Lumuma: Mto unaobeba matumaini ya vijiji saba

Kulwa Magwa

UWEPO wa mto Lumuma katika kata hiyo, umesaidia uchumi wa wakazi wa vijiji saba vya wilaya za Kilosa na Mpwapwa wanaoutumia kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

Kutokana na umuhimu huo, maisha ya kiuchumi ya wakazi wa vijiji vya Msowelo, Lufusi, Lumuma, Kidete, Mafene, Nkhumbulu na Kitati yanautegemea kwa shughuli zao.

Mwenyekiti wa Chama Cha Ushirika wa Umwagiliaji Lumuma (CHAULU) ambacho kinaratibu shughuli za mto huo, Joklan Cheliga, anasema wamekuwa wakiutumia mto huo kumwagilia maji kwenye mashamba yaliyopo kando ya bonde hilo.

shamba-lumuma

Kilimo cha mpunga kinachofanyika katika bonde la mto Lumuma, wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma

Cheliga anasema kilimo kinachofanyika katika mashamba hayo yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 800 kinahusisha mazao ya mpunga, mahindi, maharage na vitunguu ambayo huyalima kwa kubadilisha, kwa mwaka mzima.

Anasema, ubadilishaji huo wa mazao huwafanya wakazi wa sehemu hiyo kuwa ‘bize’ muda wote wa mwaka, bila kujali kwamba kuna nyakati za mvua.

“Kwa ujumla sisi mvua ije – isije tutalima maana maji huwa hayakauki, isipokuwa kuna nyakati hupungua na hapo ndipo mvua tunapozihitaji zituongezee maji, “anasema mwenyekiti huyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Lumuma.

Cheliga anasema kwamba wanachama wa CHAULU waliamua kuunda umoja huo ili uwasaidie kudhibitiana, kupanga mikakati ya utunzaji na uhifadhi wa mto pamoja na kusaidiana katika maisha yao.

Katika kuhakikisha kuwa shughuli za kilimo zinafanyika vizuri, serikali kupitia Wizara ya Maji, iliwatengenezea mabanio matano ambayo ndiyo hutumika kusafirishia hadi mashambani.

Baadhi ya wakulima wanaonufaika na mto huo wanalalamikia uharibifu uliofanywa na kampuni JTL Mining, iliyokuwa inafanya utafiti wa shaba katika mlima Kitaugimbi na msitu wa Ipondelo, ambayo imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Walisema, kampuni hiyo imeacha udongo mwingi bila kuusambaza ambao wana hofu kubwa ya kuporomokea katika mito midogo inayosafirisha maji kwenda ulipo mto Lumuma.

“Hofu ya udongo ule kupomokea katika mto huu na kusababisha uzibe ni kubwa, hasa mvua itakapochanganya kunyesha – hapo ndipo tunapoomba serikali itusaidie kuwashurutisha waje warekebishe, “ anasema Mariam Japhet.

Naye Eliza Itonange, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nkhumbulu, anasema mto huo umemfanya aweze kuendesha maisha yake vizuri pamoja na kusomesha watoto wake katika shule za kulipia.

Mwanamke huyo ambaye ni mjane, anasema kilimo cha mpunga na vitunguu kimemfanya asomeshe watoto wake wawili wa kike katika sekondari na watatu wanaosoma katika shule ya msingi zilizopo mjini Morogoro.

Mwenyekiti wa kijiji cha Lufusi, Beatus Sendwa, anasema mto Lumuma umewasaidia wananchi kutekeleza malengo yao mengi, licha ya kwamba hali zao za kiuchumi bado ziko chini.

“Hapa kila mtu anajituma katika kazi ya kilimo na mafanikio yanaonekana, “anasema Sendwa.

Naye Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye, anasema serikali inafuatilia kwa karibu shughuli mbalimbali za kilimo zinazofanyika katika na kandokando ya mto huo.

Kangoye anasema kwamba, wakati mwingine umasikini wa wakazi wanaozunguka mto huo ni wa kujitakia, ikizingatiwa kwamba wana nafasi kubwa ya kunufaika na mto huo usiokauka.

“Hatutachoka kuwahamasisha wananchi kulima na kuulinda mto huo kwa manufaa yao, lakini vilevile ya vizazi vijavyo. Binafsi nitakuwa mkali sana kwa wale watakaoharibu mto huo, maana maisha ya watu wengi sehemu hiyo yanategemea uwepo,” anasema mkuu huyo wa wilaya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *