ZOEZI la serikali kuhamia Dodoma linaonekana kusuasua tofauti na lilivyoanza licha ya makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali kuwa katika harakati za kuhamia Dodoma kabla ya Februari 28, 2017.
Inaelezwa kwamba, kusuasua kwa zoezi hilo lilinalotokana na agizo la Rais John Magufuli kumechangiwa na mambo mengi, kubwa zaidi likitajwa ‘kukurupuka’ kwa serikali bila kuangalia bajeti zake.
Wachambuzi wa masuala ya maendeleo wanaeleza kuwa, ili zoezi hilo likamilike, serikali inahitaji kati ya Shs. 1.5 trilioni hadi Shs. 2 trilioni, fedha ambazo ni nyingi na hazijaelekezwa kwenye bajeti yoyote, ikiwemo ile ya Wizara ya Sera, Uratibu na Bunge pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango.
Badala yake, kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu wa Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama kwamba bajeti ya kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma litatatuliwa kwa kutumia posho za safari za mawaziri inaonekana ilikuwa ya kisiasa kuliko uhalisia.
“Bajeti tulizopanga, hasa ya 2016/17 sisi tunajua tulipanga nini, tunafahamu mapato yaliyopitishwa na Bunge yakoje. Kwa mfano, mimi Jenista (waziri) kwa mwaka huu mzima wa fedha nina mikutano minne Dodoma. Kwenye ile mikutano yote natakiwa kulipwa posho, maana yake ni kuwa napaswa nipate posho ya miezi mitano, sasa fedha hiyo ndiyo itakayoingizwa kwenye gharama za kuihamishia Serikali Dodoma,” alisema wakati akihojiwa nakituo cha luninga cha TBC1 Agosti 2016.
Waziri Mhagama hivi karibuni alirudia kusisitiza kwamba ni lazima wizara na idara za serikali ziwe zimehamia Dodoma ifikapo Februari 28, 2017 huku akiongeza kwamba hakuna tatizo la ofisi za watumishi.
“Hakuna tatizo la ofisi za watumishi wa wizara zote, kwani majengo yamekamilika na yapo katika hali nzuri tayari kwa ajili ya kuanza kutumiwa, hivyo wakuu husika wakiwamo mawaziri wahakikishe wanatakiwa kuhamia Dodoma,” alisema.
Lakini ratiba ya kuhamia huko iliyotangazwa Agosti 2016 na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, inakwenda kwa mwendo wa kinyonga ambapo hata hiyo awamu ya kwanza bado haijatekelezwa huku ukiwa umesalia mwezi mmoja tu.
Mbali ya makatibu na naibu makatibu wakuu, awamu hiyo ya kwanza ya inahusisha pia mawaziri wote pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu na wakuu wa idara kadhaa za kila wizara.
FikraPevu inatambua kwamba, kuhama haraka kwa wahusika katika awamu hiyo ya kwanza kutatoa fursa ya awamu nyingine kufuatia, ambapo kundi la pili linatakiwa lime limehamia Dodoma ifikapo Agosti 2017.
“Awamu ya pili itakuwa Machi 2017 na Agosti 2017 na kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka bajeti zao za mwaka 2017 na 2018 na kuendelea kuwahamisha watumishi wake kuja Dodoma. Awamu ya tatu itakuwa kati ya Septemba 2017 na Februari 2018, ambapo wizara zitaendelea na uhamishaji wa watumishi wa idara zilizo ndani ya wizara zao,” Waziri Mkuu alikaririwa akisema mara baada ya Rais John Magufuli kutakaza nia ya kuhamishia serikali mjini Dodoma haraka.
Kwa mujibu wa mpango huo wa serikali, awamu ya nne itakuwa Machi 2018 mpaka Agosti 2018, awamu ya tano ni Septemba 2018 na Februari 2020, na awamu ya sita ni Machi 2020 na Juni 2020, ambayo itahusisha Ofisi ya Rais ikiongozwa na Rais na Makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kusuasua kwa uhamiaji huo kunawafanya wananchi ‘wafurahie’ mipango ya serikali inaposhindwa licha ya ukweli kwamba walikuwa wanaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuthubutu kufanya kile ambacho kimeshindikana kwa miaka 43.
Serikali inashindwa kuweka wazi kuhusu bajeti itakayotumika kuhamishia utendaji wake Dodoma, suala ambalo ni la msingi kwa sababu bila fedha mipango yote itaendelea kuwa ya kisiasa.
Katika kipindi hiki ambacho uchumi umeonekana kulegalega, suala la bajeti ni muhimu kuzingatiwa ili ijulikane fedha zinazowahamisha watumishi zinatoka katika fungu gani.
Watawala waliomtangulia Rais Magufuli walishindwa kutekeleza suala hilo si kwa sababu hawakuwa na fedha, bali hawakuwa na dhamira.
Kwa miaka mingi iliyopita, suala la kuhamishia serikali Dodoma limechukuliwa na watawala kama mtaji wa kisiasa huku Watanzania wakiwa na shauku ya kuona utekelezaji.
Hakuna anayepinga hoja ya kuhamia Dodoma kwa sababu ni uamuzi wa muda mrefu na unaweza kuleta maendeleo, lakini kinachotia mashaka ni dhamira halisi ya utekelezaji wake ambayo safari hii imeanza kwa kasi na imezima ghafla.
Kila jambo la maendeleo lina faida na hasara zake, lakini katika kutekeleza maazimio ya serikali, mara nyingi ni vyema kuangalia faida kwa mipango endelevu kuliko kukwamishwa na changamoto.
Gharama za kuhamisha makao makuu ni kubwa kwa upande mmoja kwa sababu fedha zinatakiwa zipatikane ndani ya miaka minne iliyosalia, lakini kwa upande wa pili zinaweza kuwa ndogo kwa sababu ni za mara moja tu wala siyo kujirudiarudia.
Sote tunafahamu kuwa shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hufanyika Dodoma mara nne kila mwaka, ambapo kuna jumla ya vikao 182.
FikraPevu inatambua kwamba, katika vikao hivyo, ukiacha wabunge, kuna maofisa wengi wa serikali ambao husafiri kutoka Dares Salaam kwenda Dodoma kwa gharama za serikali.
Hawa ni mawaziri, watumishi wa wizara, wageni wa serikali, watumishi wa vyombo vingine vya serikali na kadhalika ambao wanaigharimu serikali nauli au mafuta na magari ya umma, malazi, chakula na posho mbalimbali za kuwa nje ya vituo vya kazi, achilia mbali matengenezo ya maghali kutokana na safari hizo pamoja na hatari ya usalama wa nyaraka za umma.
Ukiacha vikao hivyo vya Bunge, lakini zipo gharama nyingine za watumishi kusafiri katika miji hiyo kwa shughuli za serikali, ambazo ni gharama endelevu.
Tanzania haitakuwa ya kwanza kuhamisha makao makuu yake, kwani zipo nchi nyingi ambazo zimepata kufanya hivyo.
Tangu mwaka 1950 hadi 2000, nchi 13 zimeshabadilisha makao yao makuu ambazo ni Brazil (1956 – kutoka Rio de Janeiro kwenda Brasilia), Mauritania (1957 – kutoka Saint Louis (Senegal) kwenda Nouakchott), Pakistan (1959 – kutoka Karachi kwenda Islamabad), Botswana (1961 – kutoka Mafeking kwenda Gaborone), Libya (1963 – kutoka Benghazi kwenda Tripoli), Malawi (1965 – kutoka Zomba kwenda Lilongwe), na Belize (1970 – kutoka Belize City kwenda Belmopan).
Nyingine ni Nigeria (1975 – kutoka Lagos kwenda Abuja), Ivory Coast (1983 – kutoka Abidjan kwenda Yamoussoukro), Ujerumani (1990 – kutoka Bonn kwenda Berlin), Kazakhstan (1997 – kutoka Almaty kwenda Astana), na Malaysia (2000 – kutoka Kuala Lumpur kwenda Putrajaya).
Kuhamisha makao makuu ni moja ya njia sahihi za ujenzi wa dola na utambulisho wa kitaifa, lakini kutokana na mchakato wake kuwa mkubwa, viongozi wengi huhofia kuchukua hatua kutokana na gharama kubwa za kifedha, kijamii, na hata kisiasa.
Mara nyingi miji mipya mikuu hushindwa kustawi kwa sababu hulazimu serikali kutumia gharama kubwa zaidi kuhamisha serikali yote na idara zake.
FikraPevu inaamini kwamba uamuzi wa serikali ni mzuri, lakini hata katika suala la bajeti inawezekana unakwamishwa na baadhi ya watendaji ambao wanaona dhahiri hakutakuwa na ‘upigaji dili’ ndefu za posho kama ilivyokuwa awali.
Tangu wazo la kuhamisha makao makuu kwenda Dodoma lilipokuja mwaka 1973 baada ya vikao kadhaa vya chama tawala cha wakati huo Tanzania Bara – Tanganyika African National Union (TANU) – idara karibu zote za serikali zimeshindwa kutekeleza uamuzi huo ambao baadaye ulitungiwa Sheria iliyounda Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA).
Visingizio visivyo na kichwa wala miguu ndivyo vilivyotawala na kukwamisha zoezi hilo ambalo siyo la kisiasa.
Wapo wanaosingizia kwamba mji wa Dodoma hauna miundombinu mizuri, lakini ni hao hao ambao kila mwaka huketi Bungeni kupitisha Bajeti kwa ajili ya CDA kuendeleza mji huo.
Barabara zimejengwa, ingawa siyo kwa wingi, lakini hakuna anayeweza kusingizia kwamba amechelewa kwa ajili ya foleni, maana atakuwa muongo.
Viwanja vimepimwa vya kutosha, maeneo ya umma yametengwa, lakini badala ya wakubwa hao kuhamia huko wengi wananunua viwanja vyao binafsi na kuendelea kuipuuza sheria inaiyowataka wahamishie serikali Dodoma.
Miundombinu mingi imeboreshwa katika mji huo na huduma za kijamii zinapatikana kwa urahisi tofauti na miaka 20 iliyopita kabla hata Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halijahamishia vikao vyake huko mwaka 1996 kutoka kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Wizara chache zina ofisi mbili; moja mjini Dodoma (‘makao makuu jina tu’) na Dar es Salaam. Wizara hizi ni Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi; Sera, Uratibu na Bunge), Wizara ya Fedha na Uchumi; Wizara ya Nishati na Madini; Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; Wizara ya Mipango; na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Mawaziri karibu wote wana nyumba zao (Rest House) kule Area D na nyingine Kilimani, sijui kisingizio ni nini?
Maswali mengi ya msingi yanaendelea kujitokeza kuhusu dhamira halisi ya serikali kuhamia huko wakati tayari ilikwishatangaza kujenga nyumba 80 za wizara kadhaa jijini Dar es Salaam.
Mtu angeweza kufikiri kwamba, lingekuwa ni wazo jema kwa serikali kujenga nyumba hizo 80 mjini Dodoma kama kuonyesha nia yake ya kuhamishia serikali huko.
Kila mwaka wa fedha, Serikali kupitia Wizara ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa hutenga mamilioni ya fedha za walipa kodi kwenye bajeti kwa ajili ya CDA.
Aliyekuwa Waziri wa Nchini katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Phillip Marmo, alisema mwaka 2008 kwamba serikali ilikuwa imetenga Shs. 2.4 bilioni kwa ajili ya uendelezaji makao makuu kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2008/09, kulinganisha na Shs. 400 milioni za bajeti ya mwaka 2005/06. Fedha hizo, alisema, zingetumiwa na CDA kwa ajili ya upimaji wa viwanja 10,000 huko Nzuguni, Mnadani na Mkalama na tayari vimekwishapimwa.
Mara nyingi fedha hizi hufujwa na maofisa wasio waadilifu na pengine ndiyo maana wamekuwa wakikwepa suala la kuhamia Dodoma kwa kuwa hawawezi kuzipata tena, jambo ambalo wakati fulani limewafanya wakurugenzi wa CDA kuachia ngazi kutokana na ubadhilifu.
Watanzania wanaamini uamuzi huo siyo mbaya, lakini ni vyema serikali ikaweka wazi bajeti hiyo inatoka fungu gani, maana yawezekana likawa ni agizo la kisiasa kama yalivyotokea maagizo mengine miaka iliyopita.