.

“Tukitoka hapo inabidi tupeleke hesabu ya tajiri, tukaegeshe gari kwenye kituo cha maffuta au popote pale, halafu tuangalie ustaarabu wa kurejea makwetu. Nafika nyumbani saa 6:30 au 7, lakini mpaka nioge, nile na usingizi unipitie itakuwa saa 8 tayari, naweka alarm kwenye simu yangu iniamshe saa 9:30, maana yake nitalala kwa saa 1:30 tu. Kweli, wakati mwingine tunatoa kauli mbovu kwa abiria siyo kwa kupenda, unajikuta tu umeropoka,” anafafanua.

Hamad anaeleza kwamba, takriban mara mbili amejikuta akifikishwa polisi kutokana na kauli hizo, ambazo mara nyingi huzijutia baada ya kuzitoa.

“Mara ya kwanza nilikuwa naendesha gari mwenyewe, kwa sababu pia ni dereva, wakati niko pale Buguruni Shell ninataka kutoka, gari moja ndogo ikaja, sikuiona, nikaibana ubavuni. Lilikuwa ni suala la kuzungumza kistaarabu, lakini nikajikuta nikimjibu yule jamaa kwa dharau, akanipeleka polisi na kwa kuwa kosa lilikuwa langu, nikalipa,” anasema.

Mara ya pili, anasema, alimtolea lugha ya kashfa mwalimu mmoja ambaye alionyesha kitambulisho katika utaratibu wa kusafiri bure, badala yake yeye akaanza kumtukana na kumwita ‘mzigo, mpenda dezo’ na maneno mengineyo, hivyo akapelekwa polisi ambako alishinda tangu asubuhi hadi saa 4 usiku.

Katika nchi nyingi duniani, kukosa usingizi miongoni mwa wanafunzi ni matatizo ya kawaida ingawa kitaalam wanapaswa kulala kati ya saa 8.5 hadi 9.25.

“Watumishi wa sekta ya afya nao wako hatarini kupata matatizo ya akili, hasa msongo wa mawazo,” anasema Dk. Luhaja Nginila.

Dk. Nginila anasema kwamba, watumishi wengi katika sekta ya afya hasa madaktari na wauguzi, ambao kutokana na uhaba wa wafanyakazi, wengi wanatumia muda mwingi wakiwa kazini kwa siku kadhaa na hata nyakati za usiku wanalazimika kuwa macho ili kuwahudumia wagonjwa – waliolazwa ama wanaokuja nyakati hizo.

“Unaweza kukuta daktari au muuguzi anakaa wodini kwa saa 72 bila kupokelewa, maana yake hata wakati wa usiku mtumishi huyu inabidi ‘aufukuze usingizi’ ili awahudumie wagonjwa, hali ambayo inamfanya hata tabia yake ibadilike.

“Anaweza kuwa na msongo wa mawazo, mkali bila sababu za msingi, anaweza kufanya makosa ambayo katika hali ya kawaida angeweza kuyaepuka, yote ni kwamba kichwa chake hakiko sawa,” anasema Dk. Ngonila.

Kwa mujibu wa Dk. Nginila, hali hiyo ndiyo wakati mwingine huwafanya baadhi ya watumishi, hasa wauguzi, wanakuwa na kauli mbovu na za kuudhi kwa wagonjwa kutokana na kukumbw ana msongo wa mawazo na fadhaa kwa kukosa usingizi muda mrefu.

“Kukosa usingizi ni tatizo sugu ambalo linasababisha hata kubadilika kwa tabia, kupunguza utashi hata katika shughuli za kawaida na kunaondoa ile hali ya kufurahia jambo lolote, unaweza kuwa mkali, hasira za mara kwa mara, unachukia bila sababu na unaweza kujichukia hata wewe mwenyewe,” anasema Dk. Nginila.

Hata hivyo, utafiti wa mwaka 1996 wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Chicago unaonyesha kwamba, ukosefu wa usingizi unaathiri kwa kiasi kikubwa mwili wa binadamu kwa kushinda kumeng’enya sukari hasa glucose, hali ambayo inaweza kusababisha hatua za awali za Saratani Type 2.

FikraPevu inatambua kwamba, utafiti uliofanywa mwaka 2000 na UCSD School of Medicine na Veterans Affairs Healthcare System jijini San Diego ulibaini kwamba kukosa usingizi kunaweza kusababisha madhara makubwa kwenye ubongo, ambao unaweza kushindwa kufanya kazi vizuri.

Aidha, utafiti uliofanywa na Taasisi ya Tiba ya Chicago mwaka 2001 ulionyesha kwamba, kukosa usingizi kunaweza kusababisha madhara makubwa kiafya, yakiwemo magonjwa ya moyo na uchizi.

Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 1999 unaonyesha kwamba, kukosa usingizi kunachangia kuzidiwa nguvu kwa muhimili mfumo wa tezi mbalimbali maarufu kama Hypothalamic-pituitary-adrenal axis (ambao ndio unaodhibiti hali kama fadhaa, msongo wa mawazo na kudhibiti shughuli za mwili kama mmeng’enyo wa chakula, mfumo wa kinga, hali ya fikra, masuala ya ngono, au matumizi ya nishati mwilini) na wakati huo unapunguza homoni za ukuaji na kusababisha udumavu.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa mwaka 2000 na Jarida la Tiba la Uingereza (British Medical Journal), watafiti nchini Australia na New Zealand waliripoti kwamba, kukosa usingizi kunaweza kusababisha madhara makubwa kama ilivyo kwa ulevi wa kupindukia.

Watu waliokuwa wakiendesha magari kwa muda wa saa 17-19 mfululizo walifanya makosa mengi zaidi ya wale ambao kiwango chao cha damu kilikuwa na ulevi wa asilimia .05, ambacho ndicho kiwango kinachoruhusiwa kisheria kwa mtu anayekunywa na kuendesha gari katika Mataifa ya Magharibi.

Hali hiyo inaelezwa kwamba ndiyo inachangia kutokea kwa ajali nyingi za barabarani kwani madereva ambao wanaendesha muda mrefu bila kupata usingizi wa kutosha huwa wanakumbwa na msongo wa mawazo, fadhaa na hawawezi kuchukua tahadhari zozote.

Aidha, kukosa usingizi kwa muda mrefu kumeripotiwa pia kusababisha madhara mengine ya kiafya ikiwemo matatizo ya hernia (ngiri maji), kuvimba kwa mishipa, na matatizo mengineyo.

Taarifa za Idara ya Usalama Barabarani nchini Marekani inaeleza kwamba, zaidi ya ajali 100,000 zinazotokea kila mwaka zinasababishwa na uchovu wa madereva pamoja na kusinzia.

Ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi nchini amethibitisha kwamba, hata ajali nyingi zinazotokea nchini kwenye barabara kuu zinachangiwa na madereva kukosa usingizi pamoja na uchovu.

“Usingizi ni ugonjwa ama chanzo kikubwa cha matatizo ya kiafya na kimwili, ndiyo maana huwa madereva wanashauriwa wakifika mahali walale muda wa kutosha, tena walale kwenye vitanda badala ya kulala kwenye magari ambako kunawaongezea uchovu na msongo wa mawazo,” amesema ofisa huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa jeshi.

Hata hivyo, ofisa huo amedokeza kwamba, usingizi wakati mwingine hutumika kama silaha ya mahojiano kwa watuhumiwa, ambapo wengi huwa wananyimwa usingizi kama njia ya kuwalazimisha kusema ukweli kwa kile wanachotuhumiwa nacho.

“Katika nchi nyingine mtuhumiwa anaweza hata akawekwa kwenye chumba chenye mwanga mkali usiozimwa, na akiwa huko hawezi kujua kama ni mchana au usiku, tena wengine wanaweza kufungiwa spika na kupigiwa muziki mfululizo,” amedokeza ofisa huyo.

FikraPevu inafahamu kwamba, wakati wa utawala wa Pinochet nchini Chile, na wakati wa Umoja wa Kisoviet, au hata katika Gereza la Guantanamo la Marekani huko Cuba, kuwanyima usingizi imekuwa silaha ambayo inatumika katika mahojiano maalum (interrogation).

Taarifa zinasema; “Watuhumiwa wanaofanyiwa mahojiano hulazimishwa wakae macho kwa siku kadhaa; na wanaporuhusiwa kulala tu, mara usingizi unapowapitia, huamshwa na kuhojiwa tena.

Menachem Begin, Waziri Mkuu wa Israeli kati ya mwaka 1977-83 alielezea kuhusu uzoefu wake namna alivyonyimwa usingizi kwa siku kadhaa wakati alipokuwa mateka wa KGB nchini Russia ambapo alisema:

“Kichwani mwa mfungwa anayehojiwa, hali fulani huanza kujitokeza. Nafsi yake inakuwa na hofu ya kifo, miguu inalegea, na  anakuwa na hamu ya jambo moja tu: kulala… Mtu yeyote ambaye amewahi kupatwa na hali hiyo anafahamu kwamba si njaa wala kiu ambavyo vinaweza kukuzuia pindi usingizi unapokunyemelea.”

Nicole Bieske, msemaji wa Amnesty International Australia, aliwahi kukaririwa akisema, "Katika hali yoyote, kumnyima mtu usingizi ni ukatili, kinyume na haki za binadamu na kunashusha hadhi ya mtu. Kama hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu basi ni mateso makubwa."

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *