Magufuli: siwezi kukubali mwenge ufutwe

Jamii Africa
ZANZIBAR: Rais John Magufuli amesema takribani Watumishi 59,967 wataanza kuongezewa mishahara na kupandishwa madaraja kuanzia mwezi ujao. Rais akaongeza kuwa kabla ya Watumishi kudai nyongeza ya mishahara ni lazima kwanza wafahamu uwezo wa Serikali. Akaongeza kuwa hawezi kukubali Mwenge wa Uhuru ufutwe, anajua kuwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein pia hawezi kukubali Mwenge ufutwe katika kipindi chake.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amesema mwenge wa uhuru utaendelea kukimbizwa katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuchochea shughuli za maendeleo.

Rais ametoa kauli hiyo leo katika mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar katika kilele cha mbio za Mwenge 2017, Kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere na  Wiki ya Vijana, ambapo amesema serikali yake haitakubali kufuta  shughuli za kuukimbiza mwenge wa uhuru kwa sababu una manufaa kwa ustawi wa kila mtanzania.

Kauli hiyo ya rais inajibu mijadara mbalimbali ya wananchi ambao wamekuwa na maoni tofauti juu ya kufutwa na kuendelea kukimbizwa kwa Mwenge wa Uhuru. Baadhi ya watu wanasema mwenge unatumia bajeti kubwa ambayo ingeelekezwa katika maeneo mengine.

Kwa mujibu wa rais Magufuli amesema kwa mwaka huu 2017 serikali ilitenga milioni 460 kwa ajili ya mbio za mwenge ambapo umezindua miradi mingi ya maendeleo ambayo inalenga kukuza uchumi wa watanzania na kubaini ufisadi na uzembe kwa baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali nchini.

“kwa sababu mwenge sio wa kisiasa wapo watu wanaupinga na kutaka ufutwe sijui wametoka sayari gani? Mimi nawashangaa sana, mimi siwezi kukubali mwenge ufutwe. Kila mwaka tukikimbiza mwenge huu miradi mbalimbali imekuwa ikizinduliwa” amesema na kufafanua kuwa,

“Katika miaka mitano iliyopita mwenge wa uhuru umezindua jumla ya miradi 6,838 yenye thamani ya takribani tilioni 2.51 ambapo wastani wake  kila mwaka ilikuwa miradi 1,367. Mwaka huu 2017 miradi iliyozinduliwa inahusu sekta ya afya, viwanda, kilimo, elimu, maji yenye thamani ya tilioni 1.1”.

Pia amesema mwenge wa uhuru unaunganisha watanzania na kuimarisha Muungano kwa sababu unakimbizwa katika pande zote za Muungano. Sababu nyingine ya kukimbiza mwenge ni alama ya utaifa wetu na kwa mara ya kwanza mwenge ulikimbizwa tarehe 9 Desemba 1961 wakati Tanganyika ikipata uhuru.

Hata hivyo, rais Magufuli amemwagia sifa nyingi Mwalimu Nyerere akimtaja kama shujaa aliyewaunganisha watanzania wote na kuweka misingi imara ya uongozi likiwemo Azimio la Arusha la mwaka 1967 ambalo lilifutwa na nafasi yake ikachukuliwa na Azimio la Zanzibar.

Anamtaja Mwalimu kama mfano wa kuigwa kwa sababu alithamini utu na usawa wa binadamu akipinga ubinafsi na kukubali kuishi maisha ya kawaida kama watanzania wengine. Alikubali kushauriwa na kukosolewa na kuacha kielelezo kwa viongozi wengine kufuata misingi yake.

 

Maoni ya Wadau juu Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa “ Misingi uliyoiasisi, mawazo na fikra ulizosimamia tunaienzi, ni kazi ngumu ila tutashinda hakika, Tanzania itashinda”.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kupitia Twitter  amewatakia watanzania  wote maadhimisho mema ya kumbukumbu ya 18 ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambapo ameweka nukuu mojawapo ya Mwalimu Nyerere inayosema,

 “Ila nawambieni kama hatutajenga utaratibu wa kutii sheria, kwa sababu tunaongozwa na sheria, siri kubwa ya kuzuia “Udikteta” ni kuongozwa na sheria na hamuwezi kujenga utamaduni wa kuongozwa na sheria kama hiyo haiwi wito wa Taifa, inaeeweka na taifa zima, ni taifa la watu huru”.

Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini, katika kumuenzi Mwalimu Nyerere ameweka nukuu inayoeleza kuwa “ Utii ukizidi unakuwa UOGA. Uoga huzaa unafiki na kujipendekeza, mwisho wake ni mauti”.

Mwalimu Nyerere alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania na alifariki tarehe 14 Oktoba 2017 katika hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza na kuzikwa kijijini kwake Butiama katika mkoa wa Mara.

Sherehe hizo kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha  Mwalimu Julius Nyerere zimefanyika Zanzibar ambapo zimeenda sambamba na kilele cha mbio za Mwenge 2017 na Wiki ya Vijana.  Viongozi wengine walishiriki sherehe hizo akiwemo rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ally Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Kassim Majariwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *