SEHEMU mbalimbali duniani wanawake wanatarajiwa kuishi umri mkubwa ikilinganishwa na wanaume. Kimsingi, watu wengi wana bibi zao kuliko babu zao.
Kwanini iko hivi na ni nini husababisha? Kulingana na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Southern California nchini Marekani, watafiti wa masuala ya jamii, saikolojia na utambuzi kuhusu kuzeeka wanadai tofauti za umri wa kuishi kati ya jinsia hizi zilianza mwanzoni mwa karne ya 20.
Mapinduzi ya viwanda katika nchi zilizoendelea, hasa za Ulaya na Amerika yalipelekea kuwepo kwa njia bora za kuzuia magonjwa, lishe bora na tabia nzuri ya kulinda afya ambapo katika miaka ya 1800 na mwanzoni mwa 1900 yalichangia kupungua kwa vifo, wakati huo huo jinsia ya kike kuongeza umri wa kuishi kwa kasi kubwa.
Katika miaka ya sasa, kumekuwa na upungufu mkubwa wa vifo uliotawanyika, mapitio ya takwimu za dunia yanaonyesha kwamba magonjwa ya moyo kwa watu wazima ndiyo chanzo kikuu cha vifo kwa wanaume kulingana na maprofesa kutoka Chuo Kikuu cha Southern California na AARP.
“Tunashangazwa na tofauti kubwa ya vifo kati ya wanaume na wanawake iliyoanza mwanzoni mwa miaka ya 1870,” maprofesa hao walisema.
Utafiti huo ulifanywa na William F. Kieschnick, Profesa wa Chuo Kikuu cha Southern California katika masuala ya baiolojia ya kuzeeka na Hiram Beltrán-Sánchez, mtafiti wa Kituo cha Demografia ya Afya na Kuzeeka wa Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Utafiti huo ulihusisha watu walioishi kati ya miaka ya 1800 na 1935 katika nchi 13 zilizoendelea.
Maprofesa hao walichunguza vifo vya watu wazima kuanzia miaka 40, ambapo timu hiyo ya watafiti iligundua watu waliozaliwa baada ya 1880, kiwango cha vifo vya wanawake kilipungua kwa asilimia 70 haraka zaidi ya wanaume.
Hata baada ya kudhibiti vifo vinavyotokana na uvutaji sigara, bado magonjwa ya moyo yalionekana kuwa sababu kubwa ya vifo vya wanaume wenye zaidi ya miaka 40. Inashangaza uvutaji wa sigara ulichangia asilimia 30 ya tofauti ya vifo kati ya jinsia hizo baada ya 1890.
Athari isiyolingana ya vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo kwa wanaume hasa kipindi cha kati na mwanzoni mwa uzee, inaibua swali je, wanaume na wanawake wanapatwa na hatari za magonjwa ya moyo kwa namna tofauti? Je, ni kutokana na kurithi au mambo mengine yanayowalinda katika maisha yao?
Watafiti hao walisema, tafiti zijazo zitajumuisha uchambuzi wa vyakula na tofauti ya mazoezi katika nchi mbalimbali, uchunguzi wa kina wa chembe za urithi kati ya jinsia zote pamoja na uhusiano wa matokeo hayo kwenye afya ya ubongo katika umri mkubwa ili kujua nini hasa kinawafanya wanawake waishi maisha marefu zaidi ya wanaume.