Iringa: Bei hafifu za nyanya zaendelea kuwatia umaskini wakulima

Jamii Africa

LICHA ya kuwepo kwa viwanda vitatu vya kusindika bidhaa zitokanazo na zao la nyanya mkoani Iringa, wakulima wa mkoa huo bado wanaendelea kutaabika na uhaba wa soko hali inayozidi kuwatia umaskini.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonesha kwamba, uhaba wa soko umefanya bei ya zao hilo iporomoke hatua inayowafanya wakulima wapate hasara katika kilimo cha nyanya, huku wengine wakikata tamaa.

Bei ya tenga moja la nyanya lenye ujazo wa ndoo tatu za lita 20 wakati mwingine hushuka hadi Sh. 2,000 shambani, kiasi ambacho hakikidhi wala kukaribia gharama za uzalishaji wa zao hilo.

Wakulima wa nyanya wa vijiji vya Iyayi na Image wakiwa katika soko lisilo rasmi kuuza nyanya zao. Wengi wanalalamika kwamba hawanufaiki na zao hilo kutokana na kukosa masoko, hivyo kuuza kwa hasara licha ya kutumia gharama kubwa.

“Ni hasara tupu, mtu unatumia Shs. 1 milioni kwa ekari moja, lakini ukiuza unaweza kuambulia Sh. 500,000,” analalamika Benson Mwakatundu, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Image wilayani Kilolo.

Katika Kijiji cha Tanangozi wilayani Iringa, wakulima wanalalamika kwamba licha ya kuwepo kwa viwanda viwili mkoani humo vya kusindika mazao ya nyanya, bado wameendelea kukandamizwa badala ya kupata unafuu huku bei ikishuka kuliko matarajio.

Gaston Kikoti ameiambia FikraPevu kwamba, wakulima wengi wanafikiria kuachana na zao la nyanya kwa kuwa linawatia hasara huku baadhi yao wakishindwa kulipa mikopo waliyochukua katika taasisi za fedha.

“Tulitegemea kujengwa kwa viwanda kungetuokoa, lakini hali iko tofauti kabisa, bei inashushwa na wenye viwanda na masoko yameendelea kuwa changamoto,” anasema.

Aidha, ameeleza kwamba, wamiliki wa viwanda hivyo waliwahamasisha wakulima kulima nyanya kwa wingi, lakini badala ya faida wamejikuta soko la nyanya likiporomoka na kuwatia hasara kubwa kulinganisha na mikoa mingine nchini.

"Walituhamasisha tulime nyanya kwa wingi, wakulima tukaitikia kwa kujua tumekombolewa, lakini sasa hawanunui nyanya kama walivyoahidi,” alisema Kikoti.

FikraPevu imeelezwa kwamba, bei ya nyanya inayouzwa kiwandani kwa sasa ni Shs. 170 tu kwa kilo moja, fedha ambayo inaelezwa kuwa ni ndogo kwani mtaani wakati mwingine tenga la debe tatu huuzwa kati ya Shs. 7,000 na 10,000.

Viwanda vitatu

FikraPevu inafahamu kwamba, Katika Manispaa ya Iringa kuna viwanda vitatu vya kusindika mazao yatokanayo na nyanya, matunda na mbogamboga ambavyo ni Dabaga Vegetable & Fruit Canning Co. Ltd, Ivori na Darsh Industries Limited watengenezaji wa bidhaa za Redgold, lakini pamoja na uwepo wa viwanda hivyo, bado changamoto ya uhakika wa masoko haijatatuliwa.

Kiwanda cha Dabaga cha mjini Iringa.

Kwa miaka mingi, viwanda vya Dabaga na Ivori vilivyoko katika eneo la Ipogolo ndivyo pekee vilivyokuwa vikijitahidi kununua mazao ya matunda zikiwemo nyanya katika mkoa huo, lakini uwezo wake ulionekana kuwa mdogo kuliko uzalishaji wa zao hilo.

Hata hivyo, mwaka 2014, kampuni ya Darsh Industries Limited iliamua kujenga kiwanda kikubwa cha kusindika bidhaa za mbogamboga katika Kijiji cha Ugwachanya, Kata ya Mseke, takriban kilometa 12 kutoka Iringa mjini.

FikraPevu ilielezwa kwamba, mahitaji ya kiwanda hicho yalikuwa tani 200 (kilogramu 200,000) za nyanya kwa siku, sawa na kreti 4,500 au magari 20 aina ya Fuso yenye uwezo wa kubeba tani 10 kila moja.

“Tunahitaji tani 200 kwa siku, ndio uwezo wa kiwanda, na tunawahakikishia wakulima kwamba soko la uhakika litapatikana wala wasiwe na hofu,” alisema Pratap, mmoja wa maofisa.

Wakati kiwanda hicho kinajengwa, ofisa huyo aliwahi kukaririwa akisema, kiwanda kingenunua nyanya za madaraja yote bila kubagua, hivyo kusengekuwa na ‘masalo’ yatakayomwagwa na kwamba wakulima wawe na imani ya kupata tija kutokana na kilimo hicho.

Bidhaa za zitokanazo na nyanya.

Aliongeza kusema kwamba, wangepeleka makreti ya kubebea nyanya kwenye vituo vyote vya kukusanyia zao hilo ambavyo vitateuliwa na kwamba wakulima hawatagharamia usafiri wa kupeleka kiwandani.

“Wakulima kazi yao itakuwa kupeleka nyanya kwenye vituo ambako tutakuwa tumepeleka makreti ya kubebea, usafiri utakuwa ni juu ya kiwanda,” alifafanua.

Aidha, alisema kwamba, pamoja na kununua nyanya kwa wakulima, ambayo ni malighafi ya kiwanda hicho, lakini uongozi ungetoa huduma za ugani kwa wakulima ukishirikiana na Mradi wa Tanzania Agricultural Productivity (TAPP) pamoja na maofisa ugani wa vijiji na kata husika linakolimwa zao hilo.

Pratap aliwataka wakulima kuongeza uzalishaji wa nyanya ili kukidhi mahitaji ya kiwanda pamoja na kujiongezea kipato.

Nyanya, ambalo ndilo zao kuu la biashara mkoani Iringa ukiacha mbao zinazotokana na kilimo cha ambacho ni cha muda mrefu, limekuwa na changamoto kubwa ya masoko, hali inayowafanya wakulima wengi kukata tamaa.

FikraPevu inafahamu kwamba, katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2013, Tarafa ya Mazombe wilayani Kilolo, inayoundwa na Kata za Ilula, Image, Irole, Uhambingeto, Nyalumbu, Lugalo, Mlafu na Ibumu, ilizalisha zaidi ya tani 10,000 za nyanya.

Aidha, kwa msimu wa 2011/2012, jumla ya hekta 6,817 za zao la nyanya zililimwa kwa umwagiliaji mkoani Iringa na tani 115,514 zilivunwa.

Hata hivyo, kasi ya kutatua changamoto ya masoko imekuwa ya kusuasua ingawa kumekuwepo na ujenzi wa masoko madogo vijijini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kama mashirika ya Techno Save (ambalo sasa halipo mkoani Iringa), Muvi na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).

Kila sehemu vilio

FikraPevu inafahamu kwamba, wakulima wa zao la nyanya katika maeneo mengi nchini Tanzania wana changamoto kubwa ya masoko, hali inayowafanya wauze kwa hasara na hivyo kuendelea kutopea katika dimbwi la umaskini.

Katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wakulima wanalalamika kupata hasara kutokana na zao hilo kukosa soko na kupungua bei kutoka Sh. 20,000 hadi 2,000 kwa ndoo ya lita ishirini.

“Hivi sasa ndoo moja ya nyanya imeshuka kutoka Sh. 20,000 hadi 2,000, haijawahi kutokea na imetukatisha tamaa kuendelea na kilimo ambacho hakina tija,” alisema Mwenyekiti wa Wakulima wa Nyanya wa Kijiji cha Makuyu wilayani humo, Mbaruk Seleman.

Kufuatia mkwamo huo, wakulima wa Kijiji cha Makuyu, wameiomba serikali kuwajengea viwanda vya kusindika nyanya ili waweze kuziongeza thamani na kujikwamua kiuchumi.

Mbaruk Selemani alisema ujenzi huo wa viwanda utawahakikishia soko na usindikaji, ajira na biashara kwa kuuzwa katika maeneo ambayo hayana uzalishaji.

“Hata wamiliki wa viwanda vidogo vidogo vya kusindika nyanya waliokuwa wananunua zao hilo kwetu wameshindwa kununua kutokana na wengi kuwa na mashamba makubwa ya nyanya,” alisema.

Mkulima mwingine, Josephine Mateke, alisema nyanya zinaozea shambani kutokana na kukosa soko la ndani na hata uwezekano wa kutafuta soko la nje haupo hivyo hushindwa kurudisha gharama walizotumia wakati wa maandalizi na uzalishaji.

Aidha, katika Kijiji cha Mbigiri wilayani Kilosa, wakulima wanalalamika kwamba wakati wa msimu bei ya ndoo moja ya lita 20 imekuwa ikiuzwa kwa Sh. 700 tu badala ya Sh. 5,000.

Katika Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, wakulima wa nyanya wamekuwa wakilalamika kukosa soko la uhakika la zao hilo na hivyo kujikuta wakipata hasara kila mwaka.

Inaelezwa kwamba, wakati mwingine tenga la nyanya lenye uzito wa kilogramu 50 huuzwa kwa Shs. 2,500 tu badala ya Shs. 20,000, jambo ambalo linawaumiza wengi.

Ujenzi wa viwanda

Serikali ya awamu ya tano imeazimia kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuhimiza ujenzi wa viwanda katika maeneo mengi nchini kama njia ya kuwakomboa wakulima na kuongeza pato la taifa.

FikraPevu inatambua kwamba, kuzalisha bidhaa kwa kuyasindika moja kwa moja mazao yanayozalishwa nchini kutatoa fursa pia ya kusafirisha bidhaa hizo nje ya nchi na kuongeza fedha za kigeni.

Wakati wa mojawapo ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano mwaka 2015, Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul, alihoji ni kwa nini mpaka sasa serikali haijatoa ufumbuzi wa masoko ya mazao kama nyanya, mbaazi, mahindi na mazao mengine licha ya serikali kuahidi kutafuta masoko nje ya nchi na kwa nini serikali haitoi fedha moja kwa moja kuwawezesha watu binafsi waanzishe viwanda.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, alikijibu maswali hayo, alisema hivi sasa serikali inajenga viwanda kwa lengo la kuongeza thamani na kupunguza uharibifu wa mazao (post-harvest loss).

“Jambo la kufanya Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote na Watanzania nendeni SIDO, na nimekuwa nikilisema, kusudi waweze kutambua na Naibu Waziri wa Ajira alizungumza hapa, kuna kitu kinaitwa ODOP (One District One Product) inalenga kuangalia katika eneo lenu tatizo ni nini, fursa ni ipi,” alisema.

Alisema, Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, ilikuwa inawasiliana na Serikali ya India ili waweke makubaliano ya moja kwa moja kuuza mazao hayo ya mbaazi kwa kushirikiana na Serikali ya India.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *