Magufuli: Watanzania kusafiri kwa Bajaj kutoka Kigoma hadi Dar

Daniel Mbega
KIGOMA: Rais Magufuli azindua Barabara ya Kibondo mpaka Nyakanzi yenye urefu wa KM 50. Amesema hatowavumilia wakandarasi wazembe. Rais amesema kuanzia tarehe 1 Mwezi wa 7,2017 ukibeba mazao hutatozwa ushuru si kwa gunia tu ila hadi tani 1 ya gari. Kwenye kilimo Serikali imefuta tozo 80, pia kwenye mifugo kodi 7 zimefutwa, kulikuwa na kodi hadi ya kwato #JFLeo

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, amesema anataka kuona Watanzania wakisafiri kwa Bajaj kutoka Kigoma hadi Dar es Salaam baada ya kuimarishwa kwa mtandao wa barabara za lami nchini humo.

Aidha, amesisitiza kwamba, kwa kasi ya serikali ya kujenga barabara za lami, inawezekana kusafiri kwa kutumia teksi kutoka Mtwara hadi Bukoba akirejea kauli aliyowahi kuitoa Bungeni Ijumaa, Mei 10, 2013 wakati akiwa Waziri wa Ujenzi.

Rais amesema kuanzia tarehe 1 Mwezi wa 7,2017 ukibeba mazao hutatozwa ushuru si kwa gunia tu ila hadi tani 1 ya gari.
Kwenye kilimo Serikali imefuta tozo 80, pia kwenye mifugo kodi 7 zimefutwa, kulikuwa na kodi hadi ya kwato #JFLeo

“Niliwahi kuwaeleza Bungeni wakati ule kwamba inawezekana kusafiri kwa Bajaj kutoka Bujumbura hadi Dar es Salaam, tena wanaweza kusafiri kwa teksi kutoka Mtwara hadi Bukoba lakini hawakunielewa, narudia tena inawezekana kwa sababu ya mtandao wa barabara za lami kila mahali,” alisisitiza.

Dkt. Magufuli ameyasema hayo huko Kakonko, Kigoma wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Nyakanazi – Kibondo yenye urefu wa kilometa 50.

“Napenda muamini kwamba kwa barabara hizi zinazojengwa ni rahisi kabisa kusafiri kwa Bajaj, Kigoma inaunganishwa kwa lami, kule Tabora pia lami imeunganishwa, ni jambo linalowezekana,” alisema.

Barabara hiyo ndiyo pekee katika Ukanda wa Magharibi (Western Corridor) ambayo inajengwa na kampuni ya kizalendo ya Nyanza Road Works, ambapo itagharimu Shs. 45.985 bilioni.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli pia alizindua ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kidahwe – Kasulu yenye urefu wa kilometa 63, ambayo inajengwa na kampuni ya China Railways 50 Group kutoka China kwa gharama ya Shs. 41.88 bilioni.

Hata hivyo, Rais Magufuli ameitaka kampuni ya Nyanza inayoshughulikia ujenzi wa barabara ya Kibondo-Nyakanazi kuanza kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha ujenzi huo ili kuwapa fursa wakazi wa Mkoa wa Kigoma na wengineo ya kusafiri bila taabu, huku akiongeza kwamba wapo baadhi ya wananchi ambao hawajahi kuona lami maisha yao yote mpaka wanakufa.

"Wananchi hawa wanahitaji barabara ya lami wameteseka tangu dunia iumbwe, wako watu hawajui rangi ya lami, wapo watu hapa wamezaliwa,wamezeeka hawajui rangi ya lami ikoje. Kwa sababu hawajawahi kuona barabara ya lami katika maisha yao, kwa hiyo nataka hii lami ianze na mjipange kweli mfanye kazi usiku na mchana," alisema Rais Magufuli. 

Wakati Rais Magufuli akizindua barabara hiyo, tayari ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa kilometa 112 ambayo inajengwa na kampuni ya Sinohydro Corporation ya China unaendelea.

Barabara hiyo, ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2017 inagharimu jumla ya Shs. 101.113 bilioni.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo umehusisha awamu mbili za ujenzi ambapo awamu ya kwanza ni barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa 45km na barabara ya Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa 67km.

Uzinduzi wa barabara ya Kibondo-Nyakanazi ni mwendelezo wa matukio ya uzinduzi na ufunguzi wa miradi ya barabara mkoani Kigoma na Tabora ambapo Julai 19, 2017 Rais Magufuli alifungua barabara ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga yenye urefu wa kilometa 154 ambayo imejengwa kwa ubia baina ya kampuni mbili za China ambazo ni China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO) na China Railway Seventh Group.

Barabara hiyo, ambayo iligharimu Shs. 191.454 bilioni, imeweza kuunganisha Mkoa wa Kigoma na mikoa ya Kagera na Geita na kurahisisha mawasiliano ambayo awali yalikuwa ya shida.

Jumapili, Julai 23, 2017 Rais Magufuli atafungua barabara ya Kaliua – Kazilambwa yenye urefu wa kilometa 56 ambayo imejengwa na kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO) kwa gharama ya Shs. 58.563 bilioni.

FikraPevu imearifiwa pia kwamba, siku hiyo ya Julai 23, 2017 Rais Magufuli atafungua barabara ya Urambo – Ndono – Tabora yenye urefu wa jumla ya 94km, ufunguzi ambao utafanyika mjini Urambo.

“Babara hii bado kipande cha kilometa kama 30 kutoka Urambo kwenda Tabora, lakini sehemu kubwa tayari imewekwa lami,” alisema Rais Magufuli leo hii huko Kakonko.

Barabara hiyo imejengwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ya 42km kutoka Tabora hadi Ndono imejengwa na kampuni ya CHICO kwa gharama ya Shs. 51.346 bilioni, na awamu ya pili yenye urefu wa 52km kutoka Ndono hadi Urambo imejengwa na China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya Shs. 59.764 bilioni.

Taarifa zinasema, Julai 24, 2017 Rais Magufuli atafungua barabara ya Tabora – Puge – Nzega yenye urefu wa kilometa 114.9, uzinduzi ambao utafanyika Tabora mjini.

FikraPevu inafahamu kwamba, awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka Nzega-Puge (58.8km) imejengwa na kampuni ya China Communications Construction Company (CCCC) kwa gharama ya Shs. 66.358 bilioni, wakati awamu ya pili (56.1km) kutoka Puge hadi Tabora imejengwa na kampuni ya umma ya China, Sinohydro Corporation, kwa gharama ya Shs. 62.737 bilioni.

Kulingana na ratiba hiyo, kabla ya kufungua Uwanja wa Ndege wa Tabora siku hiyo ya Julai 24, 2017 Rais Magufuli atafungua barabara ya Tabora – Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 mjini Tabora ambayo imejengwa na kampuni ya China Chongqing International Construction Corporation (CICO) kwa gharama ya Shs. 93.402 bilioni.

Aidha, Julai 25, 2017 Rais Magufuli atafungua barabara ya Manyoni – Itigi – Chaya yenye urefu wa kilometa 89.3, ufunguzi utakaofanyika mjini Itigi.

Ujenzi wa barabara hiyo umefanywa na kampuni ya Sinohydro kwa gharama ya Shs. 109.643 bilioni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *