‘Mahekalu’ ya wachimbaji

Kulwa Magwa

MAISHA ya wachimbaji wadogo, katika sehemu nyingi nchini ni ya ajabu. Wengi wanaishi katika mazingira magumu, hupata chakula kwa shida na wakati mwingine baada ya jasho jingi kuwatoka na pia hutumia vilevi vikali – pombe na dawa za kulevya.

Wachache, hata hivyo, katika kundi hilo ndio wanaoishi ‘peponi’ wakiwa katika mazingira ya kazi hayo ya kazi – yaani sehemu za machimbo na mara nyingi watu wa namna hiyo ni viongozi na wasimamizi wa wachimbaji.

Uzoefu nilioupata katika migodi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu wa Sambaru, wilaya ya Ikungi na Londoni, wilayani Manyoni unaonyesha wachimbaji hao wanaishi katika mazingira magumu.

Mathalan, wachimbaji wengi wa sehemu hizo ambao wameweka kambi katika maeneo ya migodi, wanaishi kwenye nyumba za aina hii ambazo wenyewe wanapenda kuziita ‘mahekalu’.

hekalu

Mojawapo wa 'hekalu' la wachimbaji wa Sambaru

Wanaziita hivyo wakimaanisha ni sawa na makazi mengine ya watu wanaoishi vizuri, na maana nyingine ya kauli yao inawapa hamasa ya kujituma kusaka fedha na wapatapo au wanapopata – watajenga nyumba nzuri zinazolingana na mahekalu ya matajiri.

Hata hivyo, cha ajabu ni kwamba ‘mahekalu’ hayo ya migodini hurithishana miongoni mwa wachimbaji, ambapo anayeamua kurejea kwao, kuachana na uchimbaji au kupata alichofuata – humuachia ‘hekalu’ mchimbaji mwenzake hasa aliye naye karibu.

Mmoja wa wachimbaji wa Sambaru, Hassan Said, aliniambia mahekalu hayo yapo mengi, lakini yamejengwa mbali-mbali kutokana na usiri wanaoufanyiana wachimbaji hao.

Hassan Said

Hassan Said

“Shughuli zetu ni kuchimba na mtu anapopata (dhahabu) hawezi kukuambia kapata, ndiyo maana ya makazi haya – yaani mtu anafanya mambo yake kwa siri katika eneo lake au makazi yao, “ anasema mchimbaji huyo.

Said anasema, miaka mingi iliyopita ‘hekalu’ moja lilikuwa linatumiwa na mchimbaji mmoja, lakini kutokana na ongezeko la wachimbaji, hivi sasa wachimbaji watatu hadi watano walala pamoja katika ‘vibanda’ hivyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *