Mafia: Wagonjwa wengi wanapona kwa miujiza. Hakuna dawa

Jamii Africa

BAJETI finyu inayotengwa kwa ajili ya sekta ya afya nchini, inachangia kukosekana dawa na vifaa vya tiba katika zahanati na hospitali za umma wilayani Mafia, Pwani.

Halmashauri ya Wilaya ya Mafia inahitaji zaidi ya Sh. milioni 300 kwa mwaka, kwa ajili ya dawa na vifaa vya tiba, lakini inayopatikana ni milioni 196 au chini ya hapo.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa ufinyu wa bajeti unasababisha zahanati na hospitali ya wilaya hiyo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa na vifaa vya tiba, hivyo kusababisha wananchi kwenda kununua katika maduka binafsi.

Baadhi ya dawa zinazokosekana mno ni Ampicilin, PenV, Ethromycine na vifaa vya tiba ni pamoja na reagents za kupimia wingi wa damu, hivyo  wananchi huenda kupima katika zahanati binafsi.

Wasubiri muujiza

Aisha Fakhi, mkazi wa Kijiji cha Teleni anasema tatizo la ukosefu wa dawa katika vituo vya umma limekuwa sugu na wanapokosa fedha za kununua dawa, hubaki nyumbani bila kupata tiba.

Baadhi ya magonjwa yanayowasumbua wananchi wa Mafia ni kuhara, magonjwa ya njia ya hewa, malaria, shinikizo la damu na majeraha yatokanayo na wanyama au wadudu.

Hospitali ya Wilaya ya Mafia

“Ukienda zahanati iliyopo kijijini hakuna dawa, ukienda hospitali ya wilaya, ukiwa na bahati utafanyiwa vipimo na kuambiwa dawa hakuna, unaandikiwa cheti ukanunue, kama huna pesa, basi unasubiri muujiza wa Mungu kama kupona au kufa,” anasema Fakhi anayeungwa mkono na mwananchi mwingine Sharifa Abdu, mkazi wa Bondeni.

Mwarabu Mussa, mkazi wa Kirongwe anaieleza FikraPevu kwamba haipendezi mwananchi kwenda vituo vya tiba vya umma na kukosa dawa, kwani wanaathirika kisaikolojia hasa ambao hawana fedha ya kununua dawa.

Anasema hospitali ya wilaya ni tegemeo la wananchi wanapokosa huduma kwenye zahanati katika kisiwa hicho kinachofikika kwa usafiri wa ndege na maji na kwamba inapaswa kuwa na dawa na vifaa vya tiba vya kutosha.

Hata hivyo, FikraPevu imebaini kuwa usafiri wa maji unaotumiwa na asilimia 99 ya wananchi hauna uhakika kwa siku, kuna boti moja inayotoka Mafia kwenda Nyamisati wilayani Kibiti, mahali panapounganisha kisiwa hicho na maeneo mengine.

Endapo mgonjwa atazidiwa na kuhitaji rufaa kusafirishwa haraka ni vigumu, kwani hakuna ndege maalum ya kubeba wagonjwa (Air Ambulance) na usafiri wa maji uliopo hauna uhakika.

“Tunahitaji maboresho katika zahanati na hospitali ya wilaya iwe na dawa, vifaa vya tiba kama X-Ray ya uhakika ili mtu apate tiba sahihi,” anaeleza Mussa akiomba FikraPevu kufikisha kilio chao kwa serikali.

Bajeti Kiduchu

Mafia ambacho ni kisiwa, ni moja ya wilaya zinazounda Mkoa wa Pwani ina kata nane, tarafa mbili watu 46,438 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Huduma za afya zinatolewa katika zahanati 16 na hospitali moja ya wilaya.

Katika mwaka wa fedha wa 2016/17 ilitengewa Sh. milioni 109 kutoka Mfuko wa Pamoja wa Fedha za Afya (Health sector basket fund).

Dkt. Omari Kambangwa, Katibu wa Afya Wilaya ya Mafia

Katibu wa Afya Wilaya ya Mafia, Dkt. Omari Kambangwa ameiambia FikraPevu kwamba kati ya fedha hizo Sh. milioni 35, sawa na asilimia 33, zimetengwa kwa ajili ya kununua dawa, hospitali ya wilaya imetengewa Sh. milioni 20. Zahanati zote hupewa shilingi milioni kumi na tano.

“Kwa mgawanyo huo, hospitali ya wilaya inapata milioni 5.2 kwa robo mwaka, wakati zahanati kila moja inapata wastani wa shilingi 200, 000 kwa robo mwaka. Fedha hazitoshi, kwani hospitali kila mwezi inahitaji shilingi milioni 27. Kwa robo mwaka inahitaji karibu milioni 70,” Dkt. Kambangwa anaieleza FikraPevu.

Anaongeza kuwa, “Makusanyo ya ndani na vyanzo vingine kwa ajili ya dawa, vifaa tiba ni shilingi milioni 196 kwa mwaka. Hivyo tuna tatizo kubwa la fedha kwa ajili ya dawa na vifaa tiba na hadi kufikia Novemba mwaka 2016 wilaya inadaiwa na MSD shilingi milioni 145 kutokana na malimbikizo ya fedha za kununua dawa”.

Dkt. Kambangwa ana taja vyanzo vingine vya fedha za kununua dawa, vifaa tiba ni Serikali kuu fedha ambazo hupelekwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Kwa mwaka wa fedha 2016/17 wametengewa milioni 52.8 kwa ajili ya zahanati na hospitali ya wilaya, fedha ambazo hazijapelekwa tangu mwezi Aprili 2016.

Mwajuma Hassani, Mratibu wa CHF Wilaya ya Mafia

FikraPevu inatambua kuwepo kwa vyanzo vingine ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), gharama ya uchangiaji matibabu na Mfuko wa Mzunguko wa Dawa (Drug Revolving Fund).

Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17 uchangiaji matibabu uliingiza milioni 22.8, NHIF milioni moja, CHF milioni nne na robo ya pili uchangiaji matibabu uliingiza milioni 12.5, NHIF milioni 8.8, mfuko wa mzunguko wa dawa milioni 2.9 na CHF milioni 3.2.  

Ipandishwe hadhi

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Dkt. Joseph Mziba anasema kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya afya wilayani humo ikiwemo ukosefu wa dawa na vifaa tiba, kuna haja kwa serikali kuipa kipaumbele cha pekee.

Anaieleza FikraPevu kuwa, hospitali ya wilaya ya Mafia isitazamwe kama hospitali nyingine ya wilaya. Kutokana na jiografia yake na tatizo kubwa la usafiri, kuiacha kuwa hospitali ya kawaida, ni sawa na kujifunga katika utoaji wa huduma.

Badala yake Dkt. Mziba anashauri serikali kuipandisha hadhi kuwa hospitali maalum na kuhakikisha vifaa vya tiba, dawa na wataalamu wanakuwepo wa kutosha.

“Tukiiangalia hospitali ya wilaya ya Mafia kama zilivyo hospitali nyingine za wilaya, tutakuwa tunajifunga katika kufikiri kwetu, kwa jiografia yetu, hakuna uwezekano wa haraka kumsafirisha mgonjwa kwenda maeneo mengine kupata tiba, hivyo ipandishwe hadhi iwe hospitali maalum yenye vifaa vya kutosha,” anaieleza FikraPevu.

Anafafanua kuwa, “Kama itakuwa na vifaa na dawa za kutosha ni rahisi hata kuomba wataalamu kutoka sehemu nyingine iwapo kuna dharura”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *