Historia ya Shule ya Msingi Nachingwea imebaki katika ‘kava’ la daftari…

Mariam Mkumbaru

Historia ya shule ya msingi Kiegei katika kata ya Kiegei wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, imebaki katika kava moja tu la daftari, lakini shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vitabu, vitendea kazi vya kufundishia na walimu.

Historia-ya-shule

Historia ya shule katika 'kava' la daftari

Shule hiyo iliyojengwa mwaka 1921 na wa Wakoloni, kwa sasa iko katika hali mbaya sana, haina walimu, hakuna vitabu, hakuna makabati ya kutunzia vitabu na majengo chakavu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Fred Mchekenje alisema kuwa, shule inakabiliwa na changamoto nyingi sana kwa sasa, kuna walimu watatu tuu shule nzima na wanafunzi wako 650, hakuna vitabu vya kufundishia na kujisomea kwa wanafunzi, kwa sasa kuna vitabu 20 tu vya masomo mbalimbali shuleni hapo, pamoja na vitendea kazi kama chaki hakuna pamoja na ubao wa kuandikia umechaa maandishi hayaonekani vema.

Fred-Mchekenje

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kiegei Fred Mchekenje akinionesha historia ya shule hiyo iliyopo ndani ya kava la daftari

"Uhaba wa walimu, vitabu na vitendea kazi vya kufundishia darasani, vinachangia kushusha ufauru wa wanafunzi hapa shuleni na kuchangia ongezeko la utoro na mimba za umri mdogo kwa wanafunzi wa kike,"alisema Mchekenje.

Mchekenje alisema kuwa  mwaka 2012, matokeo ya darasa la nne yalikuwa mabaya sana, walifanya mtihani watoto 95, walifauru watoto 8 wavulana 6 na wasichana 2. Kwa sasa tunahitaji walimu 15 pamoja na vitabu 300 vya kufundishia masomo mbalimbali na chaki ya kuandikia ubaoni.

Juma Ramadhini ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo, lakini toka amenza darasa la kwanza hajawahi kusoma kitabu chochote kile zaidi ya mwalimu kuwasomea na kuandika ubaoni anapoingia darasani.

wanafunzi-vitunguu

Baadhi ya wanafunzi wakiwa darasani huku nyuma ya darasa kukiwa kumeanikwa vitunguu vya mwalimu

"Nipo darasa la tano sasa lakini sijawahi kusoma kitabu toka nimeingia darasa la kwanza, naambulia kuliona kava ya nje ya kitabu pale mwalimu apoingia darasani kutufundisha, hata kusoma pia ni tatizo kwangu nachojua ni kuandika jina langu pekee lakini kusoma kitabu au gazeti siwezi,"alisema Juma.

Kwa upande wake Afisa elimu wa shule ya msingi katika wilaya hiyo Makwasa Bulenga alisema kuwa, tatizo la ukosefu wa vitabu na walimu katika shule za msingi wilaya ya Nachingwea ni kubwa sana, ndio chanzo cha wanafunzi kuferi masomo mbalimbali kwa sababu ya kukosa vitabu na walimu shuleni.

Bulenga alisema kuwa, Mwaka 2012 wanafunzi 3,636 walifanya mtihani wa kumaliza darasa la saba, wanafunzi 10,39 ndio waliofauru kujiunga na sekondari, wavulana 583 na wasichana 456 sawa na asilimia 28.5.

"Ufaulu wa wanafunzi unashuka mwaka hadi mwaka kwa sababu ya kutokuwa na walimu na vitabu vya kufundishia kwa wilaya mzima, kwa sasa kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya 15, sasa hapo kunauwezekano wa mtoto kuelewa na kufauru inavyotakiwa,"alisema Bulenga.

Wilaya ya Nachingwea ina kata 32, kati ya hizo kata sita ziko mjini ambako kidogo kuna vitabu na walimu, lakini kata 26 za vijijini huko ndio hakuna walimu pamoja na vitabu vya kufundishia.

Idadi ya wanafunzi katika shule za mjini, wavulana 2,365 na wasichana 2,424 jumla ni wanafunzi 4,789, katika shule za vijijini idadi wa wanafunzi  wavulana 13,319 na wasichana 13,728 jumla ni 27,047.

Kwa idadi hii ya wanafunzi wa shule za vijijini, ambako hakuna vitabu, walimu na vitendea kazi je? wanafunzi watajua kusoma na kuandika na kufauru katika mitihani mbalimbali? hii ni changamoto inahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee ili tuweze kupata viongozi bora nchini hapo baadae.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *