"Ilikuwa saa tatu asubuhi Mwajuma Ramadhani alianza kupata joto kali mwilini, mama yake Mwajuma akaenda duka la dawa kununua panadol akampa panadol joto likapungua baada ya saa moja, mtoto akawa anacheza vizuri alijua amepona,"alisema Winifrida Chales Mama yake Mwajuma.
Alipoona anacheza vema aliendelea na kazi zake za kila siku za nyumbani, ilipofika saa nane alimpatia tena kijiko kimoja ch panadol na usiku alimuongeza tena dawa hiyo.
Kesho yake kulipokucha waliamka akiwa hana joto kali kama alilokuwa nalo jana, ila alikuwa hatamani kula kila akimpa chakula Mwajuma alikuwa anakataa, nilijitahidi kumlisha lakini alikaata.
Baada ya saa tano mtoto alibadilika na kuanza kuishiwa nguvu huku akiwa anahema bila ya mpangilio, niliacha kazi ya kuvuna mahindi shambani na kumbeba mtoto wake mgongoni hadi kwa shemeji yake Malosi Samsoni.
Alipofika alimkuta shemeji yake anatengeneza mahindi ili wapeleke mashine ya kusaga unga, sikuweza kumsaliamia maana alikuwa amechanganyikiwa alichofanya ni kumtelesha mtoto na kumpatia mikono mwake, alishangaa kuona hali ya mtoto wake kuwa mbaya kiasi hicho.
Shemeji yake aliuzali, ameanza kuumwa lini? mbona amelegea sana kiasi hiki? ulimpatia panadol kweli? mbona umemchelewesha kumpeleka hospitali? tunafanyaje sasa na mtoto hali kama hii? mumeo yuko wapi mpaka sasa?
"Sikuwa na majibu ya maswali yote hayo aliyoku ananiuliza shemeji yangu maana nilikuwa nimechanganyikiwa sana, nilichoona cha msingi ni kumwambia anilete hospitali,"alisema Winifrida.
Winifrida Chales anaujauzito wa miezi mitano, anaishi katika kijiji cha Bitaraguru katika kata ya Kabasa wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara, ni kilometa 6 kufika kituo cha afya cha Manyamanyama.
Winifrida na shemeji yake walipanda pikipiki moja mpaka katika kituo cha afya cha manyamanya, walishuka na kuingia mapokezi akatoa daftari la mtoto ili liandikishwe akamuone dokta.
Msimu Michel ni Daktari wa zamu katika kituo cha afya Manyamanyama, alimpokea mama na mtoto huyo na kuanza kumpima kujua nini kinacho msumbua, aligundua ana malaria kali, ambayo imesababisha kupungua kwa maji na damu mwilini.
"Nimempokea mtoto huyu lakini hana damu na maji mwilini, inabidi awekewe maji chupa tatu akimaliza inabidi awekewe damu units moja na kupewa dawa ya malaria," alisema Dokta Msimu.
Dokta Msimu alisema kuwa hashangai kuona watoto wengi wanaofika hapo wakiwa katika hali mbaya kwa kuumwa malaria, kwa sababu elimu bado ni ndogo kwa jamii mbalimbali juu ya ugonjwa huo.
“Wazazi wengi wanawachelewesha watoto wakiumwa kwa kumpatia panadol au dawa za miti shamba, mpaka akimleta hapa kituo ch afya unakuta mtoto yupo katika hali mbaya na anahitaji maji na damu na upatikanaji wa maji na damu kwa Manyamanyama ni tatizo sugu, na watoto wengi hupoteza maisha,” alisema Dokta Msimu.
Dokta Msimu alitoa ushauri kwa wazazi wa Bunda, mtoto akianza kuumwa unatakiwa kumuwahisha hospitali haraka, sio kukaanaye na kumpatia panadol na dawa za mitishamba ni hatari sana kwa mtoto mdogo, umuhimu wa kumuwaisha kituo cha afya ni kupatiwa dawa za malaria kwa haraka na kupelekea mtoto kupona. Pia mtoto akiwahishwa kituo cha afya, zahanati au hospitali anapoanza kuumwa hawezi kufikia hatua ya kupungukiwa na damu na maji.
Winifrida nakwenda wodini kupata kitanda, lakini Manyamanyama hakuna dawa ya malaria, hakuna dripu, hakuna damu, inabidi aende kununua dawa duka la dawa la karibu.
Uhaba wa madawa katika kituo cha afya cha Manyamanyama, hospitali ya teule ya wilaya pamoja na zahanati 40 katika wilaya ya Bunda ni tatizo sugu, ambalo mpaka sasa linachangia vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano katika wilaya hiyo, asilimia 42 ya watoto wanaofika zahanati, kituo cha afya na hospitali wanaumwa malaria Bunda.