SHERIA ya Haki za Mtoto ya mwaka 2009, iliyotungwa na Serikali, na hatimaye kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni moja ya nyenzo muhimu katika malezi ya watoto.
Licha ya sheria hiyo kuweka bayana haki na stahili za mtoto (ambaye ni mtu yoyote mwenye umri chini ya miaka 18), kama vile kulindwa, kutunzwa, kupewa elimu, chakula na malazi, miongoni mwa haki nyingine nyingi; ukukiukwaji wa sheria hizo nao umekuwa mkubwa siku hizi kwa wazazi na walezi wa watoto, hata kupelekea wengi wao kutimka majumbani.
Ongezeko la watoto wa mitaani hapa mjini Musoma na kwingineko, linatajwa na jamii kama matokeo ya ukatili wa wazazi au walezi, uyatima, ama ukorofi tu wa watoto wenyewe, mkumbo rika, umasikini miongoni mwa jamii, kuvunjika ndoa, mimba zisizotarajiwa, ulevi wa kupindukia, ukimwi n.k.
Mmoja wa watoto niliokutana nao Mbitta Msabhi (15), anadai kuwa yeye na mdogo wake Moilo Msabhi (13), (siyo majina halisi) wakazi wa mtaa wa Kiara bondeni, mjini Musoma, walilazimika kukimbia nyumbani baada ya mama yao Mwigala Mafuru kuwatelekeza na kukimbilia visiwani.
“Mama aliniacha mimi na mdogo wangu, akakimbilia visiwani kufanya biashara, hajarudi hadi leo, hatuna chakula majirani walitufukuza tukaja huku mjini, tukawa tukila na kulala kwenye vibanda vya chakula, kwa ujira wa kuokota mkaa, kuni na kuchota maji” anasema Mbitta.
Mwingine niliyepata nafasi ya kuongea naye ni Angelina Masige (16), ambaye pia alitoroka kwao akiwa na kaka yake ambaye anadai hawajaonana tena kwa miaka mitano sasa, baada ya kupoteana mitaani tangu walipokimbia mateso kutoka kwa walezi wao.
“Baba na mama walipofariki kwa Ukimwi, alituchukua rafiki yake ambaye ni kabila moja na baba, lakini mke wake alitutesa na kutugeuza wafanyakazi wake wa ndani mpaka tukatoroka nyumbani, hapa nilipo hata sijui aliko kaka na hata shule hatusomi” anasema Angelina.
Licha ya kwamba Angelina alipaswa kuwa shuleni akiwa kidato cha pili, lakini ndoto yake ya kusoma imepeperushiwa mbali na mlezi wake huyo ambaye inasemekana kwa sasa amehamia mkoani Kigoma, huku akiwa hana mawasiliano yoyote na watoto hao kwa miaka sita sasa.
Sambamba na huyo, wapo baadhi ya watoto wa mitaani ambao wamedai kulazimika kukatisha masomo yao kinyume na matarajio, kutokana na sababu za umasikini, lakini wanasema wako tayari kuendelea na masomo ikiwa watapatikana wafadhili.
Matatizo kama hayo na mengineyo ndiyo hasa yamekuwa yakichangia tatizo hili la ongezeko la watoto waishia katika mazingira magumu, wakizurura pamoja na kwamba baadhi ya watu wameanzisha nyumba za makimbilio kwa ajili ya kutunzia jamii hiyo ya watoto.
Pamoja na kwamba zipo tuhuma mbalimbali dhidi ya baadhi ya nyumba hizo na taasisi zisizo za Kiserikali zinazojihusisha na watoto hao, lakini walau kumekuwepo na faraja kwa jamii hiyo, licha ya tuhuma za kuwageuza watoto kuwa miradi ya kujinufaisha watu binafsi.
Pamoja na utitiri huo wa mashirika na taasisi zisizo za kiserikali kujitahidi kuwapunguza watoto hao mitaani, lakini bado wanazidi kuongezeka na kuvizidia vituo hivyo, kwa idadi kubwa ya watoto inayozidi uwezo wa wafadhili na walezi kuwamudu.
Mmoja wa walezi na wamiliki wa kituo cha Jipe Moyo cha mjini hapa, Sista Margareth Michael anasema tatizo la umasikini miongoni mwa wazazi au walezi, linasababisha watoto wengi kukimbia makwao na kujisalimisha hapo.
“Awali tulifikiri ni ukatili, uyatima ama utukutu tu wa watoto wenyewe, lakini kumbe njaa na umasikini wa kutupwa pia ni tatizo linalopelekea kukuwa kwa tatizo hili…, baadhi ya watoto tumewadadisi wameonekana kuwa wana wazazi wao majumbani” anaweka bayana Sista!.
Kwa mujibu wa mmiliki huyo wa kituo cha Jipe Moyo, wamekuwa wakiwarejesha nyumbani watoto hao kila wanapobaini kuwa wana wazazi na walezi, ikiwa ni pamoja na kuwapa ushauri wazazi na walezi kuwadhibiti watoto wao licha ya ugumu wa maisha.
Shekhe Mussa Magoti akizungumzia wajibu wa wazazi na walezi kuondoa maisha magumu na maamuzi yasiyozingatia uoni wa tafakari miongoni mwa watoto, anasema kwamba jamii imesusa kuangalia sehemu yake, ambayo ni watoto katika ujumla wake.
Yeye analaumu kupungua kwa imani miongoni mwa wanadamu, anadai kwamba nyakati za zamani akifa mtu na kuacha watoto wasio na walezi, basi jamii iligawana watoto wale na kuwapa haki na stahili zote za watoto majumbani mwao, ili kuwanusuru kutorokea mitaani.
Shekh Magoti anaungwa mkono na Mzee Masatu Ndagara anayelaumu utetezi mbaya wa kigezo cha haki za binadamu na kuondolewa kwa matumizi ya kiboko katika malezi ya mtoto, hivyo kuwafanya baadhi ya watoto kufanya watakavyo.
“Soma Biblia andiko la (Mithali 22; 6, 15,) Mungu ameruhusu matumizi ya kiboko ili kumuadabisha na kumtiisha mtoto, lakini siku hizi mmevunja sheria za Mungu kwa kisingizio cha haki za binadamu, ndiyo maana watoto hawashikiki mitaani” anasema mzee Ndagara ambaye ni Msabato.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii, Manispaa ya Musoma, Buhabi Msiranga anasema tatizo la ongezeko la watoto wa mitaani limekuwa likishughulikiwa kwa njia ya kuwauliza watoto hao kuhusu wazazi, ndugu, walezi ama jamaa zao na mahala wanakoishi, kisha huwarejesha makwao na kuwachukulia hatua za kisheria wanaowatelekeza.
“Siyo kweli kuwa watoto hao wote hawana makwao wala wazazi ama walezi, wengine wanatoroka tu kwa sababu za njaa na utukutu, hivyo tumekuwa tukiwakamata na kuwarejesha makwao ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua walezi au wazazi wao” anasema Msiranga.
Pamoja na hatua hiyo anaongeza kusema kuwa zipo na jitihada nyingine nyingi zinazofanywa na serikali katika kukabiliana na tatizo hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wazazi kuhusiana na haki na malezi ya mtoto sambamba na sheria za nchi dhidi ya wanaokiuka.
Naye diwani wa kata ya Mwigobero, Mussa Kerenge anasema kuwa kujenga vituo vya kulelea watoto hao, siyo suluhisho la kumaliza wimbi la watoto wa mitaani, bali linaweza kuwatia moyo hata wengine wa majumbani kukimbilia huko.
“Sheria ziko wazi juu ya haki za mtoto na wajibu wa wazazi kwa familia, tukijenga na kuboresha vituo vya watoto ni sawa na kuwachochea wengine kutoroka majumbani, hizo chache zilizopo ziwe kwa watoto yatima pekee na waliothibitishwa tu” anasema Diwani.
Diwani huyo anaongeza kusema kuwa matatizo mengine ya watoto wa mitaani ni rahisi kushughulika nayo kwa sababu hakuna mtoto aliyeshuka toka mbinguni bali ana wazazi ama jamaa, sheria zikifuatwa kikamilifu tatizo hilo linaweza kukoma.