Unapozungumzia shilingi 100 katika jiji la Dar es salaam thamani yake ni ndogo sana kutokana na hali halisi ya kupanda kwa gharama za maisha, kwani ukiwa na kiasi hicho cha pesa huwezi hata kupanda daladala kutoka kituo kimoja mpaka kingine.
Hii ni tofauti sana kwa wakazi wa kijiji cha Nyaminywiri kilichopo kata ya Kipugira wilayani Rufiji, ambapo shilingi 100 ni nauli tosha ya kumsafirisha mkazi wa eneo hilo kutoka ng’ambo moja ya mto na kumrudisha pia.
Kijiji cha Nyaminywiri kimegawanyika katika maeneo mawili kutokana na kuwepo kwa mto rufiji, eneo moja likiwa la mashambani ambapo kuna watu wanaishi huko, wakati upande mwingine ndiko huduma mhimu kama kituo cha afya, barabara, soko na shule vinapatikana.
Wakazi wa kijiji hicho wanahitaji zaidi huduma ya usafiri wa mtumbwi ili kuwapeleka ng’ambo ya pili kupata huduma mbalimbali, na wale wa upande wa mwingine, huvuka ili kwenda mashambani kulima na kununua mazao mbalimbali kama mpunga na korosho.
Tukizungumzia wakazi wa kijiji cha Nyaminywiri hatuwezi kuwasahau wanafunzi, ambao husafiri kwa siku tano mfululizo, wakienda shule na kurudi kwa kutumia mtumbwi huo, ambao ndio usafiri pekee wa kuwafikisha shuleni na kuwarudisha pia.
Hapa ndipo suala la gharama za usafiri linapoibuka, nauli kwa mtu mzima ni sh 100 kwenda na kurudi huku wanafunzi wakilipa sh 200 kwa mwezi.
Pamoja na gharama hizo za kuvuka kutoka ng’ambo moja ya kijiji cha Nyaminywiri ambazo wengi wataziona kuwa ni nafuu ukilinganisha na maeneo mengine, wapo baadhi ya wakazi ambao wamekuwa hawalipi nauli ya usafiri huo hali inayowapa wakati mgumu, waendesha mitumbwi ambao hutegemea kipato chao kuvusha abiria katika kivuko hicho.
Dereva wa mtumbwi (Mikoloti) akiwavusha wakazi toka ng'ambo nyingine ya kijiji cha Nyaminyiri
“Baadhi ya abiria ni wasumbufu sana inatokea mtu umemvusha kwenda na kurudi na unapomdai pesa anasema hana, inaudhi sana maana hakuna sheria inayombana asipolipa kwa hiyo tunaamua kuacha tu” anaeleza Omary Ulwe (57) mwendesha mtumbwi katika kivuko cha Nyaminywiri.
Anasema kuwa wapo baadhi ya wazazi wenye watoto ambao ni wanafunzi, wamekuwa wakichelewesha kulipa sh 200 ambayo inatakiwa kutolewa kwa kila mwezi kwa mwanafunzi anayevuka katika kivuko hicho.
Pamoja na hatari mbalimbali anazokumbana nazo katika shughuli hiyo, Ulwe anasema kazi hiyo ya kuendesha mtumbwi ni kazi anayoipenda na kuithamini.
Anasema siku ambayo mambo yanakuwa mazuri amekuwa akipata shilingi 6000 na siku ambayo mambo yanakuwa si mazuri hupata sh 2000, anasema kipato hicho ni kwa kipindi ambacho sio cha mavuno.
Ulwe anasema kipindi cha mavuno ya korosho ndicho kipindi cha neema kwa kazi yake kwani kuvusha kiroba kimoja cha korosho chenye uzito wa kg 50 ni sh 200, kama mkulima atapanga mwenyewe kwenye mtumbwi ila kama atasaidiwa na mwendesha mtumbwi kupanga, basi mkulima au muuzaji hulipa sh 300 kwa kila kiroba.
“Wakati huo kila mwendesha mtumbwi hufurahia kazi hii, maana kwa siku unaweza kuvusha viroba 100, kwa hiyo unaweza kupiga hesabu” anaeleza.
Yusuph Mikoloti (32) naye anajishughulisha na kazi ya kuendesha mtumbwi anaeleza kero ya baadhi ya abiria ambao wamekuwa wakikaidi kulipa baada ya kuvushwa.
Anasema hali hii inatokana na utaratibu uliopo, ambapo mwendeesha mtumbwi haruhusiwi kumuacha mtu hata kama jana yake hakulipa.
“Unajua huwezi kumdai abiria kabla ya safari kwa sababu inaonekana unamfedhehesha, kwa hiyo hata kama hakulipa safari iliyopita inabidi umbebe mpaka ng’ambo ndipo umdai” anaeleza Mikoloti.
Anasema wapo waendesha mitumbwi watano katika kivuko hicho cha Nyaminywiri, ambao hufanya kazi kwa zamu ya siku saba na yeye anapokuwa hayuko kazini ndipo hujishughulisha shughuli za kilimo.
Lakini anakiri kuwa pamoja na matatizo yaliyopo katika kazi hiyo, anasema kazi hiyo inamlipa.
Anasema shughuli za biashara, zinapokuwa nyingi ndipo wanapoingiza kipato kikubwa.
Mikoloti anaeleza kwamba shughuli zinapokuwa nyingi ndicho kipindi cha neema kwa waendesha mitumbwi katika kivuko hicho.
Anasema wapo baadhi ya abiria wanaokuja ng’ambo kwa baiskeli, na kila baiskeli moja inavushwa kwa sh 200 wakati pikipiki inavushwa kwa kwa sh 2000.
Mikoloti anaeleza kuwa kwa siku wanavusha baiskeli zaidi ya kumi huku pikipiki zikivuka 3 kwa wiki.
Waendesha mitumbwi hao wanazungumzia nyakati mbaya wanazokabiliana nazo ikiwa ni pamoja na kupambana na wanyama aina ya viboko na mamba.
Wanasema kiboko anapokuwa amezaa basi huzunguka zunguka majini kuona kama kuna mtu au kitu chochote kinachoweza kuhatarisha maisha ya mtoto wake, ndipo anapokutana na mtumbwi huhisi ni adui.
“Mara kibao tunapishana nao na tukiona wanataka kuleta fujo basi tunapigapiga maji ili kuwachanganya na hatimaye tunafanikiwa kupita” anaeleza Ulwe.
Ulwe anaeleza kwamba mwaka 2010 kiboko alipindua mtumbwi uliokuwa umebeba wanafunzi hali iliyosababisha wanafunzi 9 kufa kwenye kwenye kivuko hicho.
Pamoja na viboko na mamba katika mto huo Mikoloti anasema wakati mwingine mbaya kwao ni kipindi cha masika kwani maji huongezeka na kuifanya kazi ya kuvusha kuwa ngumu.