Manji ajiweka kuwa adui wa Uhuru wa Habari TZ -1

Jamii Africa

Endapo mahakama zitaendelea kukubali maombi ya mfanyabiashara maarufu nchini Bw. Yusuph Manji ya kutaka kuzuia habari zake kuandikwa au kuonekana kwenye vyombo vya habari kadha wa kadha  nchini basi zitakuwa zinashiriki kwa makusudi katika mashambulizi ya wazi, dhahiri na ya makusudi dhidi ya uhuru wa habari nchini.

Bw. Manji ametajwa tangu mwaka 2006 kuwa anahusika moja kwa moja na mojawapo ya wizi wa mabilioni ya shilingi za Kitanzania kutoka benki kuu kwenye akaunti ya masalio ya madeni ya nje maarufu kama EPA. Kwa kupitia kampuni ya Kagoda Agricultural Limited Bw. Manji (Pichani) na kampuni zake kadhaa amejikuta akitajwa tajwa na kuhusishwa na wizi huo na wiki chache tu zilizopita yeye mwenyewe alikiri kuwa ni kweli alinufaika na fedha hizo za wizi – japo alidai kuwa alizirudisha baada ya kubanwa na serikali.Baada ya kashfa ya EPA kuibuliwa mwishoni  mwa mwaka 2005 na hasa baada ya kelele za wanaharakati

kikosi kazi kiliundwa kwa ajili ya kufuatilia undani wa kashfa hiyo. Kabla kikosi hicho hakijakamiliza kazi yake Gavana wa   Benki Kuu Bw. Daudi Ballali- shahidi muhimu wa wizi wa EPA akatoroshwa nchini. Huku nyuma badala ya kuachilia kutumika kwa mfumo wa upepelezi wa makosa ya jinai ukachaguliwa mfumo wa kisiasa ambao ulikuwa nje ya taratibu za uchunguzi wa uhalifu nchini yaani kutumia  kikosi kazi ambacho kiliundwa na Ikulu badala ya DPP. Kuundwa kwa kikosi kazi hicho kulisababisha baadhi ya watu kuhoji uwezo wake kisheria kuweza kusaka wahalifu. Hata hivyo hakukuwa na mapingamizi yoyote na wasomi na taasisi mbalimbali ziliridhika na mfumo huo. Kati ya majukumu yake mbalimbali kikosi hicho ilikuwa ni kuhakikisha kuwa fedha zote zilizoibwa toka akaunti hiyo ya EPA ambazo zilizidi dola milioni 133 zinarudishwa mara moja na wahusika wake wote kufikishwa mahakamani.

Hata hivyo tume iliyoundwa haikufata mara moja mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ambaye aliyatoa katika ripoti yake ya uchunguzi wa akaunti za Benki Kuu kufuatia wizi huo wa EPA. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG ambayo ilizingatia yaliyokutwa na kampuni ya ukaguzi ya Ernst and Young mambo kadhaa yalitakiwa kufanyika.

Kipengele 4.1 cha ripoti hiyo ya “SIRI” ambayo FikraPevu inayo nakala yake kinasema kuwa CAG amependekeza kwamba “The government should institute a formal criminal investigation by competent law enforcing agencies  against the 13 assignee companies and  (their) directors, and the officials of BoT involved in the fraudulent payments  amounting to TZS 90,359,078,804.13 whose results should form the basis of further action”

Zaidi ya yote yote kipengele kinachofuatia kinasema kuwa “The government should consider initiating legal procedures aiming at recovery of the funds paid to the 13 companies that undeservedly received a total of TZS 90,359,078,804.13. Initially, this can take a form of temporary bank accounts and assets freeze process pending the completion

of formal criminal investigation process by competent law enforcing organs.” Baadhi ya wahusika wa wizi huu wa EPA tayari wamefikishwa mahakamani isipokuwa wale wa Kagoda Agriculture Limited ambao serikali ilidai kuwa hawajulikani. Kwa muda mrefu tetesi zimekuwepo nchini zikiwahusisha aliyekuwa Mbunge wa Igunga Bw. Rostam Aziz (CCM) na Bw. Yusuph Manji kuwa ndio wahusika wakuu wa kampuni ya Kagoda.

Kwa muda mrefu majina ya Manji na Rostam (pichani) yalihusishwa na kampuni hii hasa kutokana na wao wenyewe au makampuni yao kuonekana kwa namna moja au nyingine kuwa ndio walinufaika na fedha za Kagoda. Lakini zaidi kuhusishwa kwao kumekuja baada ya baadhi ya wadau wakubwa wa harakati za mabadiliko nchini kuweka hadharani kile kinachodaiwa kuwa ni ushahidi “usio na shaka” wa kuhusika kwa wafanyabiashara hawa wawili rafiki na wizi wa EPA na zaidi kushindwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Eliezer Feleshi kuanzisha uchunguzi wake au kuleta mashtaka dhidi yao katika kipindi chote tangu kashfa ya EPA ianze.

Wakati DPP Feleshi akijiweka kando na kusubiri maelekezo “kutoka juu” na kusahau wajibu wake aliopewa kwa mujibu wa Katiba na Sheria Bw. Manji ameamua kuanzisha mashambulizi ya wazi, dhahiri na ya makusudi dhidi ya uhuru wa habari nchini. Mashambulizi hayo kwa kiasi fulani yamefanikiwa kuvitisha vyombo vya habari nchini kuandika habari zozote kuhusu Manji vikihofia kuonekana vinakiuka “amri halali” ya mahakama.

Fikrapevu itakuletea kwa kina sakata la Manji kutumia mahakama kujaribu kuminya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa Watanzania kupata na kujadili habari kwani mambo ambayo anayadai mahakama iamuru (na baadhi ya mahakama za chini zimekubali) yanatishia haki na uhuru siyo tu wa kuzungumza bali pia yakikubalika bila kukosolewa yatatishia uhuru wa kifikra.   

 

Mahmoud Rashid

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *