HUKUMU ya Kesi ya Kikatiba kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crimes Law) iliyofunguliwa na kampuni ya Jamii Media dhidi ya Jamhuri imeshindwa kusomwa leo.
Kesi hiyo iliyoko Mahakama Kuu iko mbele ya jopo la majaji watatu chini ya Mwenyekiti Jaji Winfrida Koroso akisaidiwa na Jaji Ignas Kitusi na Jaji Khalfani.
Wakili wa Jamii Media, Benedict Ishabakaki, amesema sababu za kushindwa kusomwa kwa hukumu ya kesi hiyo hazikuweza kuwekwa wazi mara moja, hivyo wameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya hukumu.
“Tumekuja hapa, lakini tumeelezwa kwamba hakukuwa na taarifa yoyote kuwa kesi hiyo Namba 9/2016 ingetolewa hukumu leo, ni jambo la kusikitisha kwa sababu sisi tulipewa taarifa rasmi muda mrefu,” alisema wakili huyo.
Hata hivyo, habari zisizo rasmi zinaeleza kwamba, huenda kuhamishwa kwa Jaji Koroso kwenda Mahakama ya Mafisadi nako kumechangia, ingawa wajuzi wa masuala ya kisheria wanasema hicho kisingeweza kuwa kipingamizi kwa kuwa kama hukumu ilikuwa tayari, ingeweza kusomwa na jaji yeyote, hata Msajili wa Mahakama Kuu.
Jamii Media inayoendesha mtandao maarufu wa JamiiForums na gazeti tando la FikraPevu.com ilifungua kesi hiyo mnamo Machi 4, 2016 katika Mahakama Kuu ya Tanzania ikipinga baadhi ya vifungo vilivyomo katika Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Hoja ambazo Jamii Media imezitoa katika mwenendo wa kesi hiyo ni:
– Kupinga matumizi ya kimabavu ya kifungu cha 32 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime Act), ambacho kimebainika kutoa nguvu kubwa kwa Jeshi la Polisi kutoa amri ya uchunguzi wa taarifa za siri/binafsi za watumiaji wa mitandao.
– Kupinga matumizi ya kifungu cha 38 cha Sheria ya Makosa ya Kimtadao ambacho kinapingana na haki ya mtu kusikilizwa endapo kifungu cha 32 kitakuwa kimetumika. Kifungu cha 38 kinalipa Jeshi la Polisi uwezo wa kwenda mahakamani na kusikilizwa bila uwepo wa upande wa pili (Exparte).
Taarifa kutoka Jamii Media zinaeleza kwamba, hata ikitokea Mahakama ikaona kifungu cha 32 kiko sawa kikatiba, lakini wao wanapinga 'Matumizi mabaya' ya kifungu hicho.
Wanasheria wa Jamii Media wanasema kwamba, Jeshi la Polisi lilianza kutumia kifungu hicho bila kanuni kutungwa na kwamba kifungu hicho cha 32 kinakinzana na haki ya faragha na uhuru wa kujieleza.
Katika mwenendo wa kesi hiyo kwenye hatua za awali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliweka mapingamizi sita ya awali ya kisheria, ambapo katika mojawapo ya mapingamizi hayo Mwasheria wa Serikali alisema shauri hilo halikustaili kuwa la kikatiba.
Aidha, katika mapingamizi (Preliminary Objections) hayo sita, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ilitaka kesi nzima ifutwe na Jamii Media walipe gharama zilizoingiwa.
Hata hivyo, Agosti 24, 2016, Mahakama Kuu iliyatupilia mbali mapingamizi yote sita ya awali na kutoa amri kesi hiyo kuendelea kusikilizwa.
Tangu kutungwa kwa Sheria ya Makosa ya Kimtandao 2015, Jeshi la Polisi kupitia Kitengo chake cha Makosa ya Kimtandao "Cybercrimes Unit" na cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai "Criminal Investigation Department (CID)" wanadaiwa kuwa wakituma barua mbalimbali wakimtaka Mkurugenzi wa Jamii Media kuwapa taarifa za siri/binafsi za wateja wake kwa lengo la 'kufanya uchunguzi' na 'kuwafungulia kesi' baadhi ya watumiaji wa mtando huo.
Polisi walikuwa wakituma barua hizo chini ya kifungu cha 32 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao.
Katika barua hizo zaidi ya kumi, zote zilikuwa zikitaka taarifa za watu walioandika masuala ambayo Jamii Media wanadai yana maslahi mapana ya kitaifa (Public interest) na nyingne zikiwa za kisiasa.
Aidha, barua zote za Jeshi la Polisi ziliweza kujibiwa na wanasheria wa Jamii Media, huku wanasheria hao wakionyesha nia ya kutoa ushirikiano endapo Jeshi la Polisi lingesema wazi makosa yaliyokuwa yametendeka na kama wangeeleza taarifa hizo za wateja zinakwenda kutumika kwa maslahi gani.
Inaelezwa kwamba, hiyo ilifanyika kwa nia njema (Good faith) ili kuiwezesha Jamii Media kupitia JamiiForums kuangalia uhalali wa kisheria kabla ya 'kutoa ushirikiano' kwa Jeshi hilo.
Mwanasheria wa kampuni hiyo, Benedict Ishabakaki, pia alinukuliwa nyakati kadhaa akisema watumiaji wengi waliokuwa wakitafutwa walikuwa wameandika habari au kutoa taarifa za rushwa, ufisadi na ukwepaji kodi na hivyo aliishauri Jamii Media kuwaona kama waibua maovu “Whistle Blowers” wenye nia njema kwa nchi.
JamiiForums inasema kwamba ina wajibu wa kulinda taarifa za watumiaji wake kisheria na Kikatiba, lakini pia wanatambua wana wajibu wa kisheria kutoa ushiriakiano kwa Mamlaka kama kuna taarifa watahitaji, lakini lazima maombi hayo yafanywe chini ya amri zilizo halali na zinazofuata sheria na kuzingatia haki za binadamu.
Inaelezwa kuwa, pamoja nia ya kutaka kutoa ushirikiano iyoonyeshwa na Jamii Media kwa Jeshi la Polisi katika barua zao zote zaidi ya kumi, Polisi walikataa kutoa taarifa juu ya nia ya Jeshi hilo kwa wateja wao.
Aidha, Polisi walizidi kutuma barua na mnamo Februari 4, 2016, Jeshi la Polisi lilimuandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo, barua ya kuashiria kuwa lina nia ya kumshtaki chini ya kifungu cha 22 kwa madai ya kuzuia uchunguzi wa Jeshi la Polisi.
Kufuatia vitisho hivyo vya kufunguliwa mashtaka, uongozi wa Jamii Media ulishauriana na wanasheria wao na kuamua kufungua Kesi ya Kikatiba.
Tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo, Jeshi la Polisi lilisitisha kwa muda kuandika barua hadi mwezi Septemba 2016 walipomhoji Maxence juu ya barua walizokuwa wakimwandikia na akiwanyima 'ushirikiano'.
Ulitokea ukimya wa Polisi tena hadi Disemba 13, 2016 walipomkamata Bw. Maxence Melo na kumnyima dhamana kwa siku takribani nne (4) na kumfungilia mashtaka chini ya kifungu cha 22 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao huku Jeshi hilo likijua wazi kuna kesi ya Kikatiba kuhusiana na suala hilo.